**************************
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya Magharibi limefanya operesheni maalumu ya ukaguzi wa bidhaa za chakula na vipodozi kwenye maghala, maduka makubwa ya jumla na rejareja, mipakani na bandarini kwa halmashauri 11 katika mikoa ya Katavi,Rukwa na Kigoma.
Akizungumza wakati wa operesheni hiyo Kaimu Meneja wa Kanda ya Magharibi (TBS) Bw. Rodney Alananga amesema lengo la operesheni lilikuwa kuondoa bidhaa hafifu zinazopatikana katika masoko ya mikoa ya kanda ya magharibi ili kuwalinda walaji/watumiaji wa bidhaa hizo.
"Katika operesheni hii shirika limebaini makosa yanayofanywa na wafanyabiashara ikiwemo kuuza bidhaa za chakula na vipodozi ambazo zimekwisha muda wa matumizi, bidhaa za chakula na vipodozi zisizosajiliwa na TBS, na uuzwaji wa vipodozi vilivyopigwa marufuku kutumika". Amesema Bw. Alananga
Amesema changamoto kubwa waliyojifunza ni kwamba wafanyabiashara wengi hupitisha bidhaa kwa njia za panya, hununua na kutokagua bidhaa katika maduka yao kuhakiki muda wa mwisho wa matumizi, kutotunza Kumbukumbu za manunuzi na mauzo ya wapi wamenunua na wapi wameuza, na kununua bidhaa za vyakula na vipodozi katika maduka yasiyokuwa na vibali au yasiyo sajiliwa na TBS
Aidha amesema TBS imefanikiwa kukamata bidhaa za chakula na vipodozi zenye uzito wa tani 32.2 na thamani ya TZS 97, 706, 200/= pia inatarajia kufanya uteketezaji wa bidhaa hizo baada ya taratibu zote za kisheria kufuatwa.
"TBS imechukua hatua za awali kwa kuzuia bidhaa zote zilizoonekana kuwa makosa ambazo utekelezaji na ufuatiliaji wake utaendelea ndani ya Siku 14 kwa mujibu wa notisi ya kuzuia bidhaa (seizure notice) Amesema Bw. Alananga.
TBS kwa kushirikiana na vyombo vingine vya serikali kama vile Jeshi la Polisi, Mamlaka ya Mapato, Uongozi wa Mikoa, Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri itaendelea kufanya Operesheni za kushitukiza katika maeneo ya masoko mijini, vijijini, mipakani, bandarini na kuwabaini wakiukaji na kuchukua hatua za kisheria ili kulinda afya ya watanzania, biashara na mazingira.
Pamoja na hayo TBS inatoa wito kwa wafanyabiashara kuzingatia sheria zilizowekwa ili kuweza kujiepusha na hasara zinazoweza kujitokeza kutokana na uuzaji wa bidhaa hafifu.