Mkazi wa Kijiji cha Upungu Wilaya ya Nzega mkoani Tabora, Jacob Mlela (88) ameuawa kwa kukatwa na shoka kichwani, shingoni na mikononi na mtoto wake Michael Jacob kwa kile kinachotajwa kuwa ni imani za kishirikina.
Akizungumza na waandishi wa habari Jumatano Machi 2,2022 Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora, Richard Abwao amesema kuwa tukio hilo limetokea juzi saa moja jioni katika eneo hilo, ambapo marehemu alishambuliwa akiwa nje ya nyumba yake na kukimbizwa hospitali ya Ndalla na kufariki dunia.
Amesema chanzo cha mauaji hayo ni imani za kishirikina, kwani mtuhumiwa ana tatizo la kuanguka kifafa na amekuwa akiamini kuwa baba yake ndio chanzo cha yeye kuugua ugonjwa huo.
"Mtoto anaugua ugonjwa wa kifafa ambao anaamini baba yake ndiyo chanzo cha yeye kuugua na kuchukua maamuzi hayo," amesema.
Mbali na baba yake, mtuhumiwa pia alimjeruhi ndugu yake, Magdalena Jacob ambaye kwa sasa anaendelea vizuri akiwa anapata matibabu.
Kamanda Abwao ametoa wito kwa wananchi mkoa wa Tabora kutoendekeza imani za kishirikina na wanapokuwa wanaumwa waende kuwaona wataalamu katika Vituo vya kutokea huduma.
CHANZO: Mwananchi