Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SIKU 365 ZA RAIS SAMIA ZAWEKA ALAMA YA MAFANIKIO MAKUBWA KATIKA SEKTA YA MASOKO YA MITAJI



Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameweka alama kubwa ya mafanikio katika maendeleo ya sekta ya masoko ya mitaji katika kipindi cha siku 365 za uongozi wake.


Akielezea mafanikio makubwa yaliyopatikana, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Nicodemus Mkama amesema, mafanikio hayo yametokana na mazingira wezeshi, shirikishi na endelevu ya kisera, kisheria na kiutendaji ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi bora na madhubuti wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Bw, Mkama ameongeza kuwa uchumi wa kidiplomasia na ziara za Rais nje ya nchi zimekuwa chachu yenye matokeo chanya katika kuvutia wawekezaji toka nje ya nchi na kuleta mafanikio zaidi katika masoko ya mitaji.


Bw. Mkama amesema, mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na:

· Thamani ya uwekezaji katika masoko ya mitaji imeongezeka kwa asilimia 12.02 na kufikia shilingi trilioni 32.67 katika kipindi kilichoishia Februari 2022, ikilinganishwa na shilingi trilioni 29.16 katika kipindi kilichoishia Februari 2021.

· Jumla ya mauzo ya hisa na hatifungani yameongezeka kwa asilimia 19.2 na kufikia shilingi trilioni 3.1 katika kipindi kilichoishia Februari 2022, ikilinganishwa na shilingi trilioni 2.6 katika kipindi kilichoishia Februari 2021.

· Mauzo ya hatifungani za Serikali yameongezeka kwa asilimia 38.1 na kufikia shilingi trilioni 2.9 katika kipindi kilichoishia Februari 2022, ikilinganishwa na shilingi trilioni 2.1 katika kipindi kilichoishia Februari 2021.

· Thamani ya Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja katika kipindi kilichoishia Februari 2022 imeongezeka kwa asilimia 55.8 na kufikia shilingi bilioni 868.51 ikilinganishwa na shilingi bilioni 557.28 katika kipindi kilichoishia Februari 2021.


Nicodemus Mkama, Afisa Mtendaji Mkuu, Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA)



Masoko ya mitaji Tanzania ni miongoni mwa masoko matano bora yaliyopata mafanikio makubwa kiutendaji barani Afrika, ndani ya siku 365 za uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan. CMSA, ambayo ni Mamlaka yenye jukumu la kusimamia na kuendeleza masoko ya mitaji hapa nchini imekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza mikakati ambayo imewezesha kufikia mafanikio hayo.

 Mamlaka imetekeleza mikakati ambayo imewezesha kufungua nyanja mpya katika masoko ya mitaji. Mikakati hiyo ni pamoja na: kuanzisha bidhaa na huduma mpya, bunifu, zenye mlengo maalum na matokeo chanya kwa jamii; matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano katika kutoa huduma; kuongeza idadi ya wataalamu wanaokidhi viwango vya kimataifa; na kutoa elemu kwa umma kuhusu fursa zinazopatikana katika masoko ya mitaji.

Katika siku 365 za uongozi wa Mhe. Rais Samia, Mamlaka imetekeleza mikakati ambayo imewezesha kuanzisha bidhaa na huduma mpya bunifu na zenye mlengo maalum wa maadili yaani ethical Sharia Compliant bonds (Sukuk) na zenye mguso na matokeo chanya kwa Jamii yaani social impact bond. Bidhaa hizo ni pamoja na:

· Hatifungani aina ya Sukuk (Sukuk Bond) iliyotolewa na kampuni ya Imaan Finance katika awamu mbili zenye mafanikio, ambapo katika awamu ya kwanza, kiasi cha shilingi bilioni 2.7 kimepatikana, sawa na mafanikio ya asilimia 136 na katika awamu ya pili, kiasi cha shilingi bilioni 2.03 kimepatikana, sawa na mafanikio ya asilimia 135.3. Pesa zilizopatikana zinatumika kuwekeza katika bidhaa ambazo ni Sharia compliant.

· Hatifungani (Jasiri Bond) ya kuwezesha kampuni changa, ndogo na za kati yaani startup, micro, small and médium enterprises, zinazomilikiwa na kuendeshwa na wanawake, vijana na wenye ulemavu, iliyotolewa na Benki ya NMB yenye thamani ya Shilingi bilioni 40. Hatifungani hii ni ya kwanza nchini ambayo ina mguso na matokeo chanya kwa Jamii yaani social impact bond na imekidhi matakwa ya Kanuni za Jumuiya ya Kimataifa ya Masoko ya Mitaji (International Capital Markets Association - ICMA).

· Hatifungani kwa ajili ya kuendeleza Sekta ya Nyumba na Makazi iliyotolewa na Kampuni ya Tanzania Mortgage Refinance ambapo kiasi cha shilingi bilioni 8.9 kimepatikana, sawa na mafanikio ya asilimia 127.

· Hatifungani ya Kampuni ya Afrisian Gining Limited yenye thamani ya shilingi bilioni 58 kwa ajili ya kuendeleza viwanda vya kuchambua pamba na kukamua mafuta ya kupikia.


Wawakilishi wa Watendaji wa Masoko ya Mitaji Nchini wakiwa katika picha ya pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu na Wafanyakazi wa CMSA wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Wiki ya Uwekezaji Duniani mwezi Oktoba 2021

Aidha, Bw Mkama amesema katika kuboresha utendaji wa soko la hisa, Mamlaka imeidhinisha mabadiliko ya Kanuni za Soko la Hisa la Dar es Salaam yaani Stock Exchange Rules, ili kuwezesha utoaji na uorodheshwaji wa bidhaa mpya, ikiwa ni pamoja na bidhaa zinazolenga kugharamia miradi ya maendeleo inayochangia Utunzaji wa Mazingira, Maendeleo ya jamii na Utawala Bora yaani Environmental, Social and Governance (ESG).

Vile vile katika kipindi cha siku 365 za uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia, CMSA imetekeleza mkakati wa kuwezesha utoaji wa Hatifungani za Serikali za Mitaa na Taasisi za Umma yaani Municipal and Subnational Bonds ili kuwezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa (Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya) na Taasisi za Umma, ikiwa ni pamoja na Mamlaka za Maji na Mazingira kugharamia miradi ya kimkakati yenye uwezo wa kujiendesha kibiashara. 

Mamlaka kwa kushirikiana na Mfuko wa Maendeleo ya Mitaji wa Umoja wa Mataifa (UNCDF) imetoa mafunzo kwa wadau mbalimbali kuhusu namna ambazo Mamlaka za Serikali za Mitaa na Taasisi za Umma zinavyoweza kugharamia miradi ya maendeleo inayoweza kujiendesha kibiashara.

Jitihada hizi ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Serikali wa njia mbadala za kugharamia miradi ya maendeleo katika sekta ya umma na binafsi yaani Alternative Project Financing Strategy ambao ulizinduliwa na Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Fedha na Mipango wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ili kuwezesha utekelezaji madhubuti wa Mkakati huo, Timu ya Kitaifa ya Uwezeshaji iliundwa na kuzinduliwa na Bw. Emmanuel Tutuba, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango.

Katika kuwezesha matumizi ya teknolojia katika kutoa huduma za masoko ya mitaji, CMSA imeidhinisha matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano hususan simu za mikononi na intaneti ambapo mfumo wa Sim Invest na Hisa Kiganjani zinatumika katika kuuza na kununua dhamana za masoko ya mitaji. Hatua hii imewezesha kuongeza ushiriki wa wananchi mijini na vijijini katika masoko ya mitaji.

Aidha, CMSA inashirikiana na wadau katika kuandaa miongozo ya kuendesha na kusimamia bidhaa za uwekezaji wa makundi yaani crowdfunding. Bidhaa hizi zitawezesha upatikanaji wa mitaji kwa kampuni changa, ndogo na za kati yaani startup, micro, small and médium enterprises.

Katika jitihada za kuongeza wataalamu wenye weledi na ujuzi kwa ngazi ya kimataifa kwenye masoko ya mitaji, Mamlaka kwa kushirikiana na Taasisi ya Uwekezaji na Dhamana ya nchini Uingereza yaani Chartered Institute for Securities and Investment imetoa mafunzo yanayotambulika kimataifa kwa watendaji wa masoko ya mitaji hapa nchini.

Mafunzo haya yamewezesha kujenga uwezo na ufanisi kwa watendaji wa masoko ya mitaji, ambapo idadi ya washiriki imeongezeka kutoka 494 katika kipindi kilichoishia Februari 2021 na kufikia 667 katika kipindi kilichoishia Februari 2022, ikiwa ni ongezeko la asilimia 22.9. Mafunzo haya yamewapatia wataalamu wa masoko ya mitaji fursa ya kupata leseni za kutoa huduma katika masoko ya Kitaifa, Afrika Mashariki na kimataifa. Aidha, mafunzo haya yamewezesha kuongeza idadi ya watendaji wa masoko ya mitaji wenye leseni ya CMSA kutoka 144 na kufikia 154, ikiwa ni ongezeko la asilimia saba.

Katika kutoa elimu kwa umma kwa lengo la kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu fursa zinazopatikana katika masoko ya mitaji, Mamlaka imetoa mada kuhusu fursa zinazopatikana kwenye masoko ya mitaji kwa njia ya machapisho magazetini na mahojiano kwenye vipindi vya redio na runinga; imetengeneza na kusambaza shajara na vipeperushi vyenye elimu ya masoko ya mitaji na dhamana; imechapisha na kusambaza kwa wadau Ripoti ya Mwaka ya Mamlaka ili kutoa elimu na taarifa ya utendaji kazi wa sekta ya masoko ya mitaji.

Aidha, Mamlaka imeshiriki katika maonyesho ya kitaifa na kimataifa yenye lengo la kutoa elimu kuhusu fursa na faida za kutumia masoko ya mitaji, ikiwa ni pamoja na Wiki ya Wawekezaji Duniani (world Investor Week); Wiki ya Huduma za Fedha; na maonyesho ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba); na Kuendesha mashindano kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu kuhusu masoko ya mitaji na uwekezaji.

Mashindano hayo yameonyesha mafanikio makubwa kutokana na kuendeshwa kwa kutumia njia ya matumizi ya teknologia ya habari yaani simu za mikononi na intaneti. Mashindano haya yamesaidia kuongeza elimu ya masoko ya mitaji kwa vijana wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu, ambapo idadi ya washiriki imeongezeka kutoka wanafunzi 48,662 katika kipindi kilichoishia Februari 2021 na kufikia wanafunzi 70,133 katika kipindi kilichoishia Februari 2022, ikiwa ni ongezeko la asilimia 43.7.

Mashindano haya yamekuwa na matokeo chanya kwa kuongeza idadi ya wawekezaji vijana 10,000 katika masoko ya mitaji; kuanzishwa kwa Jukwaa la Wawekezaji Vijana lenye wanachama zaidi ya 6,000 ambalo linawezesha wawekezaji vijana kupata elimu na uzoefu wa uwekezaji katika masoko ya mitaji. Aidha, mashindano haya yamewezesha kuanzishwa kwa kampuni changa ambayo imefanikiwa kuuza hisa kwa umma na kuorodheshwa katika soko la hisa na kutengeneza ajira zaidi ya 10,000.
Nicodemus Mkama, Afisa Mtendaji Mkuu, CMSA akikabidhi zawadi ya ziara ya mafunzo ya wiki moja Washindi wa juu kumi na mbili wa Shindano la Wanafunzi wa Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu Kuhusu Masoko ya Mitaji na Uwekezaji




Kwa mujibu wa taarifa ya African Market Hub ya mwezi Februari 2022, Soko la Mitaji Tanzania limekuwa miongoni mwa masoko matano bora kiutendaji barani Afrika. Aidha, kwa mujibu wa taarifa ya Benki ya Dunia juu ya tathmini ya Utekelezaji wa Itifaki ya Soko la Pamoja katika Jumuiya ya Afrika Mashariki yaani East African Common Market Protocal Scorecard 2020 on movement of capital, goods and services, Tanzania imepanda viwango vya alama za tathmini kwa asilimia 157 kutoka alama 7 hadi alama 18 kati ya 20 na kuwa nchi ya pili katika utekelezaji wa itifaki ya soko la pamoja katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kwa sasa, Tanzania hakuna vikwazo vya ushiriki wa wawekezaji wa kigeni katika soko ya hisa, hatifungani za kampuni na mifuko ya uwekezaji wa pamoja.

Bw. Mkama alihitimisha kwa kusema kuwa, Sekta ya Masoko ya Mitaji Tanzania ni salama na himilivu na yataendelea kuchagiza na kutoa mchango chanya katika kujenga Uchumi Shindani wa Viwanda kwa Maendeleo ya Watu. Vile vile Bw. Mkama amemtakia Mheshimiwa Rais Samia heri na fanaka katika uongozi wake na kumuombea kwa Mwenyezi Mungu afya njema katika kutekeleza kazi ya kuwaletea maendeleo wananchi.

Alfred Mkombo, Mkurugenzi wa Utafiti, Sera na Mipango wa CMSA wa pili kulia akimkabidhi cheti cha uwekezaji katika hatifungani Bw. Abdulmajid Nsekela, Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CRDB katika hafla ya uzinduzi wa toleo la Hatifungani ya Sukuk iliyotolewa na Kampuni ya Imaan Finance mwezi Agosti 2021

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com