**********************
Na Mwandishi Wetu
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako, amezindua Bodi ya Usimamizi ya Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) na kuwataka wajumbe wapya wa Bodi hiyo kutumia uzoefu wao kuisaidia Taasisi hiyo kutimiza malengo yake.
Waziri huyo mwenye dhamana ya Masuala ya Kazi na Ajira nchini amesema malengo ya serikali ya awamu ya sita ni kuifikisha Tanzania katika uchumi wa kati wa juu kutoka katika uchumi wa kati wa chini wa sasa ambapo alisema ili kufanikisha azma hiyo ni lazima kuhakikisha kwamba maeneo ya kazi yanakuwa salama na rasilimali watu yenye afya njema.
“Nadhani sote tunaona jinsi Rais wetu anavyofanya jitihada mbali mbali zinazolenga kuvutia uwekezaji mkubwa ndani ya nchi yetu ili kukuza uchumi ambapo kupitia uwekezaji huo ajira nyingi zitazalishwa na ili kuwepo na uzalishaji endelevu tunahitaji watu wenye afya njema pamoja na mazingira salama ya kufanyia kazi na hapo ndipo mchango wenu unapohitajika,” alisema Prof. Ndalichako.
Aidha, aliwaeleza wajumbe hao wa Bodi mpya baadhi ya majukumu yao ya msingi ikiwemo kushauri kuhusu uhuishaji wa Sera, Sheria, Kanuni na Miongozo mbali mbali endapo inakuwa imepitwa na wakati sambamba na kufuatilia mwenendo mzima wa utendaji wa Taasisi husika kwa kipindi chote cha miaka mitatu ambacho Bodi hiyo itahudumu.
Waziri Ndalichako ameitaka Bodi hiyo mpya kuisimamia Taasisi ya OSHA ipasavyo ili iweze kupata mafanikio zaidi ya ambayo yamepatikana katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, Taasisi ya OSHA imepata mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita (2016/2017-2021/2022) ikiwemo kuongeza idadi ya maeneo ya kazi yaliyosajiliwa na OSHA kutoka 4,003 hadi 23, 239 pamoja na idadi ya kaguzi za Usalama na Afya mahali pa kazi kutoka 96,000 hadi 784,000.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo ambaye aliambatana na Waziri Ndalichako katika uzinduzi huo, Prof. Jamal Katundu, amewapongeza wajumbe kwa kuaminiwa na kuteuliwa na kuwaomba kufanya kazi kwa umahiri katika kuisimamia Taasisi ya OSHA.
“Ninapohitimisha salumu zangu kwenu naomba niwaachie changamoto moja ambayo ni kufikiria kuacha alama katika Taasisi ya OSHA pindi muda wenu utakapokwisha,” amesema Prof. Katundu.
Mtendaji Mkuu wa OSHA ambaye kwa mujibu wa muundo wa Bodi hiyo ndiye Katibu wa chombo hicho, amesema Bodi hizo zimekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya Taasisi anayoiongoza na hivyo kupitia Bodi hiyo iliyozinduliwa, Taasisi yake itaendelea kukua na kupata mafanikio zaidi.
Akitoa shukrani kwa niaba ya wajumbe wenzake, Mwenyekiti wa Bodi ambaye ameteuliwa kwa kipindi cha pili kuiongoza Bodi hiyo, Dkt. Adelhelm Meru, amesem yeye pamoja na wajumbe wenzake wana ari kubwa ya kufanya kazi hivyo watajituma katika kutekeleza majukumu yao pamoja na kuzingatia weledi.
Aidha, baada ya tukio hilo la uzinduzi wajumbe wametembelea moja ya mashamba ya mbegu za mboga mboga na matunda ambayo ni miongoni mwa maeneo ya kazi yanayosimamiwa na OSHA ambapo mwakilishi wa Kampuni hiyo ya Enza Zaden Africa Ltd iliyotembelewa, Bw. Gerald Matowo, ameeleza kufurushwa kwao na ziara hiyo ya viongozi wa Wizara, Bodi pamoja na watendaji wa OSHA.