Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAJI TARIME YAWACHEFUA DC, KATIBU CCM, MBUNGE WAITARA, WASISITIZA MAJI YA ZIWA VICTORIA


Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini Mwita Waitara akiwa kwenye chanzo cha maji Nyakonga
Meneja RUWASA wilaya ya Tarime Malando Masheku
Mkuu wa wilaya ya Tarime Michael Mtenjele
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)wilaya ya Tarime,Valentine Maganga

Na Dinna Maningo,Tarime
UKOSEFU wa Maji Safi na Salama katika mji wa Tarime mkoani Mara umekuwa ni kero kwa wananchi na kuwa karaha kwa kuwa maji wanayoyatumia ni machafu yanayobadilisha rangi halisi ya nguo nyeupe  na kupoteza muonekano wake licha yakwamba kila mwisho wa mwezi watumiaji wa maji wanalipa bili za maji serikalini.

Mkuu wa wilaya ya Tarime Kanali Michael Mtenjele amesema kuwa upatikanaji wa maji katika halmashauri ya mji Tarime ni asilimia 45, lakini bado si safi na salama ni tope kwakuwa chujio linalochuja maji ni dogo halina uwezo wa kuchuja maji kipindi cha mvua ambapo kiwango cha maji ya tope uongezeka kwenye vyanzo vya maji.

Wakizungumza na Waandishi wa Habari waliofika wilayani humo kutembelea baadhi ya miradi ya maji inayojengwa na Serikali kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA),Mtenjele amesema kuwa katika halamshauri ya wilaya ya Tarime kiwango cha upatikanaji wa maji ni asilimia 70.

"Wakati mwingine ukiingia bafuni unajiuliza nioge au nisioge,maji nikama tope hutamani hata kuvaa shati nyeupe,hali ya maji bado haipo vizuri si safi yanakuja yakiwa vumbi hasa wakati wa mvua chujio ni dogo linazidiwa,tukipata maji kutoka Ziwa Victoria yatatusaidia sana’’,amesema Mtenjele.

Mkuu huyo wa wilaya amesema kuwa kuna mradi  wa maji yatakayotoka Ziwa Victoria na maji kufika Tarime na kwamba Serikali bado inaendelea na mchakato kuhakikisha mradi huo unafika Tarime ambao ndiyo utakuwa suluhisho na kwamba mbali ya chujio la maji kwenye vyanzo vya maji kuzidiwa uwezo wa kusafisha maji bado vyanzo vingine vya maji vimeathiriwa  na shughuli za binadamu.

"Pamoja na changamoto ya maji tunaishukuru serikali kwa kutupatia fedha nyingi kutekeleza miradi ya maji  wilayani hapa miradi mingine imekamilika na mingine inaendelea na ujenzi,kuna mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria zinafanyika taratibu za kitaalamu kisha mkandarasi  ambaye atafanya kazi na mradi uwe mzuri ,hatuwezi kukaa kuusubiri huo mradi tunaendelea na ujenzi wa miradi mingine ya maji",amesema Mtenjele.

Ameiomba RUWASA kuendelea kuongeza miradi ya maji safi na salama  kwa kile alichoeleza asilimia 46 ya ya maji mjini Tarime ni kidogo ikilinganishwa na uhitaji wa huduma ya maji  lakini pia kufanya jitihada kuhakikisha chujio kubwa linanunuliwa na kuweka dawa kwenye maji ili kuwanusuru wananchi wanaotumia maji machafu yasiyo safi na salama kutoka chanzo cha maji cha mto Nyanduruma.

Katibu wa Chama cha Mapinduzi(CCM) wilaya ya Tarime Valentine Maganga amesema kuwa mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria utakaopita wilaya ya Rorya hadi Tarime ni wa muda mrefu  nakwamba kuchelewa kwa mradi huo ni kuchelewa kutimiza hazma ya Chama cha Mapinduzi.

"Lengo la Chama cha Mapinduzi ni kuhakikisha Serikali inatekeleza ilani ya chama ikiwa ni pamoja na kuhakikisha huduma ya maji inapatikana kuhakikisha tunamtua mama ndoo kichwani kwa maana yakufikisha maji kwenye jamii,hii hali ya kuchimba visima vifupi na virefu hatutafikia malengo makubwa,ni vizuri zaidi kulifanya ziwa victoria kuwa chanzo cha maji,mradi ukikamilika silimia 98 ya wana Tarime watakuwa wanatumia maji safi na salama’’,amesema Valentine.

Katibu huyo wa CCM ameeleza kuwa awali miradi ya maji ilipokuwa chini ya halmashauri baadhi haikufanyika vizuri kutoka na halmashauri kuwa na Idara nyingi  na hivyo usimamizi kuwa mdogo katika Idara ya maji na kutopewa kipaumbele hali iliyosababisha Serikali kuanzisha RUWASA na kazi imeonekana.

"RUWASA wamefanya kazi kubwa na miradi inaonekana japo bado safari inayoendelea ni ndefu kuna miradi mizuri kama mradi wa Sirari ila wajaribu kuwasiliana na taasisi zingine kama TANESCO ule mradi unahitaji umeme tusipofunga transifoma hatutafika  maana wanalazimika wasukume maji usiku  ambapo watumiaji wa umeme wanakuwa wamepungua  kwa sababu mchana umeme unatumika sana.

"Kitu kikiwa kizuri siyo kwamba kinakosa changamoto,mfano mradi wa Kibasuka umekamilika kwa asilimia 97 wamefanya kazi kubwa huu mradi awali ulijengwa ukakamilika lakini haukutoa maji wamekuja RUWASA wameuendeleza na maji yanatoka,mradi kata ya Manga haujakamilika ila wamefanya kazi nzuri",amesema. 

Valentine ameitaka RUWASA kutoa elimu kwa kamati za Jumuiya za watumiaji wa maji vijijini kwa kile alichoeleza kuwa kamati hizo zimeundwa  lakini hazina elimu yakutosha ikiwemo ya usimamizi wa miradi ya maji na uendeshaji wake na matumizi ya fedha zinazolipwa na wananchi wanapokuwa wakichota maji ya bomba huku akiisisitiza Serikali kutoa fedha kwa wakati kutekeleza miradi kwa kile alichoeleza kuwa kuna baadhi ya miradi ujenzi umefikia asilimia 50 lakini pesa bado hazijafika kukamilisha miradi.

Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini Mwita Waitara amesema kuwa  maji ya Tarime ni machafu kutokana na baadhi ya vyanzo vya maji likiwemo lambo la maji kijiji cha Nyakonga kata ya Nyakonga kutofanyiwa usafi wala kuweka dawa ya kutibu maji kwenye tenki zinazohifadhi maji na kusababisha wageni wanaofika Tarime kushindwa kuyatumia maji na wenyeji nao wakihangaika kutafuta maji safi na salama.

Waitara ameongeza kuwa hali hiyo inashusha sifa ya wilaya kutokana na tatizo la maji yasiyo safi na salama kupigiwa kelele kwa miaka mingi,aliiomba Serikali kuharakisha mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria ambao umekuwa ndiyo hitaji kubwa la watumiaji wa maji.

Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilaya ya Tarime Malando Masheku amesema kuwa ili kutekeleza lengo la Serikali la kuwapatia huduma ya maji wananchi waishio vijijini kwa asilimia 85 ifikapo 2025,wilaya ya Tarime upatikanaji wa maji vijijini umeongezeka kutoka wastani wa asilimia 47.1 mwaka 2016/2017, hadi wastani wa asilimia 70 kufikia Desemba 2020/2021.

"Mahitaji  ya maji vijijini kwa sasa ni 11900m3/d,lakini uzalishaji uliopo kwa vituo vinavyotoa maji hadi sasa ni 8,330m3/d ikiwa ni asilimia 70, upatikanaji wa huduma ya maji mjini mahitaji ya maji kwa sasa ni 6000m3/d,lakini uzalishaji uliopo kwa vituo vinavyotoa huduma ya maji hadi sasa ni 15000m3d,ikiwa ni asilimia 45 nakwamba miradi ya Sabasaba na Gimenya ikikamilika upatikanaji wa maji utafikia asilimia 56’’,amesema Masheku.

Ameongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2021/2022 serikali imetoa Bilioni 4.33 kutekeleza miradi 9 ya maji zikiwemo Milioni 998,750,000.00 fedha za UVIKO-19 zinazotekeleza miradi miwili ya maji nakwamba miradi yote itakamilika ifikapo Juni,30,2022.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com