Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Dkt.Selemani Jafo akiongea na Waandishi wa habari Katika Ofisi za wizara MtumbaJijini Dodoma
Na Dotto Kwilasa-Malunde 1 Blog-DODOMA
KATIKA kipindi cha mwaka mmoja tangu Serikali ya awamu ya sita ilipoingia madarakani imefanya mambo mengi ikiwemo vikao vya kujadili masuala ya Muungano katika ngazi mbalimbali,kutekeleza miradi ya pande mbili za Muungano,kuimarisha ushirikiano na hifadhi na usimamizi wa mazingira.
Hayo yameelezwa leo Jijini hapa na Waziri wa nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Dkt. Selemani Jafo katika kikao chake na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita Katika kipindi cha mwaka mmoja.
Dk. Jafo amesema katika kipindi cha mwaka mmoja serikali ya awamu ya sita imefanya vikao vya kujadili masuala ya Muungano ili kujadili kwa kina hoja 18 ambapo kati ya hizo hoja 11 zilipatiwa ufumbuzi na kuondolewa katika orodha ya hoja za muungano.
"Hoja zilizopatiwa ufumbuzi na kuondolewa kabisa ni pamoja na uingizaji wa maziwa kutoka zanzibar, usimamizi wa utoaji na ukusanyaji wa kodi katika huduma za simu unaofanywa na mamlaka ya mapato zanzibar, mkataba wa mkopo wa fedha za ujenzi wa Barbara ya chakechake hadi wete Mkoa wa Pemba,"amesema.
Amezitaja hoja zingine kuwa ni mkataba wa mkopo wa fedha za mradi wa ukarabati wa hospitali ya mnazi mmoja, mkataba wa mkopo wa fedha za ujenzi wa bandari ya Mpigaduri, uvuvi kwenye ukanda wa bahari kuu, ajira kwa watumishi wa zanzibar katika taasisi za muungano.
Waziri huyo amesema changamoto nyingine ni mgawanyo wa mapato yatokanayo na misaada kutoka nje ya nchi, mapato yanayokusanywa na uhamiaji kwa upande wa zanzibar, uteuzi wa Makamu mwenyekiti wa Tanzania Revenue Appeal Tribinual (TRAT) kutoka zanzibar na uteuzi wa mjumbe wa bodi ya bima ya Amana kutoka zanzibar.
"Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia omeendelea kuhakikisha kuwa muungano wetu unalindwa, unadumishwa, na kuimarishwa na kuhakikisha kuwa hoja 18 za muungano zinapatiwa ufumbuzi,"amesema
Katika hatua nyingine amesema Serikali ya Tanzania na Zanzibar zimeendea kushirikiana katika miradi mbali mbali ikiwemo mpango wa kunusuru kayak maskini awamu ya tatu mzunguko wa pili ambapo sh. bilion 112.9 zimepangwa kutumika Zanzibar.
Amesema miradi mingine ni pamoja na mradi wa kuzalisha zao la mpunga,mradi wa kudhibiti Uvuvi na maendeleo ahirikishi kusini magharibi ya bahari ya Hindi, Mpango wa kurasimisha rasilimali na biashara Tanzania(MKURABITA), Mkakati wa kudhibiti sumu kuvu Tanzania (TANIPAC), na mradi wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi Kwa kutumia mifumo ikolojia vijijini(EBARR).
"Zanzibar ilipata sh. Bilion 230 zilizotokana na mkopo nafuu wa IMF kwà ajili ya kukabiliana na athali za Uviko 19 smbapo fedha hizo zimeelekezwa katika huduma za jamii ikiwemo elimu, afya, miundombinu na ujenzi wa masoko,"amesema na kuongeza;
Katika kipindi cha miezi 12 ya serikali ya awamu ya sita vimefanyika vikao 21 vya sekta ya maji, nishati, madini, uchukuzi, utumishi na utawala Bora, uratibu wa shughuli za serikali, Viwanda na Biashara, maliasili na utalii, kilimo, habari na utamaduni, ardhi, fedha na mipango, na tawala za mikoa na serikali za mitaa lengo kuhimarisha ushirikiano,"alisema
MAZINGIRA
Kwa upande wa mazingira Waziri Jafo amesema chini ya uongozi makini wa Rais Samia katika kutunga na kuboresha sera, sheria, kanuni na miongozo ya mazingira kwa kukamilisha mapitio ya sera ya taifa ya mazingira ya mwaka 1997 ambapo baraza la mawaziri limepitisha sera mpya ya taifa ya mazingira ya mwaka 2021 na mkakati wake.
Amefafanua kuwa sera hiyo iliyozinduliwa hivi karibuni na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt.Philip Mpango imejumuisha masuala ya mazingira yaliyokuwemo Katika sera ya 1997 na masuala mapya ambayo ni udhibiti wa taka za kielektroniki,usimamizi na matumizi ya kemikali na mabadiliko ya tabianchi.
"Sera ya taifa ya mazingira ya mwaka 2021 imeongeza wigo na masuala na changamoto za mazingira zinazopaswa kufanyiwa kazi katika kipindi husika ili kuleta maendeleo endelevu lakini pia imezingatia changamoto mpya za mazingira zinazoendelea kujitokeza kutokana na mabadiliko ya mifumoya kiuchumi,kijamii na mazingira,"amesema Jafo.