Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko
Na. Tito Mselem, Dodoma
Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko ametatua mgogoro wa wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu katika kijiji cha Nayu Kata ya Dabalo wilayani Chamwino mkoa wa Dodoma.
Mgogoro huo ulio dumu kwa zaidi ya mwaka mmoja ulitokea baada ya wachimbaji wadogo kugundua madini ya dhahabu katika Mlima wa Nayu uliopo ndani ya Hifadhi za Misitu ambapo Mwekezaji Sarehe Mohamed alitangulia kukata leseni ya uchimbaji mdogo wa madini katika eneo hilo kabla ya wagunduzi.
Inaelezwa kuwa, kijiji cha Nayu kina jumla ya leseni 16 ambazo Mwekezaji ana leseni 8 na wanakijiji wana leseni 8 ambazo zinamilikiwa kihalali kwa kufuata Sheria na Taratibu zilizowekwa na Serikali.
Akizungumza katika Mkutano wa hadhara na wachimbaji wadogo wa madini, Dkt. Biteko amesema Wizara ya Madini inatoa leseni za uchimbaji madini katika maeneo mbalimbali, pale inapotokea leseni ipo ndani ya Hifadhi za Misitu ni lazima mmliki apate Kibali kutoka Mamlaka ya Uhifadhi wa Misitu Tanzania (TSF).
“Sisi Wizara ya Madini tunatoa leseni kwenye maeneo yenye madini lakini ukitaka kuchimba kwenye Hifadhi za Misitu lazima upate Kibali kutoka TSF ili uchimbe kwa utaratibu ambapo Wataalam wa Misitu watakagua eneo na watakupa Kibali cha Tathimini ya Athari za Mazingira ili kuhakikisha mazingira yanabaki salama,” amesema Dkt. Biteko.
Aidha, Dkt. Biteko amemtaka Mwekezaji wa madini ya dhahabu katika kijiji hicho Sarehe Mohamed kujenga mahusiano mazuri na wanakijiji aliowakuta katika eneo hilo ili afanye kazi kwa ushirikiano.
Dkt. Biteko amesema, Rais wa Nchi hii Mhe. Samia Suluhu Hassan anataka kuona wachimbaji wadogo wa madini wananufaika na rasilimali zilizopo nchini, anataka kuwaona wachimbaji wadogo wanatoka kwenye uchimbaji mdogo kwenda wa kati na hatimaye kuwa wachimbaji wakubwa.
“Mwenyezi Mungu amewapa bahati ya kuwa na madini katika eneo lenu, niwaombe mchimbe madini haya kwa kupendana na kushirikiana, madini yawaunganishe acheni mambo ya kufitianiana na kuleteana majungu chimbeni kwa ushirikiano,” amesisitiza Dkt. Biteko.
Sambamba na hayo, Dkt. Biteko amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Gift Msuya pamoja na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma Chagwa Marwa kufungua Soko la Madini katika kijiji cha Nayu ili kuwarahisishia wachimbaji wadogo mahali pa kuuzia madini yao na kusaidia kijiji kupata tozo kutoka kwenye madini yaliyopo kwene eneo lao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Gift Msuya amesema migogoro mingi inayotokea katika eneo hilo inasababishwa na ukosefu wa elimu kwa wachimbaji wadogo, ambapo mara nyingi wakigundua madini wanaanza kuyachimba bila kufuata Sheria na Taratibu ikiwemo kukata leseni.
Naye, Mbunge wa Chamwino ambaye pia ni Naibu Waziri wa Utumishi na Utawala Bora Deogratius Ndejembi amempongeza Waziri wa Madini kwa kukubali kuongozana naye ili kutatua mgogoro huo uliodumu kwa muda mrefu.
Madini ya dhahabu katika kijiji cha Nayu yaligunduwa na wachimbaji wadogo ndani ya Hifadhi ya Misitu Mwaka 2020 hali iyopelekea wananchi zaidi ya mia saba kuingia katika eneo hilo kutafuta madini.