Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Mtwara Rehema Mwinuka (Kulia) akimkabidhi hati mkazi wa kijiji cha Nanyhanga halmashauri ya wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara Ally Salum Mkulumwile alipompelekea hati nyumbani kwake kufuatia kushindwa kujitokeza kuchukua kutokana na changamoto za ugonjwa mwishoni mwa wiki.
Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Mtwara Rehema Mwinuka (Kulia) akiwa na hati mkazi wa kijiji cha Nanyhanga halmashauri ya wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara Ally Salum Mkulumwile (katikati) pamoja na mke wake mara baada ya kumkabidhi hati yake ya ardhi alipompelekea nyumbani kwake kufuatia kushindwa kujitokeza kuchukua kutokana na changamoto ya ya ugonjwa mwishoni mwa wiki.
************************
Na Munir Shemweta, WANMM
Katika jitihada za Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuongeza kasi ya umilikishaji ardhi nchini, Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Mtwara Rehema Mwinuka amempelekea Hati ya Ardhi mkazi mmoja wa kijiji cha Nanyhanga kilichopo katika halmashauri ya wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara ambaye amepooza miguu.
Hatua hiyo ilimfanya mke wa mmiliki huyo Ally Salum Mkulumwile kutoa shukran za dhati kwa Wizara ya Ardhi kupitia Kamishna wake mkoani Mtwara na kueleza kuwa, uamuzi huo siyo tu unampa faraja mume wake ambaye ni mgonjwa bali unaongeza imani kwa wananchi juu ya utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
" Nikushukuru sana Kamishna kwa uamuzi huu mlioamua kutuletea hati hapa nyumbani maana kama unavyomuona mume wangu hawezi hata kutembea na kuongea kwake pia ni shida, asante sana" alisema mke wa Mkulumwile.
Kwa Mujibu wa Rehema aliyempekea hati mteja wake huyo mwishoni mwa wiki, hatua ya ofisi yake kumpelekea hati nyumbani ni moja ya juhudi za ofisi yake kuhakikisha wamiliki wa ardhi wasiokuwa na uwezo wa kuzifuata hati za ardhi kwenye ofisi za ardhi za mkoa kutokana na changamoto za kiafya basi wanafikiwa na kupatiwa hati.
"Hapa ni Tandahimba katika kijiiji cha Nanyhanga nimemletea hati mteja wangu mzee wangu Mkulumwile ambaye amepooza miguu na hakuweza kuja kuchukua hati yake tulipofanya zoezi la kugawa hati katika halmashauri ya Tandahimba" alisema Kamishna Rehema.
Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Mtwara aliongeza kuwa, ofisi yake iligawa jumla ya hati 26 kati ya 50 katika halmashauri hiyo ya Tandahimba na kubainisha kuwa, uelewa mdogo wa wamiliki kuhusu taratibu za kuchukua hati ulichangia wengine kushindwa kuzichukua kutokana na kutuma wawakilishi wasiozingatia taratibu za kumchukulia mmiliki hati.
"Watu wanajitokeza kuchukua hati lakini tatizo uelewa. Kuna wamiliki waliwatuma wawakilishi tukashindwa kuwapa kutokana na kushindwa kutimiza masharti ya kumchukulia mtu hati" alisema Rehema.
Alisema, ofisi yake imekuwa ikifanya zoezi la ugawaji hati mara kwa mara katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Mtwara na kwa sasa jumla ya hati 453 hazikachukuliwa na wamiliki wake mbali na juhudi mbalimbali zinazofanyika kuhakikisha wamiliki hao wanachukua hati.
Hata hivyo, alibainisha kuwa, changamoto kubwa kwa zile hati zisizo chukuliwa ni kuwa, wamiliki wake sio wakazi Mtwara na oifisi yake haina namba zao za simu huku ikidaiwa wengi wao walichukua viwanja wakati wa kipindi cha mradi wa Gesi.
Social Plugin