Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAFUASI WA MHUBIRI ANAYEJIITA 'MFALME ZUMARIDI' WAANZA KUSALIMU AMRI



WAFUASI wa mhubiri anayejiita Mfalme Zumaridi, Diana Bundala wameendelea kuomba kupewa dhamana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Mwanza, baada ya hapo awali kugomea wakisema wanampa faraja kiongozi wao huyo ambaye yuko mahabusu.

Akiahirisha kesi hiyo leo, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Mwanza, Stella Kiama amesema shauri hilo litatajwa tena Aprili 18, mwaka huu, baada ya kutokuwepo kwa Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, aliyeanza kusikiliza kesi hiyo tangu awali, Monica Ndyekobora kutokana kuwa safarini.


Watuhumiwa wanane ambao ni wafuasi wa Zumaridi wamepata dhamana baada ya kukataa kupatiwa dhamana siku ya kwanza kesi hiyo ilipotajwa, kwa madai ya kukaa na mhubiri wao pamoja hadi atoke.


Kwa sasa watuhumiwa waliobaki ni wanane ikiwa ni mabadiliko, baada ya kubadili misimamo yao ya awali waliyojiwekea ya kuendelea kukaa na mhubiri huyo.


Wakili wa upande wa walalamikiwa Erick Muta amesema, wafuasi wengine saba wanakamilisha taratibu za kuomba kupata dhamana, ili waweze kutoka mahabusu.


Mhubiri huyo wa Kanisa la Zumaridi, alikamatwa na kufikishwa mahakamani hapo Februari mwaka huu kwa makosa ya usafirishaji na utumikishaji wa watu kwa kisingizio cha imani ya dini, ambapo ilipotajwa kwa mara ya kwanza ilielezwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza shauri hilo na kuahirishwa.


Mfalme Zumaridi ni nani?


Mwaka 2019, mwana mama huyo anayejiita Mfalme Zumaridi alijizolea umaarufu mkubwa kutokana na alivyokuwa akiendesha ibada huko jijini Mwanza tofauti na makanisa mengine yanavyoendesha ibada.


Aina yake ya uendeshaji wa ibada ulikuwa gumzo kwani Mfalme Zumaridi haamini katika aina yeyote ya dini hali inayoleta maswali hadi sasa.


Mwana mama huyo anayejiita Mfalme ana wafuasi wengi wanaomuamini, na wanamwamini kama Mfalme Zumaridi na kama mwakilishi wa mungu duniani ama yesu kristo wa duniani.


Aidha, wakati fulani wafuasi wake hulala chini huku mchungaji wao akiwakanyaga na kupita juu yao, wakati mwingine waumini wa kanisa hilo pia huonekana wakigaragara kwenye matope ya majaruba ya mpunga jirani na kanisa lao kama moja ya ibada ikiwa ni ishara ya kumshughulikia shetani.


Baada ya kuonekana video mbalimbali za mahubiri yake kanisani kwake, Serikali iliingilia kati na ndipo ikachukua uamuzi wa kulifungia kanisa la Mfalme Zumaridi, ambapo pia iliamuru kutofanyika ibada kanisani hapo wala nyumbani kwa Mfalme Zumaridi.


Hatua hii pia ilikuwa ni baada ya uchunguzi kubaini kuwa baadhi ya maneno na matendo yalikuwa yakifanyika kanisani kwa Mfalme Zumaridi yalikuwa na athari na madhara kwa waumini na watu wengine pamoja na umnwepo wa malalamiko kutoka kwa wananchi na viongozi wa taasisi zingine za kidini kuhusu ukiukwaji wa sheria, maadili na imani ya kidini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com