Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WATOTO MAPACHA WACHANGA WATUPWA DAMPO MAKABURI YA MAJENGO SHINYANGA MJINI

Baadhi ya wananchi wakiwa eneo la tukio wakishuhudia watoto mapacha waliotupwa na mama yao kwenye Ghuba la taka lililopo Majengo Makaburini Manispaa ya Shinyanga.

Na Marco Maduhu, Shinyanga

Watoto wachanga mapacha wamefariki dunia baada ya kutupwa na mama asiyefahamika katika eneo la kuhifadhia taka (ghuba) lililopo Mtaa wa Majengo Makaburini kata ya Kambarage Manispaa ya Shinyanga.

Tukio hilo limebainika leo Jumatatu Machi 14,2022 majira ya saa 12 alfajiri baada ya waokota uchafu kufika kwenye Ghuba hilo, na kuanza kutafuta mali mbalimbali ndipo walipofunua mfuko mmoja wakijua huenda kuna vitu vizuri na kukuta watoto  wachanga wakiwa tayari wamefariki dunia.

Mmoja wa majirani wa eneo hilo la kuhifadhia taka Costantine Samwel, alisema mara baada ya waokota uchafu kuona watoto hao ndipo wakaanza kupiga kelele na wao wakatoka kushuhudia tukio hilo na kukuta watoto wakiwa ndani ya mfuko wameshafariki dunia.

“Ukiviangalia vizuri vichanga hivi huyu mama alivitoa vikiwa bado havijafikisha miezi Tisa, sababu hapa pembeni kama unavyoona kuna sindano na baadhi ya vitu ambavyo vimetumika kumtolea watoto hawa,”alisema Samweli.

Nao baadhi ya akina mama ambao walifika eneo hilo la tukio, kwa nyakati tofauti walilaani kitendo hicho huku wengine wakiangua kilio, na kuiomba Serikali imtafute mwanamke ambaye amefanya unyama huo, na wamchukulie hatua kali za kisheria na liwe fundisho kwa wengine.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa huo wa Majengo Majid Issa, alisema tukio kama hilo la kutupa watoto katika ghuba hilo la uchafu ni la pili, na kutoa wito kwa wanawake kama mimba zao au watoto wanakataliwa na wanaume wasiwafanyie ukatili, bali wawapeleke kwenye vituo vya malezi ya watoto.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Shinyanga George Kyando, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, na kubainisha wanafanya uchunguzi ili kumbaini mwanamke aliyefanya unyama huo.

Chanzo- Shinyanga Press Club blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com