Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAANDISHI WA HABARI MARA KUTEMBELEA MIRADI 41 YA MAJI VIJIJINI




Na Dinna Maningo,Mara

JUMLA ya Miradi mipya 41 ya Maji yenye thamani ya fedha Bilioni 16.7 zilizotolewa na serikali ili kupunguza adha ya maji inayowakabili wananchi wa vijiji mbalimbali katika mkoa wa Mara, itatembelewa na waandishi wa habari ili kuona hatua ya utekelezaji wake pamoja na kuibua changamoto zinazowakumba wananchi katika upatikanaji wa maji safi na salama.

Baadhi ya Waandishi wa Habari katika mkoa wa Mara wa vyombo vya habari vya Magazeti, Televisheni na mitandao ya kijamii  kutoka gazeti la Habari leo,Uhuru ,Nipashe,Majira,ITV,Azam Tv,Mara Online na Uhuru Digital,watatembelea miradi hiyo ya maji kwa siku sita katika wilaya sita za mkoa huo.

Lengo la kutembelea miradi hiyo iliyopo katika wilaya sita za mkoa huo ambazo ni Musoma,Tarime,Rorya,Serengeti,Butiama na Bunda ,ni kuupasha umma juu ya miradi iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini ( RUWASA) ili kuwezesha upatikanaji wa wa huduma ya maji safi na salama.

Pia Waandishi wa Habari wataibua changamoto zilizopo za upatikanaji wa maji unaowakumba wananchi waishio vijijini,kutoa elimu ya umuhimu wa kutunza na kulinda miundombinu ya maji na kuziripoti katika vyombo vya habari ili ziwafikie wananchi na serikali.

Mratibu wa waandishi wa habari watakaoitembelea miradi ya maji,Ghati Msamba ambaye ni mwandishi wa habari gazeti la Uhuru alisema kuwa baadhi ya waandishi waliiomba RUWASA kuwawezesha usafiri ili kuitembelea miradi kuona utekelezaji wake na changamoto za upatikanaji wa maji katika maeneo ya vijijini.

"Tuliomba RUWASA katika mkoa wetu wa Mara kutuwezesha usafiri kutembelea miradi ya maji vijijini kwasababu tulitamani sana kuitembelea miradi ya maji lakini ukosefu wa fedha za usafiri tukakwama ikatubidi tuombe RUWASA.

" Wametukubalia ombi letu,jumatatu tutaizungukia miradi kwa siku sita kwenye wilaya sita kuona inavyofanya kazi na jitihada za serikali katika kutatua changamoto za maji pamoja na kuibua changamoto za maji zinazowakabili wananchi wa vijijini na kutoa elimu ya umuhimu wa utunzaji wa miundombinu ya maji kisha tuandike habari na kuziripoti kwenye vyombo vya habari ili kuifikia jamii na serikali"alisema Msamba.

Meneja Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) mkoa wa Mara,Mhandisi Tulinumpoki Mwakalukwa alisema kuwa waandishi watatembelea wilaya hizo kama walivyoomba ili kuona miradi iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa.

"RUWASA mkoa wa Mara una wilaya 6 za Bunda, Butiama, Musoma, Rorya, Tarime na Serengeti, Kwa mwaka huu 2021/22 tunatekeleza jumla ya miradi mipya 41 yenye thamani ya Sh.16.7 Bilioni. Aidha tumepata nyongeza ya miradi 9 yenye thamani ya sh.4.5 Billion kwa mpango wa COVID-19(Uviko).

"RUWASA ni Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira vijijini. RUWASA inasimamiwa na Bodi ya wakurugenzi, na Mkurugenzi mkuu chini ya wizara ya maji,makao yake makuu yapo Dodoma, na ina ofisi ngazi ya mkoa inayoongozwa na Meneja wa Mkoa,na ofisi ya wilaya inayoongozwa na Meneja wa Wilaya" alisema Mwakalukwa.

Meneja huyo alisema kuwa miradi ya maji inasimamiwa na Jumuiya za watumiaji wa maji (CBWSO) vinavyoratibiwa na Meneja wa Wilaya nakwamba waandishi wa habari wataishuhudia miradi hiyo na kupata taarifa kwa kila mradi unaotekelezwa kwenye wilaya hizo.

Mwakalukwa ameongeza kuwa RUWASA inaahidi kutoa  ushirikiano kwa vyombo vya habari kama wadau muhimu wa kuihabarisha na kuielimisha jamii kuhusu ujenzi na uendeshaji wa miradi ya Maji vijijini Ili kuwa na miradi endelevu. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com