Mfanyabiashara Remigius Patrick akizungumza wakati wa kikao hicho
Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba Hamid Njovu akizungumza kwenye kikao hicho.
**
Na Mbuke Shilagi - Bukoba
Baadhi ya Wafanyabiashara wa Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera wameiomba serikali iwapunguzie makato ya Ushuru wa Huduma (Service Levy) kulingana na biashara na mtaji wa kila mfanyabiashara.
Hayo yamebainishwa leo katika kikao cha wafanyabiashara kilicholenga kujadili changamoto zinazohusiana na Ushuru wa Huduma (Service Levy) kilichoitishwa na Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Hamid Njovu na kuhudhuriwa na viongozi na watendaji mbalimbali wa serikali, wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Moses Machali.
Mmoja wa wafanyabiashara hao Remigius Patrick amesema kuwa kila mfanyabiashara anatofauti na mwingine, hivyo serikali iliangalie hilo upya na kuwapunguzia kulingana na mauzo ya kila mfanyabiashara.
Patrick ameongeza kuwa kiwango cha Ushuru ambacho ni asilimia 0.3 ya mauzo kwa kila mfanyabiashara kimekuwa ni kikubwa sana ambacho kwa mwingine ambaye mauzo yake ni madogo na ya chini kitamfanya kutopata faida na kutoifurahia biashara yake.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba Hamid Njovu amesema kuwa ushuru huo haupunguzwi kwa kiwango sawa kwa wafanyabiashara, bali viwango vinapunguzwa kwa mmoja mmoja ambaye atapiga mahesabu na kuona kiwango ni kikubwa, hivyo anaweza kumwandikia barua Mkurugenzi akilalamikia hilo.
"Mfanyabiashara akishaniandikia barua ya malalamiko, nitaiwasilisha kwa madiwani, baada ya ufuatiliaji na majadiliano inaweza kuamriwa mfanyabiasha husika apunguziwe ama asipunguziwe, na hii itatokana na nyaraka zitakazowasilishwa", amesema Njovu.