Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NDEJEMBI ADHAMIRIA KUSIMAMIA SHILINGI BILIONI 7.8 ZILIZOTOLEWA NA RAIS KUTEKELEZA MIRADI YA KUPUNGUZA UMASKINI MKOANI MWANZA


 Naibu Waziri,Ofisi ya Utumishi wa Umma na utawala bora Deogratius Ndejembi wakati  akizungumza na Waratibu,wahasibu na maafisa ufuatiliaji wa mpango wa Tasaf leo Jijini Mwanza

*****



Na Mwandishi wetu,Malunde 1 blog-MWANZA


NAIBU Waziri,Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Deogratius Ndejembi ameahidi kusimamia kikamilifu matumizi ya shilingi bilioni 7.8 zilizotolewa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ili kutekeleza Miradi 104 ya Kupunguza Umaskini Awamu ya Nne (TPRP IV), iliyoibuliwa mkoani Mwanza kwa lengo kuboresha maisha ya kaya maskini katika halmashauri zote mkoani humo.


Mhe. Ndejembi ameeleza dhamira yake hiyo leo wakati akizungumza na Waratibu, Wahasibu na Maafisa Ufuatiliaji wa Mpango wa TASAF mkoani Mwanza, katika kikao kazi chake na maafisa hao chenye lengo la kuhimiza usimamizi mzuri wa fedha zilizotolewa na Serikali ili kutekeleza Miradi ya Kupunguza Umaskini Awamu ya Nne mkoani humo.


Mhe. Ndejembi amesema, shilingi bilioni 7.8 ni fedha nyingi ambazo Mhe. Rais amezitafuta kwa wadau wa maendeleo ili zitumike kuboresha maisha ya kaya maskini na kuongeza kuwa, wananchi wana matarajio makubwa ya fedha hizo ziwasaidie kunyanyua maisha yao, hivyo atahakikisha anafuatilia kwa ukaribu ili zitumike kwa lengo lililokusudiwa.


Ameongeza kuwa, atahakikisha anafanya ufuatiliaji wa karibu wa utendaji kazi wa Waratibu, Wahasibu na Maafisa Ufuatiliaji wa Mpango ili fedha hizo zitumike vizuri, na kuwaasa kuwa atakayejaribu kucheza nazo zitamtokea puani hivyo ni heri acheze na mshahara wake na si fedha hizo.


“Mmemsikia Mhe. Rais mara kadhaa akisema mtu akimzingua naye anamzingua, hivyo kabla Mhe. Rais hajanizingua mimi nitawazingua kweli kweli na ndio maana nimeamua kuwaelezeni ukweli ili kila mmoja wetu atekeleze wajibu wake,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.


Katika kutekeleza azma yake ya kufanya ufuatiliaji, Mhe. Ndejembi ameahidi kufanya ziara mara kwa mara kanda ya ziwa ili kujiridhisha na namna Miradi Miradi 104 ya Kupunguza Umaskini Awamu ya Nne inavyotekelezwa.


Aidha, amewataka waratibu wa TASAF katika Halmashauri zote za Mkoa wa Mwanza kuhakikisha wanawashirikisha Wakuu wa Wilaya na Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya ili kuwe na uwazi na ufuatiliaji mzuri wa utekelezaji wa miradi hiyo yenye manufaa kwa wananchi wanaotoka katika kaya maskini.


Naibu Waziri Ndejembi amesema kuwa, yapo maeneo ambayo yamefanya utekelezaji mzuri wa miradi ya TASAF, hivyo nikaona ni vema nije mkoani Mwanza kwa lengo la kuhimiza usimamizi mzuri wa miradi hiyo ya Kupunguza Umaskini Awamu ya Nne ili mnapoanza utekelezaji kusitokee ubabaishaji.


“Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa imejionea mkoani Njombe kituo cha afya chenye ubora na thamani kimejengwa na TASAF kwa gharama ya milioni 80 tu, hivyo natamani miradi yote ya TASAF iendelee kujengwa kwa gharama stahiki,” Mhe. Ndejembi amefafanua.


Kwa niaba ya Waratibu, Wahasibu na Maafisa Ufuatiliaji wa Mpango wa TASAF mkoani Mwanza waliohudhuria kikao kazi hicho cha Mhe. Ndejembi na Maafisa hao, Mratibu wa TASAF Sengerema Bw. Malissa Ndugha amemshukuru Mhe. Ndejembi kwa kuwakumbusha jukumu la kusimamia vizuri fedha za miradi ya TASAF ili thamani ya fedha hizo zilizotolewa na Serikali ionekane.


Bw. Ndugha amemhakikishia Mhe. Ndejembi kuwa, wamepokea maelekezo yake na watayatekeleza kikamilifu ili kutomuangusha Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amezitafuta fedha hizo kwa lengo la kuboresha maisha ya kaya maskini. 


Miradi ya Kupunguza Umaskini Awamu ya Nne (TPRP IV) ilizinduliwa tarehe 27 Oktoba,2021 jijini Mwanza. Jumla ya Miradi 104 yenye zthamani ya shilingi 7,845,316,205.24 imeibuliwa na kupitishwa kwa ajili ya utekelezaji Mkoani Mwanza katika Halmashauri zote za Kwimba, Magu, Misungwi, Ilemela, Nyamagana, Sengerema, Ukerewe na Buchosa. Kati ya miradi hiyo 104, 31 ni ya afya, 49 ya elimu na 24 ni ya kutoa ajira za muda (PWP).

 

Naibu Waziri,Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na Waratibu, Wahasibu na Maafisa Ufuatiliaji wa Mpango wa TASAF mkoani Mwanza (hawapo pichani) wakati wa kikao kazi chake na maafisa hao chenye lengo la kuhimiza usimamizi mzuri wa fedha za kutekeleza Miradi ya Kupunguza Umaskini Awamu ya Nne mkoani humo. 

 

Waratibu, Wahasibu na Maafisa Ufuatiliaji wa Mpango wa TASAF mkoani Mwanza wakimsikliliza Naibu Waziri,Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) wakati wa kikao kazi Naibu Waziri huyo na maafisa hao chenye lengo la kuhimiza usimamizi mzuri wa fedha za kutekeleza Miradi ya Kupunguza Umaskini Awamu ya Nne mkoani humo.


Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Salum Kalli akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri,Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi kuzungumza na Waratibu, Wahasibu na Maafisa Ufuatiliaji wa Mpango wa TASAF mkoani Mwanza wakati wa kikao kazi cha Naibu Waziri huyo na maafisa hao chenye lengo la kuhimiza usimamizi mzuri wa fedha za kutekeleza Miradi ya Kupunguza Umaskini Awamu ya Nne mkoani humo.

 

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bi. Sarah Mshiu akizungumza na Waratibu, Wahasibu na Maafisa Ufuatiliaji wa Mpango wa TASAF mkoani Mwanza (hawapo pichani) wakati wa kikao kazi Mhe. Deogratius Ndejembi na maafisa hao chenye lengo la kuhimiza usimamizi mzuri wa fedha za kutekeleza Miradi ya Kupunguza Umaskini Awamu ya Nne mkoani humo.

 

Mratibu wa TASAF Mkoa wa Mwanza Bi. Monica Mahundi akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ya mkoa wa Mwanza kwa Naibu Waziri,Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi wakati wa kikao kazi cha Naibu Waziri huyo na Waratibu, Wahasibu na Maafisa Ufuatiliaji wa Mpango wa TASAF mkoani Mwanza chenye lengo la kuhimiza usimamizi mzuri wa fedha za kutekeleza Miradi ya Kupunguza Umaskini Awamu ya Nne mkoani humo.

 

Mratibu wa TASAF Wilaya ya Ilemela Bw. Frank Ngitahoh akimueleza Naibu Waziri,Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) namna Wilaya yake ilivyotekeleza Mpango wa TASAF wakati wa kikao kazi cha Naibu Waziri huyo na Waratibu, Wahasibu na Maafisa Ufuatiliaji wa Mpango wa TASAF mkoani Mwanza, chenye lengo la kuhimiza usimamizi mzuri wa fedha za kutekeleza Miradi ya Kupunguza Umaskini Awamu ya Nne mkoani humo.

 

Sehemu ya Waratibu, Wahasibu na Maafisa Ufuatiliaji wa Mpango wa TASAF mkoani Mwanza wakimsikiliza Naibu Waziri,Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi akikisisitiza jambo wakati wa kikao kazi chake na maafisa hao chenye lengo la kuhimiza usimamizi mzuri wa fedha za kutekeleza Miradi ya Kupunguza Umaskini Awamu ya Nne mkoani humo.


Mratibu wa TASAF Wilaya ya Sengerema Bw. Malissa Ndugha akitoa neno la shukrani kwa Mhe. Ndejembi kwa niaba ya Waratibu, Wahasibu na Maafisa Ufuatiliaji wa Mpango wa TASAF mkoani Mwanza waliohudhuria kikao kazi cha Naibu Waziri huyo na maafisa hao chenye lengo la kuhimiza usimamizi mzuri wa fedha za kutekeleza Miradi ya Kupunguza Umaskini Awamu ya Nne mkoani humo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com