Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

OFISI YA RAIS, UTUMISHI YAZINDUA MFUMO WA KIELEKTRONIKI WA TATHMINI YA HALI YA RASILIMALI WATU

Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Jenista Mhagama akiongea na Waandishi wa habari na baadhi ya Viongozi wa Umma wakati akizindua Mfumo wa kielektroniki wa tathmini ya hali ya rasilimaliwatu katika Taasisi za Umma huku ikiagiza waajiri wote kusimamia Wakurugenzi au Wakuu wa Idara zinazosimamia Rasilimaliwatu katika taasisi zao ili wakamilishe zoezi hilo ifikapo tarehe 31 Machi, 2022.
Waziri wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na utawala bora Jenista Mhagama akizindua mfumo wa kielektroniki wa tathmini ya hali ya rasilimaliwatu katika Taasisi za Umma  unaolenga kuwezesha kukusanya, kuchakata na kuchambua taarifa za Watumishi kwa njia ya kisayansi ili kubaini mahitaji halisi ya Watumishi katika Wizara na Taasisi za Umma.
Baadhi ya viongozi na  Watumishi wa Umma wakisikiliza Waziri Ofisi ya Rais, utumishi Jenista Mhagama (hayupo pichani)wakati akizungumzia mfumo wa kielektroniki wa tathmini ya hali ya rasilimaliwatu katika Taasisi za Umma Katika Ofisi Mtumba Jijini Dodoma
**

Na Dotto Kwilasa-Malunde 1 blog-DODOMA

OFISI ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, imezindua Mfumo wa kielektroniki wa tathmini ya hali ya rasilimaliwatu katika Taasisi za Umma huku ikiagiza waajiri wote nchini kusimamia Wakurugenzi au Wakuu wa Idara zinazosimamia Rasilimaliwatu katika taasisi zao ili wakamilishe zoezi hilo ifikapo tarehe 31 Machi, 2022. 

Hayo yamejiri leo Machi 23,2022 Jijini hapa na Waziri wa Wizara hiyo Jenista Mhagama wakati akizindua mfumo huo unaolenga kuwezesha kukusanya, kuchakata na kuchambua taarifa za Watumishi kwa njia ya kisayansi ili kubaini mahitaji halisi ya Watumishi katika Wizara na Taasisi za Umma. 

Waziri huyo amesema kwa taasisi zilizo nje ya Mfumo wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara katika Utumishi wa Umma (HCMIS) zilipelekewa nyenzo ya kukusanya taarifa ambazo zitaingizwa kwenye Mfumo wa Kielektroniki kwa ajili ya kuchakatwa zaidi. 

Akizungumzia mfumo huo amesema zoezi hilo litatusaidia katika kutathmini hali halisi ya Watumishi waliopo na wanaohitajika katika taasisi zote za umma ili kuweza kuwapanga kwa kuzingatia mahitaji halisi ya kila taasisi na kwamba Serikali itakuwa na taarifa na takwimu sahihi kuhusu watumishi waliopo, mahitaji ya watumishi wanaohitajika katika kutekeleza majukumu ya kuwahudumia wananchi.

"Matarajio ya zoezi hili ni kuweka msawazisho wa Watumishi wa Umma katika taasisi za Umma,kwa tathmini iliyopo inabainisha kuwa utoshelevu wa mahitaji ya watumishi kwa taasisi za Umma upo kati ya asilimia 52 hadi 90 hata hivyo, zipo baadhi ya taasisi ambazo zina watumishi wa ziada katika baadhi ya kada;

Zoezi hili lilianza mwezi Januari 2022 na lilitakiwa likamilike katikati ya mwezi Februari, 2022 hata hivyo, tukiangalia mwenendo wa zoezi hili mpaka leo inaonesha bado Wizara na Taasisi nyingi hazijakamilisha zoezi hili muhimu,"amesema

Amesema,taarifa zilizopo hadi sasa kati ya Wizara na Taasisi 427 zilizo kwenye Mfumo wa HCMIS zote zimeshaanza kutumia Mfumo na zipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji wa zoezi hilo na zipo kati ya asilimia 13 hadi 97. 

Aidha, taasisi 41 kati ya taasisi 70 zilizo nje ya Mfumo wa HCMIS zimeshawasilisha taarifa zao na sasa wataalam wanachakata taarifa hizo kwa ajili ya kuziweka kwenye Mfumo na kwamba bado kuna Wizara na Taasisi nyingi hazijatekeleza maelekezo ya Serikali ipasavyo.

"Bila shaka wote mnakumbuka kuwa mwezi Januari 2022 mara tu baada ya kuteuliwa niliongea nanyi kupitia Waandishi wa Habari juu ya mwelekeo wa Mifumo ya Utendaji kazi na niliahidi kurudi kwenu na Mfumo wa Kielektroniki utakaotusaidia kufanya tathmini ya hali ya watumishi katika taasisi za Umma,

"Ofisi yangu itahakikisha inazingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2030; Ilani ya Uchaguzi wa Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 – 2025; Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa Awamu ya Tatu 2021/22 – 2025/26 pamoja na maono ya Rais wa Serikali ya Awamu ya Sita na Amiri Jeshi Mkuu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuhusu Utumishi wa Umma wa kidijtali na unaofanya kazi kwa uadilifu, kwa bidii, unaotenda haki, unaowajibika kwa hiari na unaozingatia uzalendo wa kitaifa"amesema.

Waziri Jenista amesema taarifa za kwenye Mfumo huo zimebainisha kuwa zipo Taasisi zilizofanya vizuri na ambazo hazijafanya vizuri katika kuingiza taarifa kwenye Mfumo huku akitolea mfano, Taasisi 10 bora zilizofanya vizuri kuwa ni pamoja na Shule ya Sheria Tanzania (97%); Tume ya Ushindani (97%); Chuo cha Ardhi Morogoro (97%) na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala (96%).

Nyingine ni Ofisi ya Rais kumbukumbu na Nyaraka za Taifa (95%); Sekretarieti ya Mkoa wa Iringa (95%); Wakala ya Mafunzo ya Mifugo (95%); Mamlaka ya Serikali Mtandao (95%); Taasisi ya Utafiti wa Wanyama Pori (95%); na Wakala ya Mafunzo ya Menejimenti ya Elimu (94%). 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com