Na LEONARD ONYANGO
SHANGWE na nderemo zilitanda kote nchini Kenya watahiniwa milioni 1.2 walipopokea matokeo yao ya Mtihani wa Darasa la Nane (KCPE) wa 2021.
Kulingana na Waziri wa Elimu, Prof George Magoha, watahiniwa walifanya vyema zaidi ikilinganishwa na wenzao waliofanya mtihani wa KCPE 2020 na 2019 licha ya kujiandaa kwa muda mfupi.
Magata Bruce Mackenzie mwanafunzi wa shule ya Gilgil Hills, Kaunti ya Nakuru aliibuka kidedea baada ya kupata alama 428.
Katika mtihani wa KCPE 2020, mtahiniwa aliyeongoza, Mumo Faith, alipata alama 433.Bruce, 14, jana aliambia Taifa Leo nyumbani kwao katika eneo la Rongai, Kaunti ya Kajiado, kuwa ananuia kuwa mhandisi katika siku za usoni.
Alisema sasa anatarajia kujiunga na Shule ya Upili ya Alliance.Alisema kuwa japo alikuwa akifanya vyema shuleni, hakutarajia kuibuka nambari moja kitaifa.
“Sikuwa nyumbani wakati waziri Magoha alipotangaza matokeo. Niliporejea mama yangu aliniambia kwamba mimi ndiye niliyeongoza kitaifa. Nilifurahi kupita kiasi. Nashukuru Mungu,” akasema Bruce.
Mama yake, Brenda Makori alisema Bruce – ambaye ni mtoto wake wa tatu, aling’aa kwenye mtihani kutokana na nidhamu na bidii yake masomoni.
Kwa mujibu wa matokeo yaliyotolewa na Wazir Magoha, Ashley Kerubo Momanyi wa shule ya Makini, Kibos, Kaunti ya Kisumu, aliibuka katika nafasi ya pili kwa alama 427.
Wengine waliotia fora kitaifa ni Mbugua Sharon Wairimu wa Emmanuel Academy, Mueti Shantel Ndinda wa Kitengela International, Stanley Otieno Omondi wa shule ya Rophine Field Junior, Wekesa Naomi Neema wa White Star Academy na Kimani Ethan Karuga wa Stepping Stones Preparatory ambao wote walipata alama 426. Kulingana na Prof Magoha, idadi ya watahiniwa waliopata alama 250 na zaidi ilikuwa kubwa ikilinganishwa na KCPE ya 2020.
Watahiniwa waliopata kati ya alama 400 na 500 ni 11,857 ikilinganishwa na 8,091 mwaka jana au 9,673 mnamo 2019.Idadi ya watahiniwa waliopata kati ya alama 300 na 399 iliongezeka hadi 315,275 kutoka 282,090 mnamo 2020.
Idadi ya watahiniwa waliopata kati ya alama 200 na 299 ilipungua kutoka 589,027 KCPE ya 2020 hadi 578,197. Lakini idadi ya watahiniwa waliopata kati ya alama 100 na 199 iliongezeka kutoka 299,677 KCPE ya 2020 hadi 307,532.
Hata hivyo, watahiniwa 1,170 kati ya milioni 1.214,031 waliofanya mtihani wa KCPE wa 2021 katika vituo 28,313 kote nchini, walipata chini ya alama 99 ikilinganishwa na 307 mnamo 2020.
Watahiniwa wa mtihani wa KCPE 2021 walifanya mtihani wao Machi, mwaka huu, baada ya kujiunga na Darasa la Nane Julai, mwaka jana.
Serikali ilikataa ombi la wakuu wa shule kuwa mitihani ya KCPE na KCSE (ya kidato cha nne) iahirishwe kutokana na ongezeko la visa vya uteketezaji wa shule. Wakuu wa shule pia walisema kuwa watahiniwa hawakuwa wamejiandaa vyema.
Watahiniwa 11,523 walikosa kujitokeza kufanya mtihani licha ya kujisajili. Idadi hiyo, hata hivyo, ilipungua ikilinganishwa na KCPE 2020 ambapo watahiniwa 12,424 walikosa kujitokeza.Wanafunzi walemavu pia waling’aa katika mtihani huo.
Mtahiniwa aliyeongoza Bethany Tahillah Migosi wa shule ya Thorn Grove akizoa alama 417 . Nao Kamau Jackson Ndegwa wa shule ya Muthiria, Musyoka Kings Kevin wa Kathonzweni A.I.C na Migosi Dominic Sese wa shule ya Mau Narok walifunga orodha ya wanafunzi bora wenye mahitaji maalumu kwa alama 401.
Idadi kubwa ya watahiniwa waliofanya KCPE 2021 walikuwa na ulemvu wa viungo vya mwili na matatizo ya kusikia.
Idadi ya watahiniwa wa umri wa chini ya miaka 12 pia iliongezeka kutoka 26,378 mtihani wa KCPE uliopita hadi watahiniwa 33,627.
Kaunti zilizoongoza kwa kuwa na wanafunzi wa umri wa chini ni Baringo, Bomet, Kericho, Pokot Magharibi na Nyamira.Kaunti za Turkana, Garissa, Kilifi, na Mandera ziliongoza kwa kusajili watahiniwa wa umri wa miaka 19 na zaidi.
Taarifa ya nyongeza na Hillary Kimuyu