Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Breaking : SERIKALI YATANGAZA AJIRA MPYA 44,096....WATUMISHI ELFU 90 WAPANDISHWA VYEO, 6026 WABADILISHWA KADA

Na Dotto Kwilasa, Malunde1 Blog-DODOMA


KATIKA  kuboresha Utumishi wa Umma,Serikali imeajiri watumishi wapya 44,096, kupandisha vyeo watumishi 92,619 na kubadilisha kada za watumishi 6,026 kwa mwaka wa fedha 2021/2022 huku ikitoa kipaumbele katika Sekta za Elimu na Afya kuongeza tija, moyo wa kufanya kazi kwa bidii na uwajibikaji wa hiari kwenye Utumishi wa Umma. 

 

Hatua hiyo ni utekelezaji wa ahadi ya  Serikali katika eneo la uboreshaji wa maslahi ya watumishi kupitia uamuzi wake wa kutoa idhini ya kuajiri watumishi wapya, kupandisha vyeo watumishi pamoja na kubadilisha kada ili kuziwezesha taasisi za umma kuwa na rasilimaliwatu ya kutosha yenye ujuzi na maarifa stahiki katika kuufanya Utumishi wa Umma kuwa na tija na utoaji wa huduma bora kwa katika maendeleo na ujenzi wa uchumi wa nchi. 


Akieleza taarifa hiyo leo Aprili 12,2022 Jijini Dodoma,Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Jenista Mhagama amesema kati ya nafasi 44,096  za ajira mpya, Serikali kupitia Taasisi zinazotumia Mfumo wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (Human Capital Management Information System-HCMIS) imeshaajiri watumishi  12,336  wakiwemo watumishi 11,492 wa ajira mpya na watumishi 844 wa ajira mbadala  hadi sasa. 


Amesema,utekelezaji wa ajira hizo utaigharimu Serikali kiasi cha shilingi Bilioni  26,297,541,175.00 kwa mwezi sawa na Shilingi 315, 570,494,100.00 kwa mwaka.


Amesema,wamezingatia mgawanyo wa ajira katika Sekta nyingine zikiwemo Kilimo, Maji, Mifugo, Uvuvi pamoja na maeneo mengine yenye uhitaji ambapo Sekta ya Kipaumbele ya Elimu imetengewa  jumla ya nafasi 12,035 zikiwemo nafasi 9,800 kwa ajili ya Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari.


"Mchakato wa ajira hizi utasimamiwa na Ofisi ya Rais, TAMISEMI ambapo nafasi 2, 235 kwa ajili ya Wahadhiri wa Vyuo Vikuu na Vyuo vya Elimu ya Juu pamoja Wakufunzi wa Vyuo vilivyopo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,mchakato wa ajira hizi utasimamiwa na Taasisi husika za elimu kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma,"amesema.


Waziri Mhagama pia ametaja sekta ya  Kipaumbele ya Afya kuwa imekasimiwa nafasi za ajira 10,285 zinazojumuisha nafasi 7,612 kwa ajili ya Hospitali, Vituo vya Afya na Zahanati zilizopo katika Mamlaka za Serikali za Mitaa. 


Amefafanua kuwa mchakato wa ajira hizi utasimamiwa na Ofisi ya Rais, TAMISEM na kwamba nafasi 1650 kwa ajili ya kuajiri watumishi wa kada za Afya katika Hospitali za Kanda, Hospitali za Rufaa za Mikoa na kwamba mchakato wa ajira hizo utasimamiwa na Wizara ya Afya; na nafasi 1023 kwa ajili ya Vyuo vya Afya, Hospitali nyingine za kimkakati na zile za Mashirika ya Dini (District Designated Hospitals-DDHs) na Hiari ( Voluntary Agency-VAHs) zenye mkataba na Serikali. 


"Mchakato wa ajira hizi utasimamiwa na Wizara ya Afya kwa Vyuo vya Afya na Hospitali nyingine za kimkakati na Ofisi ya Rais, TAMISEMI  kwa Hospitali za DDHs na VAHs,nafasi  2,392 zinatarajiwa kujazwa kwenye Sekta zingine za kipaumbele ikiwa ni pamoja na kada za Kilimo nafasi za ajira 814. ; Kada za Mifugo  nafasi 700;Kada za Uvuvi nafasi 204; Kada za Maji  nafasi 261",amesema.


Waziri huyo pia amesema Kada za Sheria zimepewa nafasi 513 huku akieleza kuwa chakato wa ajira hizo utasimamiwa na Wizara pamoja na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.


Pamoja na hayo ajira nyingine ni nafasi 7,792 kwa ajili ya kuajiri Watumishi wa kada nyingine kwenye Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Taasisi nyingine za Umma na mchakato wa ajira hizo utasimamiwa na Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Taasisi nyingine za Umma pamoja na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.


UPANDISHAJI VYEO NA UBADILISHAJI WA KADA

Kwa  kutambua umuhimu wa rasilimaliwatu na kwa lengo la kuboresha maslahi ya watumishi, Serikali  pia itawapandisha vyeo/madaraja watumishi 92,619  na Serikali itatumia jumla ya Shilingi 23,078,224,169.50 kwa mwezi sawa na Shilingi 276, 938,690,034.00 kwa mwaka na kuwabadilisha vyeo/kada (Recategorization) watumishi 6,026 waliotengewa Ikama na Bajeti ya Mishahara kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 kuanzia tarehe 01 Mei, 2022.


Amebainisha gharama itakayotumika  ni  Shilingi 824, 441,522.00 kwa mwezi sawa na Shilingi 9,893,298,264.00 kwa mwaka. 

 

Aidha, jumla ya watumishi 25,412 watakuwa wamebadilishiwa kada katika kipindi tajwa na kueleza Kuwa hayo ni  mafanikio makubwa na inadhihirisha nia thabiti ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kushughulikia haki na stahiki za Watumishi wa Umma. 


"Niwataarifu kwamba kwa mara ya kwanza, upandishaji vyeo kwa watumishi 92,619 utafanywa  moja kwa moja na Mfumo wa Mpya wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (HCMIS) kwa kutumia Orodha ya Watumishi wenye sifa (Eligibility List) iliyopo kwenye Mfumo huo. 


Aidha Waajiri watawajibika kuandaa na kuwapa barua za kupanda cheo baada ya watumishi hao kupokea mishahara mipya inayoendana na cheo/daraja jipya kwa ajili ya kumbukumbu za kiutumishi,"alifafanua Waziri Mhagama.


Waziri huyo mwenye dhamana ya Utumishi  amesema,uidhinishaji huo utawezesha watumishi wote 92,619 kupata mishahara ya vyeo vipya kwa wakati moja, hivyo kuondoa ucheleweshaji katika upandishaji wa vyeo pamoja na uzalishaji wa malimbikizo ya mishahara.


"Nitumie fursa hii kuwakumbusha waajiri kupitia tena Orodha ya Watumishi wenye sifa (Eligibility List) iliyopo kwenye Mfumo wa HCMIS kwa lengo la kujiridhisha iwapo watumishi husika bado wana sifa na vigezo vya kupandishwa vyeo hadi sasa,naziagiza Mamlaka za Ajira, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Wizara ya Afya pamoja na Sekretarieti ya Ajira Katika Utumishi wa Umma kuhakikisha wanaendesha michakato ya ajira hizi kwa uwazi, weledi, uadilifu pamoja na kutoa fursa sawa kwa waombaji wote,"amesema.


Waziri huyo pia ametumia nafasi hiyo kuwaasa baadhi ya waajiri kutotumia fursa hiyi kuajiri watumishi wazembe au wasiotekeleza majukumu yao kikamilifu kwa lengo la kujaza nafasi kwani jambo hili halikubaliki na halitavumiliwa kwa namna yeyote. 


"Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora itafuatilia mchakato mzima wa ajira hizi hatua kwa hatua ili kuhakikisha Serikali inapata watumishi wenye sifa na ubora ambao wapo tayari kulitumika Taifa,upande wa upandishaji vyeo na ubadilishaji kada, nawakumbusha waajiri wote kuhakikisha zoezi tajwa linafanyika kwa haki na kwa wakati kwa kuzingatia sifa na vigezo vilivyoainishwa katika Miundo ya Utumishi ,"amesema.


Pia amewataka waajiri wote nchini wahakikishe watumishi wa umma wapya wote watakaoajiriwa wanapata mafunzo elekezi (Induction Course) kupitia Chuo cha Utumishi wa Umma kabla ya kupangiwa vituo vya kazi kama ilivyoelekezwa na Serikali.  

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com