Askofu Wolfgang Pisa, Jimbo Katoliki la Lindi, Tanzania
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko ameridhia ombi lililowasilishwa kwake na Askofu Bruno Pius Ngonyani wa Jimbo Katoliki la Lindi, Tanzania la kutaka kung’atuka kutoka madarakani.
Wakati huo huo, Baba Mtakatifu amemteua Mheshimiwa Sana Padre Wolfgan Pisa O.F.M. Cap. kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Lindi. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mteule Wolfgan Pisa O.F.M. Cap. alikuwa ni Paroko usu wa Parokia Kwangulelo Jimbo kuu la Arusha na Jaalimu Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino Tanzania, SAUT, Tawi la Arusha.
Itakumbukwa kwamba, Askofu mteule Wolfgang Pisa O.F.M. Cap. alizaliwa tarehe 6 Julai 1965 huko Karatu, Jimbo Katoliki la Mbulu. Baada ya masomo na malezi ya kitawa Lusaka, Zambia na Chuo Kikuu Kishiriki cha Jordan, Morogoro aliweka nadhiri za daima tarehe 15 Agosti 1998 na hatimaye, kupewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 1 Septemba 1999.
Tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre amewahi kutekeleza shughuli zake za kichungaji na kitume kama Jalimu na Mlezi, Seminari Ndogo ya Maua, Jimbo Katoliki la Moshi kati ya mwaka 1999 hadi mwaka 2000. Baadaye alitumwa na Shirika kujiendeleza zaidi katika masomo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na hapo akajipatia Shahada ya Uzamili.
Akateuliwa kuwa Gambera wa Seminari Ndogo ya Maua kati ya mwaka 2005-2008. Baadaye alijiendeleza zaidi katika masomo ya maadili Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Marekani, Catholic University of Amerika huko Washington, DC kati ya mwaka 2009 hadi mwaka 2011.
Akachaguliwa kuwa Mkuu wa Shirika la Wakapuchini Kanda ya Tanzania na kuwaongoza tangu mwaka 2011 hadi mwaka 2017. Baadaye kati yam waka 20017-2019 akarejea tena darasani huko Catholic University of Amerika huko Washington, DC na kujipatia Shahada ya Uzamili katika Maadili.
Amewahi kufanya shughuli zake za kifchungaji Parokiani Kibaigwa, Jimbo kuu la Dodoma kati ya mwaka 2019-2020. Tangu wakati huo, hadi kuteuliwa kwake, Askofu mteule Wolfgang Pisa O.F.M. Cap. alikuwa ni Paroko usu wa Parokia Kwangulelo Jimbo kuu la Arusha na Jaalimu Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino Tanzania, SAUT, Tawi la Arusha.