*************************
Na. John Mapepele
Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirkiana na wadau wa mbalimbali wa michezo nchini leo Machi 29, 2022 wanaadhimisha kilele cha wiki ya Rais Samia ikiwa ni kampeni maalum ya kuelimisha umma, kujadili na kutafakari mafanikio makubwa yaliyopatikana kwenye mwaka mmoja wa utendaji wake tangu aingie madarakani kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Machi 19, mwaka jana.
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa ndiye Mgeni Rasmi atakayeongoza kongamano hilo la michezo katika kuadhimisha mwaka mmoja wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe, Samia Suluhu Hassan katika sekta ya Michezo.
Kongamano hilo linatarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam katika Uwanja wa Benjamini Mkapa kuanzia saa nane mchana na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa michezo nchini.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo. Yusuph Singo Omary, wadau mbalimbali wa michezo ikiwa ni pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo. Dkt, Hassan Abbasi watatoa mada kwenye kongamano hilo.
Amewataja wadau wengine watakaowasilisha mada kuwa ni pamoja na Peter Sarungi ambaye ni Rais wa TAFF, Jackson Ndaweka ambaye ni Kaimu Katibu Mkuu Shirikisho la Riadha nchini, Salum Madadi ambaye ni Mkurugenzi wa Mashindano wa Shirikisho la Soka nchini (TFF) na Amina Mfaume ambaye ni Mkurugenzi wa Ufundi wa Chama cha Kuogelea (TSA).
Aidha, amesema lengo la Kongamano hilo ni kuelezea mafanikio ya mwaka mmoja wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe, Samia Suluhu Hassan kwenye Sekta ya Michezo.
‘Kongamano hili tumeliratibu vizuri ili kuonyesha mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi hiki cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wetu Kipenzi, mama Samia Suluhu Hassan” ameongeza Mkurugenzi Omary.
Mkurugenzi Singo amesema baada ya kongamano hilo kutakuwa na mchezo wa kirafiki kati ya Sudan na Taifa Stars ambao utachezewa katika Uwanja wa Benjamini Mkapa.
Ametoa wito kwa wadau mbalimbali wa soka na wapenda michezo kujitokeza kushiriki kwenye kongamano hilo la aina yake na baadaye kwenye mechi dhidi ya Sudan na Taifa Stars ili kuja kujionea burudani na kuishangilia timu ya Taifa.