Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BARRICK YAIBUKA MSHINDI BORA TUZO ZA WIKI YA AFYA NA USALAMA MAHALI PA KAZI (OSHA)


Wafanyakazi wa Kampuni ya Barrick Tanzania wakifurahia tuzo walizojishindia katika maonesho ya OSHA jijini Dodoma.
 **

Kampuni ya Barrick Tanzania, imeshinda tuzo nane katika hafla ya utoaji wa Tuzo za Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) ya mwaka 2022 iliyofanyika jijini Dodoma huku Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu, ukinyakua Tuzo ya mshindi wa jumla ya kufuata kanuni za Usalama ipasavyo (the Top OSHA Compliance Award).

Mbali na ushindi huo mkubwa, Bulyanhulu, pia iliibuka kidedea kwa kushinda Tuzo za kuelezea kwa ufasaha shughuli za kampuni, na ushindi wa jumla wa mshiriki wa maonesho na katika kipengele cha Ubunifu katika uchimbaji wa Madini katika maonesho ya OSHA ya mwaka huu.

Kwa upande wa Mgodi wa Barrick North Mara, ulishinda Tuzo za juu katika Mpango Bora wa uhamasishaji kanuni za Afya na Usalama na wadau wake na imeshinda kipengele cha Huduma za Usalama. Pia ilikuwa Mshindi wa pili katika kipengele cha uhamasishaji kuzingatia Usalama kwa Wajasiriamali Wadogo (SMEs) na Tuzo la OSHA katika Sekta ya Madini.

Maonesho ya mwaka huu ya OSHA yalifanyika katika Viwanja vya Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete mjini Dodoma. 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu Mheshimiwa Profesa Joyce Lazaro Ndalichako, alikuwa mgeni Rasmi katika hafla ya utoaji wa Tuzo za mwaka huu.

Ushindi wa Barrick Tanzania wa mwaka 2022 unatokana na mafanikio ya kampuni ya 2021 ambapo ilipata ushindi wa jumla wa Tuzo za Utekelezaji wa Majukumu ya kusaidia Jamii (CSR),Mshiriki Bora katika maonyesho na Tuzo ya Ubunifu katika Usalama na Afya (OHS Innovation).

Akiongea baada ya hafla ya utoaji wa Tuzo hizo, Meneja wa Barrick Tanzania, Georgia Mutagahywa alisema, "Huu ni wakati mzuri kwa Barrick kwa ushindi wa Tuzo hizi ambao unadhihirisha kazi kubwa inayofanywa na Wafanyakazi wetu na Washirika wetu kibiashara ili kuifanya Kampuni kuwa mahali salama na pazuri pa kufanya kazi.

"Usalama ni suala kuu tunalolipa kipaumbele cha kwanza, hivyo tumejitolea kufanya kila kuweka mifumo itakatayofanikisha kusiwepo na matukio ya kujeruhiwa katika maeneo yetu ya Kazi", alisema Mutagahywa”.

 Tuzo hizi ni ushuhuda wa dhamira ya Kampuni ya kuhakikisha kanuni za usalama zinatekelezwa na kuzingatiwa wakati wote na Wafanyakazi , Washirika na Wadau wake.

Afisa Afya wa mgodi wa Bulyanhulu,Dk. Said Kudra, akipokea Tuzo kutoka kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu Mheshimiwa Profesa Joyce Lazaro Ndalichako (kushoto) katikati ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo Patrobas Katambi.
Afisa Afya wa mgodi wa Bulyanhulu,Dk. Said Kudra,akifurahia tuzo na baadhi ya wafanyakazi wenzake.
Wafanyakazi wa Mgodi wa North Mara wakifurahia Tuzo walizojishindia katika maonesho ya OSHA jijini Dodoma.
Wafanyakazi wa Mgodi wa Bulyanhulu wakifurahia tuzo walizojishindia katika maonesho ya OSHA jijini Dodoma.
Wafanyakazi wa Barrrick walioshiriki maonesho ya OSHA wakiwa katika picha ya pamoja baada ya Kampuni kushinda Tuzo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com