Na Mwandishi wetu -Mwanza
Ikiwa leo ni kilele cha siku ya mwanamke Duniani, klabu ya waandishi wa habari ya Mkoa wa Mwanza(MPC) imezindua tuzo ya heshima ya Mwanahabari Shujaa sambamba na kuwatangaza Husna Milanzi na Johari Shani kupata tuzo hiyo kwa mwaka 2022.
Kwa muijibu wa Mwenyekiti wa MPC bwana Edwin Soko alisema kuwa, tuzo hiyo kuanzia mwakani 2023 itatolewa kila ifikapo Januari 11, ikiwa ni siku ya kumbukumbu ya vifo vya waandishi wa habari watano waliofariki Wilaya ya Busega,Mkoa wa Simiyu kwa ajali ya gari walipokuwa wakienda kutimiza majukumu yao ya kikazi wilayani Ukerewe.
Zoezi hilo limefanyika kwenye hafla fupi iliyoandaliwa na MPC kwa ajili ya kuwapongeza waandishi wa Habari wanawake wa Mkoa wa Mwanza.
Mgeni rasmi ambaye ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Desk & Chair Foundation Alhaj Sibatin Meghjee aliwapongeza waandishi wa habari wanawake wa Mkoa wa Mwanza kwa kufanya kazi zao kwa weledi na kuwaomba wazidi kuzingatia maadili ya uandishi wa habari.
Pia Meghjee alifanya zoezi la kukabidhi vyeti vya tuzo ya heshima ya Mwanahabari Shujaa kwa familia ya marehemu Husna Milanzi na Johari Shani, ambao wote walipoteza maisha kwenye ajali ya Januari 11, 2022.
Naye Mwakilishi wa waandishi wa habari wanawake Clara Matimo alitoa shukrani kwa mgeni rasmi na kuibua ombi maalumu kwa mgeni rasmi kwenye kuwashika mkono waandishi wanawake kwenye kusudio lao la kuwa na mradi wa bajiji kwa ajili ya kuongeza kipato kwa waandishi wa habari.
MPC imekuwa na utaratibu wa kuadhimisha siku ya Mwanamke Duniani kwa kuandaa tukio maalumu kwa ajili ya kuwapongeza waandishi wa habari wanawake Mkoa wa Mwanza.