Watumishi wanne katika Halmashauri ya wilaya ya Tarime wakiwa katika Mahakama ya wilaya ya Tarime.
Na Dinna Maningo,Tarime
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilaya ya Tarime mkoani Mara,imewafikisha Mahakamani watumishi wanne wa Halmashuari ya wilaya ya Tarime wakituhumiwa kwa kosa la Rushwa na Uhujumu Uchumi,makosa ambayo yanatokana na fedha za ujenzi wa Bwalo na Jiko katika shule ya Sekondari Manga.
Watumishi wao ni Mhandisi Ujenzi Ernest Maungo,John Nago ambaye ni fundi sanifu,Mwl. Sara Jonas aliyekuwa mkuu wa shule ya Sekondari Manga na Mwl.Mukama Mazigo ambaye ni afisa Elimu Vifaa na Takwimu wakidaiwa kufanya matumizi ya nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri, ufujaji na ubadhilifu.
Watumishi hao wamepandishwa kizimbani Machi 23,2022, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya wilaya ya Tarime Yohana Myombo,Mwendesha mashtaka wa TAKUKURU na Wakili wa Serikali Mwinyi Yahaya amesoma mashtaka manne, ambapo shtaka la kwanza hadi la tatu la matumizi ya nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri yanawahusu washtakiwa wote na shtaka la nne la Ufujaji na Ubadhilifu linamhusu mshitakiwa wa kwanza Mhandisi Ernest Maungo.
Wakili Yahaya amesema kuwa washatkiwa wamefunguliwa shauri la Uhujumu Uchumi namba 10 la mwaka 2022 ambapo shtaka la kwanza ni matumizi ya nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri kinyume na kifungu cha 22 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 mapitio ya 2019 ikisomwa pamoja na aya ya 21 ya Jedwali la kwanza pamoja na kifungu cha 57 (1) na 60 (2) vya sharia ya Uhujumu Uchumi Sura ya 200 mapitio ya 2019.
Yahaya ameieleza mahakama kwamba Disemba 8,2020 washtakiwa wote wakiwa watumishi wa umma katika halmashauri hiyo ,kwa lengo la kumdanganya mwajiri mbaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Tarime,walitumia nyaraka ambayo ni dokezo sabili la tarehe 8,12,2020 kuhusu ripoti ya ukaguzi wa malipo ya ujenzi wa jengo moja la bwalo na jiko katika shule ya sekondari Manga EP4R au TAMISEMI 2020/202,ikiwa na maelezo ya uongo kuonyesha kwamba Tsh.Milioni 3,135,000 yalikuwa ni malipo ya ujenzi wa bwalo na jiko katika shule hiyo wakati wakijua kuwa si kweli na kwa ufahamu wao walilenga kudanganya mwajiri.
Wakili huyo ameeleza kuwa shtaka la pili ni matumizi ya nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri kinyume na kifungu hicho cha sheria ya Kuzuia na Kupambana na rushwa Sura ya 329,kwamba Januari 11,2021 washtakiwa wote walitumia nyaraka ambayo ni dokezo sabili la tarehe januari,11,2021 kuhusu ripoti ya ukaguzi wa malipo ya ujenzi wa jengo moja la bwalo na jiko katika shule hiyo EP4R au TAMISEMI 2020/2021 ikiwa na maelezo ya uongo kuonesha kwamba Tsh.Milioni 3,230,000 yalikuwa ni malipo ya ujenzi huo wakati wakijua si kweli na kwa ufahamu wao walilenga kumdangaya mwajiri.
Yahaya amesema kuwa shtaka la tatu ni matumizi ya nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri kinyume cha sharia hiyo ya kuzia na kupambana na rushwa ambapo aprili 14,2021 washtakiwa wote wakiwa watumishi walitumia nyaraka ambayo ni dokezo sabili la tarehe 14,4,2021 kuhusu ripoti ya ukaguzi wa malipo ya ujenzi wa jingo moja la bwalo na jiko katika shule hiyo EP4R au TAMISEMI 2020/2021 dokezo hilo likiwa na maelezo ya uongo ya kuonesha kwamba Tsh.Milioni 3,135,000 yalikuwa ni malipo ya ujenzi huo.
Ameongeza kuwa Mhandisi Ernest Maungo ambaye ni mshtakiwa wa kwanza anakabiliwa na shtaka la Ufujaji na Ubadhilifu kinyume cha kifungu cha 28 (2) cha sharia ya Kuzuia na Kupambana na rushwa Sura ya 329 na kifungu cha 57(1) na 60(2) vya sharia ya Uhujumu Uchumi ,kwamba Disemba 8,2020 Mhandisi Ernest kwa kukosa uaminifu alibadilisha matumizi ya Tsh.Milioni 9,500,000 kwa ajili ya matumizi binafsi fedha zilizotolewa na serikali kwa ajili ya ujenzi wa bwalo la chakula na jiko katika shule hiyo.
Washtakiwa wote wamekana mashtaka yote yanayowakabili na wameshindwa kutimiza masharti ya dhamana hivyo wamepelekwa rumande na kesi yake itatajwa Aprili 6,2022 kwa ajili ya kusikilizwa.
Wakati huohuo,Wakili Yahaya amesema kwamba Juni,2020 Halmashauri ya wilaya ya Tarime ilipokea Tsh. Milioni 100,000,000 kutoka serikalini kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Bwalo na Jiko katika shule hiyo ya Manga ambapo kazi ya ujenzi ilianza Octoba,13,2020 na ilitakiwa kukamilika Mach,2021.
Amesema kuwa hadi Agost,2021 ujenzi ulikuwa haujakamilika na kulikuwa na upungufu uliofanyika wakati wa ujenzi unaoashiria kuhatarisha usalama wa jengo na maisha ya wanafunzi,walimu na wananchi wengine wanaoishi maeneo hayo,kutokana na upungufu huo TAKUKURU imefanya uchunguzi ambao umeleteleza shauri hilo.
Social Plugin