Mkuu wa wilaya ya Tarime Mhe. Kanali Michael M. Mntenjele akitoa hotuba ya ufunguzi wa mafunzo/mkutano wa kuutambulisha Mwongozo wa Mafunzo ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kwa vijana wa Skauti katika ukumbi wa chuo cha ualimu Tarime Machi 15, 2022. Kulia kwake ni Rais wa Skauti wilaya ya Tarime Bw. Simbanilo Shabani Changiki na kushoto kwake ni Katibu Tawala wa wilaya hiyo Bw. John Marwa na Kamishina wa Skauti wa Wilaya Bw. Charles Chacha Marwa.
Walezi wa Skauti ngazi ya kata wa wilaya ya Tarime (waliosimama) wakiwa na Mhe. Mkuu wa Wilaya ya Tarime Mhe. Kanali Michael Mntenjele (aliyeketi katikati) baada ya kukabidhiwa Mwongozo wa Mafunzo kwa Vijana wa Skauti Machi 15, 2022 katika ukumbi wa chuo cha ualimu Tarime. Wengine walioketi kutoka kushoto ni Kamishna wa Skauti wa wilaya hiyo Bw. Charles Chacha Marwa, wapili ni Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Bw. John Marwa, wa nne ni Rais wa Skauti wa Wilaya ya Tarime Bw. Simbanilo Shabani Changiki na wa tano Ni Mkuu wa TAKUKURU wa Wilaya hiyo Bw. Protas B. Sambagi.
Mkuu wa wilaya ya Tarime Mhe. Kanali Michael M. Mntenjele aliyeketi katikati pamoja na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Usalama (W) baada ya kukabidhiwa Mwongozo wa Mafunzo ya Kuzuia na kupambana na Rushwa Machi 15, 2022 katika ukumbi wa chuo cha ualimu Tarime.
Kamishina wa Skauti wilaya ya Tarime Bw. Charles Chacha Marwa akiwasilisha mada katika mafunzo ya kuutambulisha Mwongozo wa Mafunzo ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kwa vijana wa Skauti kiwilaya Machi 15, 2022 katika ukumbi wa chuo cha ualimu Tarime.
Mkuu wa TAKUKURU (W) Tarime Bw. Protas B. Sambagi akiwasilisha mada katika Mafunzo ya kuutambulisha Mwongozo wa Mafunzo ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kwa vijana wa skauti yaliyofanyika kiwilaya Machi 15, 2022 katika ukumbi wa chuo cha ualimu Tarime.
Na Dinna Maningo,Tarime.
IMEELEZWA kuwa Vijana wa Skauti ni kundi muhimu katika Taifa nakwamba endapo wakipewa elimu ya kuzuia na kupambana na rushwa wataitumia vyema na kuwa msaada shuleni na kwenye jamii katika kupinga vitendo vya rushwa.
Hayo yalielezwa na mkuu wa wilaya ya Tarime Kanali Michael Mtenjele katika mkutano wa kutambulisha mwongozo wa kuwafundisha vijana wa skauti kuhusu kuzuia na kupambana na rushwa wilayani humo uliofanyika katika ukumbi wa chuo cha ualimu Tarime.
Mtenjele alisema kuwa mapambano dhidi ya rushwa ni jukumu la kila mmoja na si jukumu la TAKUKURU au Serikali pekee,ila kila mwananchi kwa nafasi yake anao wajibu wa kuzuia na kupambana na rushwa.
"TAKUKURU inalo jukumu la kuwaelimisha na kuwashirikisha wananchi wa rika na makundi mbalimbali katika mapambano ya rushwa ikiwa ni pamoja na vijana walio shuleni ili wajifunze kuchukia na kuikataa rushwa tangu wakiwa wadogo.
"Wahenga walisema Samaki Mkunje angali Mbichi na Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo,ndiyo maana zimeanzishwa klabu za wapinga rushwa katika shule za msingi,sekondari na vyuo ili kuwa na vijana na hatimaye taifa la watu waadilifu,wawajibikaji na wazalendo wanaochukia rushwa na maovu yote katika jamii”alisema Mtenjele.
Mtenjele alisema kuwa mkakati wa taifa dhidi ya rushwa wa mwaka 2018/2018-2021/2022 unasisitiza ushirikishwaji wa wadau katika mapambano ya dhidi ya rushwa nakwamba chama cha skauti ni chama cha hiari chenye lengo kubwa la kuwalea ili wawe wenye kuipenda na kuijali nchi yao (wazalendo) huku wakiwa ujasiri wakakamavu na wenye kuthubutu kutenda mambo yaliyo mema kwa faida yake,kwa jamii na taifa kwa ujumla.
"Skauti wakiwa ni miongoni mwa wadau ni fursa nzuri ya kuwalea vijana katika maadili na kuwahamasisha kuzuia na kupambana rushwa,ninapongeza ushirikiano wa TAKUKURU na chama cha Skauti Tanzania (TAKUSTA) kwakuwa utaongeza kasi ya mapambano dhidi ya rushwa nchini.
Aliongeza"Ninafahamu kwamba pamoja na mafunzo ya kuzuia na kupambana na rushwa vijana wa skauti watapata elimu kutoka jeshi la uokoaji na elimu hiyo wataitumia vyema na kuwa msaada shuleni na katika jamii"alisema Mtenjele.
Mtenjele aliwaagiza Maafisa Elimu kutoa maelekezo kwa wakuu wa shule kuhusu umuhimu wa maudhui ya mwongozo na namna unavyooweza kutumika kwenye Taasisi za elimu ili kukuza maarifa shuleni na nje ya shule na vijana wa skauti wajengwe kimaadili ili kuondokana na tatizo la ukosefu wa maadili unaolikabili taifa.
Aliwaagiza viongozi wa Skauti kuwawezesha vijana wa skauti wakawe mfano wa kuishi katika viapo vya skauti na kuendeleza kauli mbiu inayosema"Uskauti ni kuliunganisha Taifa" uskauti ufike shuleni hadi vyuoni na TAKUKURU iendelee kuelimisha na kuhamasisha makundi yote ya jamii ili kushiriki ipasavyo katika mapambano dhidhi ya rushwa TAKUSKA! Tokomeza Rushwa!.
Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa(TAKUKURU) wilaya ya Tarime, Protas Sambagi alisema kuwa moja ya jukumu la taasisi hiyo ni kuelimisha jamii na makundi mbalimbali ili kupambana na vitendo vya rushwa nakwamba skauti wakipata mafunzo watasaidia kuelimisha wanafunzi wenzao.
"lengo la kikao ni kutambulisha mwongozo wa kuwafundisha vijana wa skauti kuhusu kuzuia na kupambana na rushwa,tumeanza na viongozi wa skauti na wataalamu wa elimu na matarajio yetu ni kuifikisha elimu hii mashuleni na ndani ya jamii ili kuongeza uelewa kwa wananchi ili kuweza,kutoa taarifa dhidi ya vitendo vya rushwa,tunaamini elimu hii itawasaidia Skauti katika kuzuia na kupambana na rushwa"alisema Sambagi.
Kamishna wa Skauti wilaya ya Tarime Charles Marwa alisema kuwa mafunzo hayo yatawezesha walimu na walezi wa skauti kuelewa namna ya kudhibiti na kupambana na rushwa na vijana kuwa waadilifu,waaminifu na kuzitii mamlaka za nchi kwani makusudio ya kuwepo wa Skauti ni kuwalea katika maadili ya kizalendo,waipende nchi yao na kuitumikia"alisema Marwa.
Katibu wa Skauti katika wilaya hiyo,Julius Ally alisema kuwa wamepokea mwongozo huo nakwamba watashirikiana na TAKUKURU kuzuia na kupambana na vitendo vya rushwa kwakuwa wamepata elimu nao watasaidia kuifikisha kwa vijana wa skauti ambao nao wataifikisha kwa wanafunzi na jamii.
Aliongeza kuwa wilaya hiyo ina vijana wa skauti wasiopungua 500 anawakaribisha vijana wengine kujiunga na Skauti kwani kuwepo Skauti shuleni kunadumisha amani.
Social Plugin