SERIKALI YAELEZA TIBA ASILI ILIVYOWABEBA WATANZANIA KWA MIAKA 2 VITA DHIDI YA COVID-19

 

Waziri wa Afya nchini Ummy Mwalimu akiongea na Waandishi wa habari kuhusu hali ya ugonjwa wa virusi vya Corona tangu kuripotiwa kwake miaka miwili iliyopita.


Na Dotto Kwilasa, Malunde1 Blog-DODOMA.

SERIKALI kupitia Wizara ya afya  imesema inatambua mchango wa tiba asili nchini katika kipindi chote cha mapambano dhidi ya ugonjwa wa Corona hivyo kuona umuhimu wa kuimarisha zaidi huduma hizo kwa kuongeza ubora ili kuongeza wigo wa upatikanaji wake. 

Hayo yameelezwa leo Jumatano, Machi 16, 2022,Jijini Dodoma na Waziri wa afya Ummy Mwalimu wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu hali ya ugonjwa wa virusi vya Corona (Uviko-19) miaka miwili tangu kuripotiwa kwake kwa mara ya kwanza hapa nchini na kueleza kuwa tiba asili ni sehemu ya  mchango wa matumaini.

Kutokana na umuhimu huo ,Waziri Ummy amesema Wizara hivyo inatarajia kuanzisha mashamba ya mitidawa kwa kushirikiana na Taasisi ya Taifa ya utafiti wa magonjwa ya binadamu(NIMR)kuona namna ya kufanya Ili kufanikiwa Katika hili ikiwa ni pamoja na kuendelea kusajili vituo vinavyotoa tiba asili, wataalamu ili kuleta tija katika sekta ya tiba asili kuwa na mashiko.

"Niseme ukweli,tiba asili imewabeba Sana wananchi katika kipindi chote cha mapambano ya Corona na bado inaendelea kuwa na thamani, ilikuwa nisehemu ya kuwapa matumaini wananchi na kupona,tiba hii imetuondolea presha wizara ya afya hasa tuliposikia kuwa inawezekana tukapokea wagonjwa laki moja kwa siku nikasema hivi tutawalaza wapi;?amehoji Waziri Ummy na kuongeza;

Tukitumia muda kufikiria cha kufanya mpaka tukaandaa na uwanja mkubwa Kwa ajili ya kuwalaza wagonjwa lakini Kutokana na tiba hii baadhi ya wagonjwa hawakuja moja kwa moja Hospitali na badala yake walitulia na kuendelea kutumia tiba mbadala kwa kushauriwa na wataalamu wetu na sasa imeendelea kuwasaidia walio wengi nchini ,"amesema.

Hata hivyo ameonya kwamba dawa hizo zinapaswa kutumika baada ya kufanya utafiti na kugundua kuwa hazina kemikali zenye athari kwa binadamu  hali itakayoleta afueni  hasa katika maeneo ya vijijini.

Katika hatua nyingine Waziri huyo amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kukabiliana na uvico 19 kwa kuzingatia mazingira yaliyopo ili  kuwapa wananchi nafasi kuendesha shughuli za uchumi bila kuathirika.

Amezitaja hatua ambazo zimechukuliwa  na Serikali  katika kupambana na UVIKO19 kwa kiasi kikubwa kuwa  zimezingatia mazingira na hali ya jamii ya watanzania ikiwemo kuruhusu wananchi kuendelea kujitafutia kipato chao (yaani kutokuwa na lockdown) na hivyo kupunguza hofu na kunusuru uchumi wa jamii na Taifa kwa ujumla. 

Amesema hadi kufikia tarehe 15 Machi 2022, jumla ya watu 33,789 wamethibitika kuwa na maambukizi ya UVIKO - 19 na watu 803 wamepoteza maisha nchini.

"Katika kipindi hiki pia tumeweza  kuongeza wigo wa uchunguzi wa kimaabara wa UVIKO-19 ambapo kwa sasa kuna maabara saba ndani ya nchi zenye uwezo wa kupima UVIKO19 kulinganisha na Maabara moja ya Afya ya Jamii iliyokuwepo wakati wa kulipuka kwa ugonjwa huu mwezi Machi 2020,

Maabara hizi ni pamoja na Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii, Maabara katika Hospitali za Kanda za Bugando, Mbeya na Maabara katika Hospitali za Rufaa za Mikoa ya Dodoma, Arusha, Kigoma, na Maabara iliyopo katika Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro.

Aidha, Serikali imesimika mitambo 15 ya hewa tiba ya Oksijeni katika Hospitali mbalimbali nchini ili kuweza kutoa huduma za wagonjwa mahututi wanaohitaji uangalizi maalum. Ndugu Wananchi, Serikali pia imeendelea kuikinga jamii kwa kuwezesha upatikanaji wa chanjo ya UVIKO-19 nchini, ambapo hadi kufikia tarehe 12 Machi 2022, jumla ya watu 2,820,545 wenye umri wa miaka 18 na kuendelea, wamepata chanjo kamili dhidi ya ugonjwa huu,"amefafanua 

Sambamba na hayo Waziri Ummy pia ametumia nafasi hiyo kueleza hali ya kiwanjo cha uchanjaji Kimikoa kwamba, Ruvuma (23%), Katavi (14%), Dodoma (13%), Mtwara (12%), Mara (11%), Mwanza (11%), Lindi (10%), Dar-es-Salaam (10%), Simiyu (10%), Pwani (9), Kilimanjaro (9%), Kagera (9%) na Mbeya (9%) , Arusha (8%), Geita (7%), Shinyanga (7%), Iringa (7%), Njombe (7%), Rukwa (6%), Morogoro (6%), Tanga (5%), Kigoma (5%), Tabora (5%), Singida (5%), Songwe (4%) na Manyara (3%).

Ameweka wazi kuwa kwa kuzingatia hali hiyo,Mikoa inahitaji kuongeza juhudi katika kuhimiza wananchi kujitokeza kuchanja na kwamba licha ya  kuonekana kupungua kwa ugonjwa huu kwa sasa,wananchi wanapaswa kuelewa kuwa ugonjwa huu hutokea kwa mtindo wa mawimbi ambayo yanaambatana na mabadiliko mbalimbali ikiwemo kuibuka kwa anuai mpya za kirusi, kubadilika kwa dalili, kuongezeka makali ya ugonjwa na kubadilika kwa njia mahususi za kukabiliana nao. 

"Lazima tuwe na tahadhari,ndani ya wiki hii kumeripotiwa taarifa ambazo bado hazijathibitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusu kuibuka kwa aina mpya ya kirusi cha COVID19 katika nchi za China, South Korea na Japan,Wizara ya Afya inaendelea kuwasiliana na Shirika la Afya Duniani kuhusu suala hili sambamba na kuendelea kuimarisha ukaguzi na ufuatilia wa wasafiri wanaongia nchini kwetu,"amefafanua. 

Hata hivyo kwa kuzingatia hali ya sasa ya maambukizi ya UVIKO-19 nchini na mwenendo wa ugonjwa huu duniani, Serikali imelegeza masharti kwa Wasafiri wanaoingia nchini ambao wamekamilisha dozi ya chanjo ya UVIKO-19 hivyo kuanzia kesho tarehe 17/03/2022 wanaondolewa hitaji la kuwa na cheti cha kipimo cha kuthibitisha kutokuwa na maambukizi (negative RT - PCR certifícate) kilichokuwa kikihitajika hapo awali.

"Masharti haya na masharti mengine yataainishwa kwenye mwongozo wa wasafiri ambao utakuwa ukibadilika kulingana na mwenendo wa maambukizi ya ugonjwa huu nchini na duniani kwa ujumla,"amesisitiza Waziri Ummy na kuongeza;

"Mwelekeo wetu kwa sasa ni kuendelea kutoa huduma za kudhibiti UVIKO-19 kupitia huduma nyingine jumuishi za afya kama vile Kifua Kikuu, huduma za mama na mtoto, huduma za VVU/UKIMWI, huduma za malaria, huduma za magonjwa yasiyoambukiza na kadhalika ;

"Tunaongeza wigo wa uchunguzi wa kimaabara katika Mikoa yote nchini na hivyo kuhakikisha upatikanaji wa majibu ya wagonjwa kwa wakati, huduma za kipimo cha haraka (COVID-19 Rapid Antigen Test) zitaanza kutolewa ndani ya wiki moja katika vituo mbalimbali vya huduma za afya nchini na kuimarisha upatikanaji wa dawa na vifaatiba muhimu katika kukabiliana na ugonjwa huu ikiwemo kuimarisha huduma za wagonjwa mahututi na wanaohitaji uangalizi maalumu,"amesema


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post