Mfano wa Nyundo inayotumika Mahakamani
**
Mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Kigoma imemhukumu kunyongwa hadi kufa mtu mmoja aitwaye Kinyota Kabwe mkazi wa Muzye wilayani Kasulu kwa kosa la kumuua kwa makusudi jirani yake kwa kumchoma mkuki mara tatu na kusingizia alikuwa amechanganyikiwa.
Kesi hiyo namba 105 ya Jamhuri dhidi ya Kinyota Kabwe imesikilizwa na Jaji mfawidhi wa Mahakama hiyo Lameck Mlacha, inaelezwa mnamo Septemba 15, 2013 majira ya saa tisa alasiri mshtakiwa akiwa na mkuki alienda nyumbani kwa Lucia Tekena na kumchoma mkuki shingoni,kifuani na tumboni huku binti wa marehemu nae akijeruhiwa na mshtakiwa.
Inaelezwa kabla ya tukio hilo ambalo baada ya muda mfupi mwanamke huyo alipoteza maisha na yeye kukamatwa nikama kulikuwa na ugomvi na mvutano kati yake na mkewe nyumbani kwake ambao unahisiwa kuna uwezekano ulikuwa una muhusisha marehemu pia hivyo kusababisha mauaji hayo.
Upande wa Jamhuri uliongozwa na wakili Antia Julius na upande wa utetezi ukiongozwa na wakili Edna Aloyce. Upande wa utetezi uliwasilisha ushahidi wa mshtakiwa na kaka yake ulio eleza mshtakiwa ana matatizo ya akili na alikuwa anatumia dawa kwa muda hivyo kuna wakati hali ilikuwa inakuwa mbaya huku muhusika akisema hakumbuki tukio la kuchoma mkuki.
Jamhuri iliwasilisha mashahidi watano akiwemo aliye shuhudia mauaji hayo na Daktari wa magonjwa ya akili aliye mpima na majibu yakawa kuwa hana ugonjwa wowote wa akili.
Jaji Mlacha amesema inaonyesha mshtakiwa alikusudia kuua ndio maana alielekeza mkuki tumboni ,kifuani na shingoni na suala la ugonjwa wa akili hiyo ni namna ya kutafuta kujitetea na haina mashiko, hivyo akamhukumu adhabu kunyongwa hadi kufa.
Chanzo - EATV