Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KIVULINI YAWATAKA WANAUME KUFICHUA UKATILI WA KIJINSIA WANAOFANYIWA


Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kutetea Haki za Wanawake na Watoto KIVULINI, Yassin Ally (pichani) amewataka wanaume wanaotendewa vitendo vya ukatili wa kijinsia na wake zao kujitokeza na kufichua ukatili huo ili hatua stahiki zichukuliwe kuutokomeza.

Ally ametoa rai hiyo wakati akizungumza kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika kwa ngazi ya Mkoa Mwanza katika uwanja wa Nyamagana, Machi 08, 2022.

Amesema kuna baadhi ya wanaume wanafanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo vipigo na kunyimwa unyumba lakini wananyamaza ambapo amewasihi kuripoti ukatili huo katika ngazi mbalimbali ikiwemo madawati ya jinsia pamoja na mashirika ya kutetea haki za binadamu kwa ajili ya usuluhishi.

Ally amebainisha kuwa kundi la wanaume ni miongoni mwa makundi yanayoathirika na vitendo vya ukatili wa kijinsia lakini wengi wao huamua kukaa kimya na kufa na tai shingoni bila kutoa taarifa.

Amewashauri wazazi kuwalea watoto katika misingi bora ikiwemo kuwaandaa watoto wao wa kiume ili wawe na ujasiri wa kutonyamazia ukatili wa kijinsia hatua itakayosaidia kujenga kizazi chenye usawa wa kijinsia.

Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Ngusa Samike amewahimiza wanawake kuwa mstari wa mbele kushirikiana na wenza wao katika masuala ya maendeleo ikiwemo kushiriki ipasavyo kwenye zoezi la Sensa linalotarajiwa kufanyika Mwezi Agosti mwaka huu.

Aidha ametumia fursa hiyo kuwahimiza wanawake kuwashawishi wanaume zao ambao hawajafiwa tohara kuwa tayari kufanyiwa tohara salama inayotolewa katika Vituo mbalimbali vya afya hatua itakayowasaidia kujikinga na maambukizi ya virusi vya UKIMWI.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI, Madawa ya Kulevya na Magonjwa yasiyoambukiza, Fatma Tawfiq amewataka wanawake kuwa na sauti ndani ya mahusiano yao ikiwemo kusisitiza matumizi ya kinga ili kupambana na maambukizi ya VVU/ UKIMWI.

Tawfiq pia amewahimiza wanawake kuchangamkia fursa za mikopo ya asilimia 10 iyotolewa katika Halmashauri kwa ajili ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi kwa kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo na kuepukana na utegemezi unaosababisha baadhi yao kujihusisha na biashara haramu ya ukahaba.

Akisoma risala kwa niaba ya wanawake mkoani Mwanza, Tunu Kimea amesema bado wanawake wanakumbana na changamoto mbalimbali na kuomba Serikali kuunga mkono jitihada zinazofanywa na wadau kutokomeza changamoto hivyo ikiwemo vitendo vya ukatili wa kijinsia pamoja na miundombinu siyo salama katika maeneo ya kufanyia biashara.

Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Katibu Tawala Mkoa Mwanza, Ngusa Samike akizungumza kwenye maadhimisho hayo.
Mkuu wa Wilaya Nyamagana, Amina Makilagi akitoa salamu kwenye maadhimisho hayo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI, Madawa ya Kulevya na Magonjwa yasiyoambukiza, Fatma Tawfiq akitoa salamu kwenye maadhimisho hayo.
Mkurugenzi Shirika la KIVULINI, Yassin Ally akihamasisha Maandamano ya Siku ya Wanawake Duniani 2022.
Wadau mbalimbali wakiwasili kwenye uwanja wa Nyamagana kushiriki Siku ya Wanawake Duniani.
Viongozi mbalimbali wakiwasili kwenye maadhimisho hayo akiwemo Mkuu wa Wilaya Nyamagana, Amina Makilagi (kulia).
Viongozi mkoani Mwanza wakifurahia burudani kwenye maadhimisho hayo.
Wadau mbalimbali wakiwa kwenye maadhimisho hayo.
Burudani ya kucheza na nyoka.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com