Wizara ya ulinzi ya Urusi imetoa taarifa kuhusu vifo va wanajeshi wake pamoja na majeruhi – kwa mara ya pili tu – ikidai kuwa wanajeshi wake 1,351 wameuawa na wengine 3,825 kujeruhiwa, shirika la habari la Ria Novosti linaripoti.
Vyanzo vya kijeshi vya Ukraine vimekadiria kuwa wanajeshi 15,000 wa Urusi wameuawa, ingawa idadi hiyo inaweza kujumuisha majeruhi pamoja na vifo. Idara ya ujasusi ya Marekani imesema huenda wanajeshi wa Urusi waliouawa katika vita hiyo ni zaidi ya nusu ya idadi hiyo inayodaiwa na Ukraine.
Taarifa ya kwanza kutoka wizara ya ulinzi ya Urusi kuhusu majeruhi ilikuwa tarehe 2 Machi, na ilisema kuwa wanajeshi 498 waliuawa tangu uvamizi huo ulioingia mwezi wa pili sasa.
Gazeti la Komsomolskaya Pravda (KP) lilichapisha makala mtandaoni iliyonukuu wizara ya ulinzi ikisema wanajeshi 9,861 wa Urusi waliuawa katika mzozo huo.
Baadaye, sehemu ya makala hiyo iliondolewa na mhariri wa KP aliiambia BBC kuwa taarifa hizo zilitokana na udukuzi.
Social Plugin