Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YATOA BILIONI 7.9 KUENDELEZA UJENZI WA MELI MPYA YA KISASA MV. MWANZA HAPA KAZI TU



Meli ya MV.MWANZA HAPA KAZI TU ikiwa kwenye karakana ya ujenzi wa Meli katika eneo la Mwanza South inayoendelea kujengwa chini ya Mkandarasi Gas Entec kutoka Korea Kusini
Meli  kubwa ya MV. UMOJA itakayotumika kusafirisha mizigo baada ya ukarabati kukamilika

Baadhi ya mafundi wanaofanya ukarabati wa Meli ya MV. UMOJA wakifungua vifaa mbalimbali kwenye injini
Injini ambazo zinatolewa  kwenye Meli ya MV. UMOJA kwaajili ya kuweka mpya ikiwa ni sehemu ya ukarabati wa Meli hiyo
MV.CLARIAS ni Meli ambayo imekarabatiwa na Kampuni ya huduma za Meli kupitia mapato yake ya ndani ambayo itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 216 na tani 10 za mizigo
Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni za huduma za Meli akizungumza na waandishi wa habari leo hii katika karakana ya ujenzi wa Meli kubwa ya Mv.Mwanza hapa kazi tu katika eneo la Mwanza South

Na Hellen Mtereko, Mwanza

Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu imetoa jumla ya shilingi Bilion 7.9 kwa lengo la kuendeleza ujenzi wa Meli mpya ya kisasa ya Mv. Mwanza hapa kazi tu.


Hayo yamebainishwa leo  Alhamisi Machi 3,2022 na Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya  huduma za Meli (MSCL), Philemoni Bangambilana wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye karakana ya ujenzi wa Meli hiyo, eneo la Mwanza South.

Amesema katika kipindi cha mwaka mmoja wa  utawala wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu amefanya Mambo makubwa ikiwa ni pamoja na kuendeleza ujenzi wa Meli kubwa ya Mv. Mwanza hapa kazi, ambayo ikikamilika itakuwa na uwezo wa kubeba abilia 1200, tani za  mizigo 400, Magari madogo 20 pamoja na magari makubwa 3.


Bangambilana ameleeza kuwa mradi huo kwa sasa umefikia asilimia 64 na ifikapo mwezi Mei itashushwa majini na ujenzi utaendelea kujengwa kwenye maji, ujenzi huo utagharimu shilingi bilioni 96 hadi utakapokamilika na unatarajia kukamilika mwezi wa 9 mwaka huu.

"Kukamilika kwa Meli hii ya Mv.Mwanza  inayotekelezwa na kampuni ya Gas Entec Company Limited kutoka Korea Kusini, itarahisisha huduma za usafiri kwa Wananchi na itachochea maendeleo sanjari na  kuongeza pato la Taifa", amesema Bangambilana.

Katika hatua nyingine Bangambilana ameleeza kuwa  Serikali imetoa bilioni 2.9  kwaajili ya ukarabati wa Meli kubwa ya Mv. Umoja ambayo itatumika kusafirisha mizigo.

Amesema utekelezaji wa  mradi huo ulianza Novemba 25,2021 na kwa sasa ukarabati umefikia asilimia 20, na ukarabati utagharimu bilioni 19.4 huku shughuli zinazoendelea kufanyika ni kutoa mitambo ya zamani na kuweka vifaa vipya .

Hatahivyo Bangambilana  amesema kuwa Kampuni ya huduma za Meli (MSCL) kupitia mapato ya ndani wamefanikiwa kukarabati Meli ndogo ya  Mv.Clarias ambayo inaweza kubeba abilia 216, tani 10 za mizigo.

" Tunatarajia mwishoni mwa wiki hii kuanza safari ya kutoa huduma katika visiwa vya Gana,Goziba kwa kutumia Mv. Clarias ambapo shughuli mbalimbali zinaendelea kufanyika, ninaamini kwamba tukiwa na chombo cha Serikali ambacho kitapeleka huduma za uhakika, itakuwa ni faraja kubwa kwa Wananchi kwasababu chombo cha Serikali gharama zake ziko chini hivyo kinamnufaisha mwananchi anapokuwa anatekeleza shughuli zake", amesema Bangambilana.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com