Mwalimu wa kitengo cha wanafunzi wenye ulemavu wa akili shule ya msingi Turwa Halmashauri ya mji wa Tarime Mwalimu Mpulan Kashindye akionesha baadhi ya zana za ufundishaji na ujifunzaji shuleni hapo
Zana za ujifunzaji na ufundishaji
***
Na Frankius Cleophace Tarime.
Wazazi na walezi wilayani Tarime Mkoani Mara wameaswa kuwapeleka watoto wao shule hususani wale wote wenye ulemavu na siyo kuwaficha majumbani kutokana na ulemavu walionao.
Hayo yamebainishwa na Mwalimu wa kitengo cha wanafunzi wa ulemavu wa akili katika shule ya msingi Turwa iliyopo Halmashauri ya mji wa Tarime Mkoani Mara Mwalimu Mpulan Kashindye wakati akijibu swali kuhusu uwepo wa mazingira rafiki ya ujifunzaji na ufundishaji kwa wanafunzi wenye ulemavu kuanzia miaka 0-8 katika shule hiyo.
Mwalimu Kashindye alisema kuwa shule ya msingi Turwa yenye wanafunzi wa darasa la kwanza mpaka darasa la saba ina jumla ya wanafunzi wenye ulemavu tofauti 81 ambapo ulemavu wa kusikia wanafunzi 18, ulemavu wa kuona wanafunzi 03 wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia 60 nakueleza katika Halmashauri ya mji wa Tarime zipo shule tatu zenye wanafunzi wa mahitaji maalum ambazo ni Buhemba shule ya msingi, Turwa Shule ya msingi na Mtaahuru shule ya msingi.
Vile vile Mwalimu aliongeza kuwa suala la miundombinu ya wanafunzi yakiwemo majengo ni rafiki sana kwa wanafunzi ambapo ameipongeza serikali kwa kuboresha miundombinu ya majengo katika shule ya msingi Turwa nakusisitiza wazazi sasa kuleta wanafunzi ili waweze kupatiwa elimu.
“Sisi tunapokea watoto kuanzia miaka 03 anakuwa anacheza na wanafunzi anapata chakula na kurejea nyumbani anapofikia miaka sita tunamuunganisha na wanafunzi wengine nakuanza kupatiwa elimu ya ujifunzaji kama wanafunzi wengine hivyo sasa wazazi watumie vyema fursa hii na siyo kuficha watoto maji”, alisema Mwalimu.
Michezo inatumika vipi kufundisha wanafunzi wenye ulemavu.
Katika ufundishaji na Ujifunzaji Mwalimu alisema kuwa suala la michezo katika shule hiyo linatumika sana katika ujifunzaji na ufundishaji ambapo amesema kuwa zipo zana mbalimbali za ufundishaji na ujifunzaji mfano Midori inayoongea ambapo midori hiyo hutumika kuchangamsha wanafunzi wenye ulemavu ambao siyo wachangamfu shuleni hapo.
Vilevile aliongeza kuwa shuleni hapo kuna bembea ya kisasa ambayo mara nyingi wanafunzi utumia kuruka na kucheza jambo ambalo linasaidia kuwajenga kisaikolojia pia watoto hao wanapata chakula pamoja na uji shuleni jambo ambalo linatajwa kuchangia wanafunzi kupenda shule.
Pia Mwalimu aiongeza kuwa bado mwitikio wa wazazi siyo mkubwa kuleta wanafunzi wenye ulemavu shuleni hapo ambapo ameshauri kuwa serikali sasa ione umhimu wa kuwepo na ziara ya matembezi kuanzia ngazi za mitaa kata hadi wilaya kwa ajili ya kubaini watoto wenye ulemavu ambao hawajapelekwa shule ili waweze kupatia haki yao ya msingi ya kupatiwa elimu.
Changamoto zinazokabili shule ya Msingi Turwa yenye wanafunzi wa mahitaji maalum.
Mwalimu alisema kuwa licha ya miundombinu kuwa rafiki kwa wanafunzi hao bado kuna changamoto zinazokabili shule hiyo, mfano ukosefu wa vitabu vya Nukta Nundu kwa ajili ya wanafunzi wasioona, Ukosefu wa mashine ambapo mahitaji ni mashine tano lakini iliyopo ni moja, changamoto ya Ukosefu wa bweni ilikuwasaidia watoto wanatoka maeneo ya mbali waweze kuishi shuleni hapo, Ukosefu wa Matundu ya vyoo kwa walimu ambapo walimu wanalazimika kutumia choo kimoja na wanafunzi,
Vilevile kitengo cha walimu wa wanafunzi wa ulemavu wa akili ni wachache sana ukilinganisha idai ya wanafunzi.
“Kwa wastani mwalimu anapaswa kufundishi wanafunzi kumi lakini walimu ni wachache mwalimu mmoja analazimika kufundisha wanafunzi zaidi ya Ishirini” ,alisema Mwalimu Mpulan.
Hata hivyo changamoto ya ukosefu wa baiskeli kwa ajili ya watoto wenye ulemavu wa viungo imetajwa ambapo alisema kuwa shule inabaiskeli moja inayotumiwa na wanafunzi wote watano jambo ambalo ni changamoto wakati wa ujufunzaji na wakati wa kwenda chooni.
Mwita Wansaku ni mkazi wa mtaa wa Nyamisangura Halmashauri ya mji wa Tarime Mkoani Mara alisema kuwa bado jamii inachangamoto ya kuficha watoto wenye ulemavu nakuomba serikali kuona umhimu wa kutoa elimu kwenye jamii ili kupeleka watoto wenye ulemavu shuleni.
“Ni Kweli watoto wapo wengi majumbani wenye ulemavu lakini wazazi hawawapeleki shule kwa kuona aibu sasa elimu inapaswa kutolewa ili watoto wajengewe misingi bora wakiwa wadogo kwa sababu ni walemavu alafu wananyimwa pia haki yao ya elimu ni ukatili”, alisema Mwita.
Ulimwengu mzima una takribani watoto milioni 250 wenye umri chini ya miaka mitano ambao wanapatikana kwenye nchi zenye uchumi wa chini na zile zenye uchumi wa kati ambao wapo kwenye hatari ya kutokufikia hatua zao za ukuaji.
Takribani robo tatu sawa na asilimia 66 ya watoto wote wenye umri chini ya miaka mitano walio kusini mwa jangwa la Sahara wapo kwenye hatari ya kutokufikia hatua timilifu za ukuaji kutokana na kukosa malezi bora, umaskini, utapiamlo pamoja na matatizo mengine ya kijamii na kiuchumi.
Hadi sasa maendeleo ya mtoto hayajapewa uzito unaostahili, badala yake msisitizo umewekwa kwenye kupunguza vifo licha ya kwamba kipindi cha miaka 0-8 ni fursa muhimu ya kuboresha maendeleo ya binadamu na hivyo kupata mtaji bora wa rasilimali watu yenye tija.
Pia ifahamike kwamba, kukosekana kwa fursa za ukuaji kwa watoto wenye umri huo kunaweza kusababisha changamoto katika maendeleo yao ambayo yanaweza kuathiri kizazi na kizazi.
Kumekuwa na hatua na jitihada mbalimbali katika kutatua changamoto za Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (MMMAM),Mifumo na miongozo mbalimbali imeandaliwa ikiwa imelenga kusaidia utekelezaji wa kina wa shughuli za MMMAM ili kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu.
Miongoni mwa miongozo iliyoandaliwa ni ule wa malezi jumuishi uliozinduliwa na Shirika la Afya Duniani mwaka 2018 ambao una maona kuwa na “Dunia ambayo mtoto anaweza kufikia hatua zake za ukuaji na hakuna mtoto atakaeachwa nyuma” Mfumo huu wa malezi jumuishi unatoa mwongozo sahihi kwa nchi mbalimbali kuwekeza kwenye hatua zote za ukuaji wa mtoto.
Tanzania ni moja ya nchi zenye uchumi wa kati wa chini ambapo asilimia 43 ya watoto wapo kwenye hatari ya kutokufikia hatua timilifu za ukuaji na maendeleo kutokana na viashiria vya hatari mbalimbali vya maendeleo kama vile utapiamlo, umaskini, kukosekana kwa uhakika wa chakula, msongo wa kifamilia, miundombinu duni na uhaba wa rasilimali pamoja na utelekezaji na unyanyasaji wa watoto.
Vilevile wazazi au walezi kutokuwa karibu na watoto wao suala ambalo linachangiwa na kukosekana kwa uelewa wa akina wa MMMAM.
Programu za malezi jumuishi nchini Tanzania zinahitaji kupewa kipaumbele na msisitizo kutokana na kukosekana kwa uratibu mzuri na zinatekelezwa kama sehemu za programu za kisekta au tafiti zinazofanywa na wadau zikilenga baadhi ya umri wa watoto na kutekelezwa kwenye maeneo machache.
Kutokana na umuhimu wa Mfumo wa Malezi Jumuishi, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa MMMAM imeandaa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto itakayo tekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano (2021/22-2025/26).
Mpango huu umelenga kutatua changamoto za ukuaji na maendeleo ya watoto wenye umri wa miaka 0-8. Programu hii itatoa mchango katika kufanikisha Mpango wa tatu wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano 2021/22 - 2025/26 kwa kutambua kwamba watoto ambao wanakosa kufikia kikamilifu hatua za ukuaji ni changamoto kwa maendeleo ya taifa na tishio kwa malengo ya kiuchumi na kijamii ikiwa ni pamoja na kujenga nchi ili kufikia uchumi wa kati.
Kutokana na sababu hizo, programu hii imelenga kuwekeza moja kwa moja kwenye maendeleo ya watu ili kuharakisha upatikanaji wa matokeo chanya ya maendeleo ya awali ya mtoto kwa kuhimiza ushiriki wa sekta mbalimbali katika kutoa huduma za malezi jumuishi yenye vipengele vitano: afya bora kwa mtoto na mama/mlezi; lishe ya kutosha kuanzia ujauzito; malezi yenye mwitikio; fursa za ujifunzaji wa awali; ulinzi na usalama kwa watoto.
Programu Jumuishi ya Taifa ya MMMAM inatakiwa izingatiwe na afua zote za malezi zitekelezwe kwa ujumuishi kwa kuwa inalenga kuleta matokeo chanya katika ukuaji na maendeleo ya awali ya mtoto na kufikia maono: “Watoto wote Tanzania wapo kwenye mwelekeo sahihi wa kufikia ukuaji timilifu”
Kwa muktadha wa Programu Jumuishi ya Taifa ya MMMAM, kundi la watoto walio katika mazingira hatarishi linajumuisha watoto wote walio katika hatari ya kutofikia ukuaji timilifu kutokana na changamoto za mazingira mbalimbali wanamoishi.
Watoto hao ni pamoja na watoto wenye utapiamlo/udumavu; ulemavu wa aina yoyote; wanaochelewa katika hatua za ukuaji; waliozaliwa na maambukizi ya VVU/ au wenye wazazi wenye VVU, yatima; watoto wanaolelewa na wazee, watoto wenzao au walezi ambao ni wagonjwa sana; watoto wanaoishi kwenye maeneo yasiyofikika kwa urahisi na wanaotoka katika familia maskini.
Pia watoto waliofanyiwa ukatili wa aina yoyote, wanaoishi mitaani au kwenye kambi, vituo vya misaada au kwenye mazingira mahususi kama vile watoto wanaoishi na mama zao waliofungwa kwenye magereza, pia wanajumuishwa katika kundi hili, Ili kukabiliana na ukosefu wa usawa na kuhakikisha kuwa hakuna mtoto anayeachwa nyuma, Programu Jumuishi ya Taifa ya MMMAM imelenga kushughulikia mahitaji ya watoto wote wakiwemo kundi hili.
Watoto wote wanapaswa kupata huduma timilifu, hata hivyo tofauti zinategemea na uhitaji binafsi wa mtoto, kwa mfano, mtoto mwenye changamoto ya kujifunza anaweza kuhitaji njia tofauti ya kujifunza ukilinganisha na mtoto asiyekuwa na changamoto hiyo.
Mwandishi wa Habari za Malezi na Makuzi na maendeleo ya awali ya watoto mkoani Mara Frankius Cleophace akifanya mahojiano na Mwalimu wa kitengo cha wanafunzi wenye ulemavu wa akili shule ya msingi Turwa Halmashauri ya mji wa Tarime Mwalimu Mpulan Kashindye.
Mwalimu wa kitengo cha wanafunzi wenye ulemavu wa akili shule ya msingi Turwa Halmashauri ya mji wa Tarime Mwalimu Mpulan Kashindye akionyesha baadhi ya zana za ufundishaji na ujifunzaji shuleni hapo
Mwonekano wa shule ya msingi Turwa iliyopo Halmashauri ya mji wa Tarime kwa ajili ya wanfunzi wenye mahitaji maalum
Social Plugin