MRADI WA MAJI KIBARA WAWAONDOLEA ADHA WANANCHI KUTEMBEA KM 30 KUFUATA MAJI ZIWANI


Mradi wa Maji Kibara
Meneja RUWASA wilaya ya Bunda,William Boniface


Na Dinna Maningo,Bunda.

WANANCHI kijiji cha Kibara kata ya Kibara wilayani Bunda mkoa wa Mara,wamepata huduma ya maji ya bomba ambapo awali walilazimika kutembea umbali km 30 kufuata maji Ziwa Victoria na hivyo kuathiri shughuli zao za kijamii.

Wakizungumza na Waandishi wa Habari,Mwenyekiti wa kamati ya Jumuiya ya watumiaji wa maji kata ya Kibara,Robert Mgono alisema kuwa mradi wa maji Kibara ulianzishwa 1972 na ulistisha kutoa maji baada ya miundombinu ya maji kuchakaa.

"Wateja wanaotumia maji ya bomba ni 263 bado maeneo mengine hayajasambaziwa maji wanachota kwenye  vituo mbalimbali vinavyotoa huduma ya maji na wengine wanachota kwenye visima vya asili,mradi ulisimama baada ya miundombinu kuchakaa tunaipongeza Serikali kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira vijijini (RUWASA)wametujengea mradi na maji yamesambwazwa kwenye vituo 29 vya kutolea maji", alisema Mgono.

Mkazi wa kijiji hicho Lucy Paul alisema kuwa upatikanaji wa huduma hiyo ya maji umewezesha kufanya shughuli za kilimo kwa wakati kulima bustani za mbogamboga kwakuwa kuna maji ya kutosha kumwagilia,aliomba kuongezwa kwa vituo vingine vya maji  na kuyasambaza majumbani ili kuwafikia wananchi wote.

Fundi Mradi Evodis Rwegasha alisema kuwa bado kuna changamoto ya mapato yatokanayo na huduma ya maji kwakuwa watu wengi wamechimba visima na wanachota maji ya bomba pindi tu kunapotokea kiangazi baada ya visima kukauka hali ambayo inashusha mapato ya fedha kwakuwa shughuli zote za uendeshaji wa mrandi yakiwemo malipo ya umeme na malipo mengine hutegemea fedha ambazo wananchi hulipa wakati wanapochota maji.

Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mhandisi William Boniface,alisema kuwa mradi wa maji Kibara unahudumia watu 21,000 umegharimu sh. Milioni 558,kuna vituo 29 vya maji,nakwamba katika mwaka wa fedha 2021/2022 wilaya hiyo ya Bunda imepatiwa Bilioni 5.9 kutekeleza miradi ya maji 15 ambayo itakamilika juni 20,2022.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post