WAZIRI MCHENGERWA -MAANDALIZI SERENGETI 2022 YAMEKAMILIKA, WASANII ONESHENI UMAHIRI WENU


**************** 

Na. John Mapepele 

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa ametoa wito kwa wasanii wote wa muziki wanakaotumbuiza kwenye tamasha kubwa la historia la Serengeti Machi 12-13, 2022 jijini Dodoma kuonyesha umahiri wao ili kuutangaza utamaduni wa kitanzania duniani na kuliingizia taifa mapato. 

Mhe. Mchengerwa amesema hayo leo Machi 9, 2022 ambapo amefafanua kuwa lengo la tamasha hilo pamoja na kutoa burudani ni kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia muziki wa Tanzania. 

“Tumekusudia kufanya mapinduzi makubwa kwenye sekta zetu kwa kuzifanya ziwanufaishe wasanii wenyewe na Taifa kwa ujumla hivyo tamasha hili linakwenda kufungua Tanzania kwenye ngazi za kimataifa”. Amefafanua 

Mh.Mchengerwa amesema zaidi ya wasanii mia moja watakutanishwa katika siku mbili za kuitikisa dunia kupitia tamasha hilo ambalo limeratibiwa na Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo. 

Katibu Mkuu wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Dkt, Hassan Abbasi amesema maandalizi ya tamasha hilo yanaendelea vizuri tayari kwa ajili ya burudani hiyo kabambe ambayo haijawahi kutokea katika miaka ya hivi karibuni. 

“Nisema tu kwamba kila kitu kinakwenda vizuri ni matarajio yetu watu watashiriki kikamilifu kwenye tamasha hili ambalo limeratibiwa kwa kiwango cha juu kabisa”. Ameongeza Dkt. Abbasi 

Amewataka wakazi wa Dodoma na watanzania kwa ujumla kushiriki ili kujionea vipaji na vipawa vya wasanii wa kitannzania. 

Aidha, Mhe. Mchengerwa amewataka wasanii watakaoshiriki kutambua kuwa dunia itakuwa ikiwafuatilia kupitia vyombo mbalimbali vya habari hivyo ni fursa ya kipekee ya kuonyesha uwezo wao ili waweze kunufaika na kazi zao. 

Tayari wasanii mbalimbali wameshatua jijini Dodoma kwa ajili ya maandalizi ya kutoa burudani kwenye tamasha hili.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post