Serikali ya Comoro imesema bado hakuna mwili wowote uliopatikana baada ya kuanguka kwa ndege inayofanya safari zake visiwani humo.
Ajali hiyo imetokea wakati ndege hiyo ya Tanzania inayomilikiwa na kampuni ya Fly Zanzibar ilipokuwa inatoka makao makuu ya visiwa vya Comoro, Moroni kwenda kisiwa cha Mwali juma lililopita.
Kwa mujibu wa mkurugenzi wa mawasiliano wa viwanja vya ndege Comoro Mohamed Said, Ndege hiyo ilikuwa imebeba abiria 12 raia wa Comoro na marubani wawili raia wa Tanzania na inaaminika ilianguka baada ya kukumbana na hali mbaya ya hewa wakati ikikaribia kutua.
Serikali ya Comoro kwa kushirikiana na kampuni ya wapiga mbizi ya ufaransa bado inaendelea kusaka miili ya watu hao 14, lakini mpaka sasa ni mabegi ya abiria na baadhi ya mabaki ya ndege ndivyo vitu pekee vilivyo patikana.
Mmiliki wa Ndege hiyo Rubani Mohamed Mazrui amesema kuwa ndege nyingine ya kampuni hiyo inaendelea na shughuli za kusaka watu hao na ishara yoyote inayoashiria kuwepo kwa kitu chochote kinachohusiana na ajali hiyo.
Ameongeza kuwa shughuli za uokoaji zinaendelea lakini mpaka sasa hakuna mwili wowote uliopatikana wala kisanduku cha kunakili data za safari ya ndege ‘blackbox’.