Na Mbuke Shilagi-Kagera.
Takriban watu 2,557 wamegundulika kuwa na ugonjwa wa kifua kikuu (TB) katika Mkoa wa Kagera kwa mwaka 2021.
Takwimu hizo zimetolewa na Meneja wa Mradi wa Kifua Kikuu na Ukimwi kutoka shirika la MDH Kagera Dkt. Frank Marugu wakati akizungumza katika maadhimisho ya siku ya Kifua kikuu Duniani yaliyofanyika kimkoa katika uwanja wa Uhuru katika Manispaa ya Bukoba.
Dkt. Marugu amesema kuwa watu hao waliogundulika kuwa na TB mwaka 2021, watu 484 wamegundulika katika wilaya ya Bukoba, Muleba wagonjwa 440, Kyerwa wagonjwa 394, Biharamulo wagonjwa 363, Karagwe wagonjwa 345, Ngara wagonjwa 316, pamoja na Missenyi wagonjwa 215.
Ameongeza kuwa kwa mwaka 2021 Mkoa wa Kagera umefanikiwa kuwaweka kwenye matibabu wagonjwa hao kwa asilimia 92.
Aidha amesema kuwa mpaka sasa watu 810 wamegundulika kuwa na ugonjwa wa kifua kikuu kwa mwaka 2022, huku akiwataka wanannchi kujitokeza kupima ugonjwa huo kwa wingi pale wanapoona dalili mojawapo ili kupata matibabu haraka kwa sababu TB inatibika.
Ametaja baadhi ya dalili za kifua kikuu kuwa ni kukohoa mfululizo, kutokwa na jasho na kutokwa na makohozi yaliyochanganyikana na damu.