Mrajisi Mkuu wa Vyama vya Ushirika Dkt. Benson Ndiege Jijini Dodoma akizungumza wakati akifungua kikao kazi cha watendaji ,Ofisi ya Mrajisi pamoja na wadau kilicholenga usimamizi na uendeshaji wa shughuli za SACCOS zilizopewa Leseni.
Na Doreen Aloyce, Dodoma
WATENDAJI wanaosimamia na kuendesha Shughuli za Vyama vya Ushirika SACCOS vilivyopewa Leseni hapa nchini Daraja A na B wametakiwa kuwasilisha taarifa zao za kila mwezi kwa kutumia Mfumo ulioandaliwa na Ofisi ili kuepuka changamoto wakati wa kufanya tathimini , utunzaji mbaya wa taarifa na Takwimu za Vyama.
Wito huo umetolewa na Mrajisi Mkuu wa Vyama vya Ushirika Dkt. Benson Ndiege Jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha watendaji ,Ofisi ya Mrajisi pamoja na wadau kilicholenga usimamizi na uendeshaji wa shughuli za SACCOS zilizopewa Leseni.
Aidha Dkt. Ndiege amesema Taasisi nyingi zinazotoa huduma za fedha nchini zikiwemo SACCOS zimekuwa zikikumbana na changamoto nyingi ikiwemo utunzaji mbaya wa taarifa na Takwimu za Vyama ,kutorejeshewa kwa mikopo inayokopwa na wanachama kwa wakati pamoja na kutotekelezwa vyema matakwa ya sheria.
"Niwasihi leo mmepata semina hii lakini kumbuka kushindwa kutekelezwa kwa matakwa ya sheria kunaweza kuathiri na kusababisha changamoto katika utoaji wa huduma kwa wanachama wenu ikiwa ni pamoja na kuchukuliwa kwa hatua ya kutozwa fedha kutoka kwenye mshahara wako na sio fedha za Chama husika ,hatutaki tena Ofisi ishindwe kupata Takwimu na taarifa ambazo zinasaidia kufanya tathmini", amesema Dkt. Benson.
Amesema kutumia mifumo ya Tehama kwa ajili ya kurahisisha utendaji kazi na kuongeza ufanisi vyamani na kwamba inapaswa kutumika badala ya kufanya kazi kimazoea.
Pia amesema SACCOS zinapaswa kuhakikisha zinafanyia kazi mapungufu ya hoja za ukaguzi wa nje kwa lengo la kuondoa hati chafu na zile zitakazoendelea kupata hati chafu watendaji wakuu watachukuliwa hatua ikiwemo kuondolewa kwenye nafasi zao kwa mujibu wa kanuni 85(1)(g) ya mwaka 2019.
Mkurugenzi wa Utawala Kampuni ya Digital Solutions Jonas Makubo amesema wamekuwa wakisaidia Taasisi za Kiserikali na binafsi kuweka mifumo maofsini ambapo mpaka sasa wamefikia Mikoa 14 jambo ambalo limewarahisishia wao kupata huduma kwa urahisi.
Amesema kuwa Kampuni hiyo imeleta mapinduzi makubwa kwenye Vyama vya Ushirika hamsini ambavyo vimefungiwa mifumo na imeleta tija kwa namna wanavyotunza kumbukumbu na kutoa huduma kwa uwazi .
Naye Mkurugenzi wa Tanzania Mentors Action ambao wanafanya kazi ya kufunga mifumo Dkt. Paul Nandrie amesema kuwa inawasaidia wanachama kukopa kupitia simu yake ya mkononi.
"Mfumo huu una faida kubwa ikiwemo kupata mikopo kwa njia ya simu kupitia mitandao yote na kurudisha mwenyewe na pia mifumo hii inaweza kufunga mahesabu ya Vyama vya Ushirika na kuwawezesha wao kuwa na viambatanisho ambavyo vitasaidia kupata hati safi", amesema Dkt. Nandrie.
Kwa upande wao washiriki wa Vyama hivyo vya SACCOS wamesema kuwepo kwa mifumo hiyo itasaidia kutunza nyaraka mbalimbali zikiwemo utunzaji wa fedha.
Mrajisi Mkuu wa Vyama vya Ushirika Dkt. Benson Ndiege Jijini Dodoma akifungua kikao kazi cha watendaji ,Ofisi ya Mrajisi pamoja na wadau kilicholenga usimamizi na uendeshaji wa shughuli za SACCOS zilizopewa Leseni.
Mkurugenzi wa Tanzania Mentors Action Dkt. Paul Nandrie akizungumza kwenye kikao kazi cha watendaji ,Ofisi ya Mrajisi pamoja na wadau kilicholenga usimamizi na uendeshaji wa shughuli za SACCOS zilizopewa Leseni.
Jonas Makubo Mkurugenzi wa Utawala Kampuni ya Digital Solutions akizungumza kwenye kikao kazi cha watendaji ,Ofisi ya Mrajisi pamoja na wadau kilicholenga usimamizi na uendeshaji wa shughuli za SACCOS zilizopewa Leseni.
Social Plugin