DKT. MABULA ATAKA SEKTA YA ARDHI KUPEWA KIPAUMBELE


Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza wakati wa hafla ya utoaji hatimiliki za kimila kwa wananchi wa wilaya ya Ikungi mkoani Singida tarehe 15 Machi 2022Sehemu ya washiriki wa hafla ya utoaji hatimiliki za kimila iliyofanyika katika halmashauri ya wilaya ya Ikungi mkoani Singida tarehe 15 Machi 2022.Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Ushirikiano la Japan (KOICA) Kyuchoel Eo akizungumza wakati wa hafla ya utoaji hatimiliki za kimila kwa wananchi wa wilaya ya Ikungi mkoani Singida tarehe 15 Machi 2022.Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Benelith Mahenge akizungumza wakati wa hafla ya utoaji hatimiliki za kimila kwa wananchi wa wilaya ya Ikungi mkoani Singida tarehe 15 Machi 2022.Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Ushirikiano la Japan (KOICA) Kyuchoel Eo akitoa hati kwa baadhi ya wananchi wa Ikungi wakati wa hafla ya utoaji hatimiliki za kimila uliofanywa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula mkoani Singida tarehe 15 Machi 2022.

*****************

Na Munir Shemweta, WANMM SINGIDA

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Ageline Mabula amewataka wananchi kuipa kipaumbele sekta ya ardhi kwa kuwa sekta hiyo ikitumiwa vizuri itawezesha kuchochea mapinduzi kichumi.

Aidha, aliwataka wananchi na taasisi zote zinazomiliki ardhi nchini kuhakikisha zinatimiza wajibu wa kulipa kodi ya pango la ardhi kila mwaka kwa maendeleo endelevu.

Dkt Mabula alisema hayo tarehe 15 Machi 2022 wakati wa hafla ya utoaji hatimiliki za kimila kwa wananchi wa wilaya ya Ikungi mkoani Singida. Zaidi ya hati 5,050 zimeandaliwa kupitia mradi wa matumizi ya ardhi uliotekelezwa kwa pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Wanawake (UN Women) na Shirika la Kimataifa la Ushirikiano la Japan (KOICA).

‘’Mimi na Wizara yangu tunaamini kuwa ardhi ikitumiwa vyema kwa maana ya kupangwa, kupimwa na kumilikishwa itawezesha kuchochea mapinduzi makubwa na ya haraka ya kiuchumi kwa mwananchi mmoja mmoja kwenye mikoa yetu na taifa kwa ujumla’’ alisema Dkt Mabula.

Waziri wa Ardhi aliwaambia wananchi wa Ikungi waliopokea hati katika hafla hiyo kuwa, wamenufaika kwa kupata nyaraka za kumiliki ardhi alizoziekeza kuwa zina faida kubwa katika maisha yao ya kila siku.

Alitaja baadhi ya manufaa hayo kuwa, ni kuwa na usalama wa miliki za ardhi, uhakika wa milki, kupunguza migogoro na kutumia hatimiliki kama dhamana katika taasisi mbalimbali kama vile taasisi za fedha, vyombo vya kisheria sambamba na kupandisha thamani ya ardhi.

‘’ Nitoe rai kwa wananchi wote kuwa na tabia ya kutumia na kuchangamkia fursa kama hizi zinapotokea katika maeneo yetu ili kuweza kupata manufaa kama haya’’ alisema Dkt Mabula.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Ikungi mkoani Singida Justice Kijazi alisema, mradi wa uandaaji na utekelezaji mpango wa matumizi bora ya ardhi uliofadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Japan (KOICA) katika halmashauri yake ulifanikisha kuandaliwa kwa hati za kimila 5,050 na ulilenga kunufaisha wananchi wa Ikungi hasa wanawake na wasichana.

‘’ Halmashauri yetu ya Ikungi ina jumla ya vijiji 101 na kati ya hivyo vijiji 68 tayari vimepimwa huku vijiji 28 vikiwa vimefanyiwa mpango wa matumizi ya ardhi na tayari hati 5,050 zimeshakamilika kwa ajili ya kupatiwa wananchi’’ alisema Kijazi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Misaada la Japan (KOICA) nchini Tanzania Kyuchoel Eo alisema Shirika lake litaendelea na juhudi za kusaidia wanawake na wasichana katika wilaya ya Ikungi ikiwa ni mikakati yake ya kuunga mkono usawa wa jinsia katika masuala ya ardhi.

Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt Benelith Mahenge alieleza umuhimu wa upangaji na upimaji ardhi katika mkoa wake kwa kueleza kuwa ardhi ni jambo la msingi kwa kuwa kila kiumbe duniani kinaitegemea.

‘’Viumbe vyote vinategemea ardhi na sote ni mashahidi migogoro inayoongoza ni ya matumizi ya ardhi na kwa bahati mbaya ardhi haiongezeki hivyo tukipata miradi kama hii tutatatua au kupungiuza migogoro ya ardhi’’ alisema Mahenge.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post