Rais Samia Suluhu ameagiza tozo ya TZS 100 iliyokuwa imetolewa kwenye mafuta irejeshwe kwa sababu hesabu zake tayari zilikuwa zimepigiwa kwenye bajeti. Aidha, amesema kwa mwenendo wa upandaji wa bei ya mafuta duniani, kuondoa TZS 100 hakutasaidia, ila kutainyima serikali mapato.
Rais Samia amesema hayo leo Jumatano Machi 30, 2022 wakati akipokea Ripoti ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru) ya mwaka 2020/2021 na Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ikulu ya Chamwino, Dodoma.
“Kipindi hiki cha pili mafuta yamepanda kwa Sh. 156 kwa lita Waziri akaona nikitoa Sh. 100 yapande kwa Sh. 56 nitaleta unafuu ndani ya nchi lakini kwa bahati mbaya hakuangalia kwa upana zaidi kwamba ile ilikuwa tayari iko kwenye bajeti iliyopitishwa na bunge.
“Tumekaa kama serikali tumerekebisha ile Sh. 100 iliyotoka nimeagizwa irudishwe, Tathimini tuliyoifanya hata kama ile shilingi tukiitoa kwa mwenendo wa upandaji wa bei ya mafuta duniani bado isingekuwa na impact ila tungejikosesha kile ambacho tunakusanya.
“Bei ya mafuta kwa Tanzania ni ndogo ukulinganisha na nchi za Afrika Mashariki na Kati, lakini wenye sekta wapo kimya hawasemi, tunamsubiria Rais, Nani ni Rais, Rais ni taasisi.
“Mafuta yamekuwa yakipanda bei toka mwaka jana katikati ya mwaka tukachukua hatua ya kupunguza tozo ndani ya mafuta kwa mara ya kwanza ili kushusha bei ya mafuta kwa wananchi lakini mafuta yameendelea kupanda, Waziri akachukua hatua.
“Wabunge katika maeneo yenu nendeni mkawaeleze wananchi wenu kuhusu mambo yanayoendelea kimataifa, mfano vita ya Ukraine na Urusi imechangia kwa kiasi kikubwa bei ya mafuta kupanda, nendeni mkawaeleze wananchi.
“Ukisoma maoni ya Watanzania wengi kwa sasa ni kupanda kwa bei ya bidhaa, itakumbukwa tulikuwa na kipindi cha janga la Uviko-19 na hivyo uzalishaji wa bidhaa ulipungua na kusababisha bei hizo kupanda, angalia sasa uzalishaji unaendelea kuongezeka.
“Waambieni Wananchi yanayoendelea huko duniani… Afrika Mashariki na kati ni Tanzania pekee ambayo bei ya mafuta bado ipo chini kulinganisha na hizo nchi nyingine,” amesema Rais Samia.
Social Plugin