Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akifungua kikao kazi jijini Dodoma leo cha uanzishwaji wa mradi wa ujumuishwaji wa anuai za jamii katika Mradi wa Tanzania ya Kidijitali unaotekelezwa na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Sehemu ya washiriki wa kikao kazi cha uanzishwaji wa mradi wa ujumuishwaji wa anuai za jamii katika Mradi wa Tanzania ya Kidijitali wakimsikiliza Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro wakati akifungua kikao kazi hicho leo jijini Dodoma.
*******************
Na. Mary Mwakapenda-Dodoma
Tarehe 03 Machi, 2022
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro amesema Serikali imeyashirikisha makundi ya anuai za jamii katika utekelezaji wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali ili makundi hayo yaendane na maendeleo ya TEHAMA na yanufaike kikamilifu na huduma zinazotolewa na Serikali kupitia TEHAMA.
Dkt. Ndumbaro amesema hayo leo jijini Dodoma wakati akifungua kikao kazi cha uanzishwaji wa mradi wa ujumuishwaji wa anuai za jamii katika Mradi wa Tanzania ya Kidijitali unaotekelezwa na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Dkt. Ndumbaro amesema, uzoefu unaonyesha makundi ya anuai za jamii yasipowekewa mkakati maalum wa kushirikishwa katika uchumi wa kidijitali, mara nyingi yamekuwa yakisahaulika, hivyo Serikali kwa kutambua umuhimu wake imeamua kuyashirikisha rasmi kwenye utekelezaji wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali ili uwe na tija kwa wananchi kama ilivyokusudiwa.
Dkt. Ndumbaro ameongeza kuwa makundi ya anuai za jamii katika utumishi wa umma hayana mwamko wa kutumia TEHAMA kiutendaji, ila yanalazimika kuitumia kutokana na majukumu waliyo nayo, hivyo changamoto ni kubwa zaidi kwa makundi ya anuai za jamii yaliyo nje ya utumishi wa umma.
Dkt. Ndumbaro amesema kutokana na hali hiyo, Serikali imeona ni wakati muafaka kwa makundi hayo ya anuai za jamii kushirikishwa kikamilifu ili jamii iweze kwenda pamoja kwenye ulimwengu wa kidijitali.
Akizungumzia mchango wa makundi ya anuai za jamii katika kikao kazi hicho, Dkt. Ndumbaro amesisitiza kuwa maoni yao yataisaidia Serikali kutekeleza vema Mradi huo wa Tanzania ya Kidijitali hasa katika eneo la kuboresha utoaji wa huduma bora kwa umma.
Aidha, ameyashukuru makundi ya anuai za jamii yaliyoitikia wito wa kuhudhuria kikao kazi hicho ili kuiwezesha Serikali kupata maazimio yenye tija kwa mustakabali wa maendeleo ya taifa.
Kikao kazi hicho kililenga kujenga uelewa na kubadilishana uzoefu juu ya ujumuishwaji wa masuala ya anuai za ijamii katika Mradi wa Tanzania ya Kidijitali unaotekelezwa na Serikali kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2021-2026.
Social Plugin