Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BAKWATA MWANZA WAZINDUA HARAMBEE YA KUCHANGIA UJENZI WA VITUO VYA AFYA...KIVULINI YACHANGIA MILIONI 2

 

Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (BAKWATA) Mkoa Mwanza limezindua harambee kwa ajili ya kufanikisha upatikanaji wa fedha ili kukamilisha ujenzi wa Vituo vya Afya vya Baraza hilo katika Wilaya zote mkoani Mwanza.

Uzinduzi wa harambee hiyo umefanyika Jumamosi Aprili 23, 2022 katika Msikiti wa BAKWATA Mkoa Mwanza uliopo Mirongo jijini Mwanza na kuhudhuriwa na waumini na viongozi wa dini, Serikali pamoja na wadau mbalimbali.

Sheikh wa BAKWATA Mkoa Mwanza, Hassan Kabeke amesema ujenzi wa vituo hivyo vya afya mkoani Mwanza ni sehemu ya utekelezaji wa mpango mkakati wa miaka mitano wa baraza hilo ulionza kutekelezwa mwaka 2019 hadi 2023.

Amesema awali baraza hilo halikuwa na kituo cha afya hata kimoja jambo ambalo liliifanya jamii ya kiislamu kuonekana iko nyuma katika suala la maendeleo na kwamba huu ni wakati mwafaka wa kuondoa aibu hiyo.

“Hatukuwa na kituo cha afya hata kimoja, hatuwezi kuendelea kuwa watu wa kuchekwa hivyo niwasihi kila mmoja wetu aguswe na kuchangia kwenye mradi huu ambapo harambee rasmi itafanyika Julai 30, 2022”, amesema Sheikh Kabeke.

Katika hatua nyingine Sheikh Kabeke ameomba Serikali kuunga mkono jitihada hizo kwani BAKWATA inachofanya ni kuondoa majungu na manung’uniko ambayo yamekuwa yakijitokeza kwa jamii ya kiislamu inapoona Serikali ikitoa fedha kwenye taasisi za afya zinazomilikiwa na dini nyingine.

Katibu wa BAKWATA Mkoa Mwanza, Sheikh Ramadhani Chanila amesema utekelezaji wa ujenzi wa vituo vya afya vya BAKWATA mkoani Mwanza tayari umeanza tayari umeanza kupitia michango ya wadau mbalimbali ambapo kiasi cha shilingi milioni 25 kimekusanywa na kuanzisha ujenzi katika Wilaya ya Ilemela, Sengerema na Misungwi

“Katika Wilaya ya Ilemela ujenzi umefikia hatua ya madirisha, Sengerema hatua ya renta na Misungwi katika hatua ya msingi. Katika Wilaya za Kwimba na Magu zoezi la kutambua viwanja vya utekezaji wa mradi linaendelea”, amesema Sheikh Chanila na kuongeza kuwa awamu ya kwanza ya mradi huo ambayo ni majengo inaratajiwa kugharimu shilingi bilioni 2.8.

Miongoni mwa wadau waliohudhuria harambee hiyo ni pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la KIVULINI, Yassin Ally ambaye amewakumbusha waumini wa dini ya kiislamu kuwa wanapotimiza ibada ya Swala wasisahau pia kutimiza wajibu wao ikiwemo kuwajibika katika malezi bora katika familia ili kuondoa wimbi la watoto wa mitaani huku akiunga mkono harambee hiyo kwa kuchangia shilingi milioni mbili.

Akizindua harambee hiyo iliyoambatana na Baraka za mvua, Mkuu wa Mkoa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel amesema hilo ni jambo la Mwenyezi Mungu hivyo yeyoye atakayechangia atabarikiwa ikizingatiwa huu ni Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ambapo ametumia fursa hiyo kutoa rai kwa taasisi mbalimbali ikiwemo za kifedha kuunga mkono ujenzi huo.

“Kwa kuwa hili ni jambo la Mwenyezi Mungu acha nipambane, nilitekeleze na nitabarikiwa mimi na familia yangu. Nina watoto saba, niliomba 12, huwezi kujua nitapata wangapi kwa sadaka hii” ,alidokeza Mhandisi Gabriel akiwahamasisha wadau mbalimbali kuchangia harambee hiyo.

Uzinduzi wa harambee hiyo umefanikisha upatikanaji wa fedha taslimu na ahadi kiasi cha shilingi milioni 28.7 ambapo wadau wamehimizwa kuchangia kupitia Benki ya CRDB akaunti nambari 01 50 65 81 86 00 jina BAKWATA HARAMBEE ambapo kilele chake ni Julai 30, 2022.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Mkuu wa Mkoa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel akitambulisha akaunti ya benki kwa ajili ya kupokea michango ya harambee kutoka kwa wadau mbalimbali ili kufanikisha ujenzi wa vituo vya afya vya BAKWATA mkoani Mwanza.
Mkuu wa Mkoa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel akijionea ramani za ujenzi wa vituo vya afya vya BAKWATA mkoani Mwanza pamoja na kutambulisha nambari za kupokea michango kutoka kwa wadau.
Mkuu wa Mkoa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel akizungumza kwenye uzinduzi wa harambee ya kuchangia ya vituo vya afya vya BAKWATA mkoani Mwanza.
Waumini wa dini ya kiislamu pamoja na wadau mbalimbali wakifuatilia harambee hiyo iliyofanyika Msikiti wa BAKWATA jijini Mwanza.
Sheikh wa BAKWATA Mkoa Mwanza, Hassan Kabeke akizungumza kwenye uzinduzi wa harambee hiyo.
Katibu wa BAKWATA Mkoa Mwanza, Ramadhani Chanila akisoma taarifa ya utekelezaji mradi wa vituo vya afya vya BAKWATA mkoani Mwanza wakati wa uzinduzi wa harambee ya kuchangia mradi huo.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu Mkoa Mwanza, Amina Masenza ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa Mstaafu akiwahamasisha akina mama kuchangia harambee hiyo akisema ujenzi wa huokoa maisha ya akina mama hususani wakati wa kujifungua.
Mkuu wa Mkoa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel akipokea kadi nambari moja kufungua jaramba la uchangiaji ujenzi wa vituo vya afya vya BAKWATA mkoani Mwanza.
Sheikh wa BAKWATA Mkoa Mwanza Hassan Kabeke (kushoto) akimkabidhi Mkuu wa Mkoa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel (kulia) kadi 70 kwa ajili ya kuwaalika wadau mbalimbali ili wafanikishe harambee ya ujenzi wa vituo vya afya vya BAKWATA mkoani Mwanza.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la KIVULINI, Yassin Ally akitoa salamu wakati wa harambee hiyo ambapo amechangia shilingi milioni mbili ili kufanikisha ujenzi wa vituo vya afya vya BAKWATA kila Wilaya mkoani Mwanza.
Uzinduzi wa harambee hiyo umefanikisha upatikanaji wa fedha taslimu na ahadi kiasi cha shilingi milioni 28.7 ambapo wadau wamehimizwa kuchangia kupitia Benki ya CRDB akaunti nambari 01 50 65 81 86 00 jina BAKWATA HARAMBEE ambapo kilele chake ni Julai 30, 2022.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com