Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipokea Tuzo ya Heshima kutoka Bi. Nuru Awadh kwa niaba ya Wanawake wenye Ulemavu Tanzania kabla ya kuzungumza na Makundi hayo Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma leo tarehe 16 Machi, 2022. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akinyanyua juu Tuzo ya Pongezi mara baada ya kukabidhiwa kutoka kwa Watu wenye Ulemavu Tanzania katika hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma leo tarehe 16 Machi, 2022.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Makundi mbalimbali ya watu wenye Ulemavu, Sauti ya Wanawake wenye Ulemavu (SWAUTA), Shirikisho la Jumuiya ya Watu wenye Ulemavu Zanzibar (SHIJUWAZA) na Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu SHIVYAWATA, katika viwanja vya Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma leo tarehe 16 Machi, 2022.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipokea Tuzo ya Pongezi kutoka kwa Watu wenye Ulemavu Tanzania kutoka kwa Stella Jailos wa SWAUTA kabla ya kuzungumza na Makundi hayo Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma leo tarehe 16 Machi, 2022.
Makundi mbalimbali ya burudani ya Watu wenye Ulemavu wakitoa burudani katika viwanja vya Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma leo tarehe 16 Machi, 2022.
Makundi mbalimbali ya watu wenye Ulemavu, Sauti ya Wanawake wenye Ulemavu (SWAUTA), Shirikisho la Jumuiya ya Watu wenye Ulemavu Zanzibar (SHIJUWAZA) na Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu SHIVYAWATA, wakimsikiliza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan wakati akiwahutubia katika viwanja vya Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma leo tarehe 16 Machi, 2022.
*********************
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameziagiza Wizara za Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na Wizara ya Afya kuhakikisha kuwepo mifumo madhubuti ya kutambua mapema aina mbalimbali za ulemavu ili kuweza kutoa huduma ipasavyo.
Rais Samia ametoa agizo hilo leo wakati akizungumza na watu wenye ulemavu katika hafla iliyofanyika viwanja vya Ikulu Chamwino, mkoani Dodoma.
Mhe. Rais Samia amesema unyanyapaa wa watu wenye ulemavu katika jamii umepungua kutokana na jitihada za baadhi ya watu wenye ulemavu kupaza sauti, hivyo kuwataka watu wenye ulemavu kujikubali walivyo katika jamii.
Kwa upande wa elimu, Serikali imeendelea kuhakikisha upatikanaji wa elimu kwa watu wenye ulemavu kuanzia ngazi ya awali hadi Chuo Kikuu.
Kwa mwaka 2022, jumla ya watoto wenye ulemavu 2,883 wameandikishwa katika Elimu ya awali, wakiwemo wavulana 1,470 na wasichana 1413 huku wanafunzi 1,157 wakiandikishwa kidato cha kwanza.
Vilevile, Rais Samia amesema Serikali inafanya jitihada kuimarisha hospitali na kuajiri madaktari bingwa kwa ajili ya matibabu ya watoto wenye vichwa vikubwa na kuwataka wananchi kuwafichua watoto hao mapema ili waweze kupatiwa tiba ya upasuaji.
Halikadhalika, Rais Samia ametoa rai kwa watu wenye ulemavu kujitokeza kuhesabiwa wakati wa Sensa ya Watu na Makazi mwezi Agosti mwaka huu wa 2022 bila kuwaficha watoto wenye ulemavu ili kupata takwimu sahihi zitakazowezesha Serikali kupanga mipango ya maendeleo shirikishi kwa watu wenye ulemavu.
Social Plugin