Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RIPOTI YA CAG YAIBUA MADUDU KWENYE MFUMO WA BIMA YA AFYA, ABAINI WANAUME KUJIFUNGUA

 Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali (CAG)Charles Kichere akiwasilisha ripoti yake kwa Waandishi wa habari  Leo Jijini hapa mara baada ya kuwasilisha ripoti hiyo Bungeni ambayo ameielezea kuwa imeibua ubadhilifu wa fedha kwenye Taasisi mbalimbali.

****

Na Dotto Kwilasa, Malunde1 Blog-DODOMA

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ametoa  ripoti yake kwa mwaka wa fedha ulioishia June 30,2021 inayoonesha madudu kwenye mfumo wa bima ya Afya ambapo madai 56 yanayoonesha wanaume walipata huduma ya upasuaji (C/S) au huduma za kawaida za kujifungua wakati huduma hizi hutolewa kwa wanawake tu.


Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Aprili 12,2022 Jijini hapa mara baada ya asubuhi kuiwasilisha ripoti hiyo bungeni, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (C.A.G) Chares Kichere amesema wanachama 444 waliopata huduma ya kuchunguzwa picha kamili ya damu (full blood picture) zaidi ya mara moja kwa siku moja (Hadi mara 30) kwenye kituo kimoja.


Kichere amebainisha kuwa kuwapo kwa malipo ya madai yaliyorudiwa, pamoja na madai yanayoonesha wanachama wa NHIF waliopokea miwani ya kusomea zaidi ya mara moja wakati utaratibu unaruhusu kutoa miwani mara moja kwa mwaka.


Amesema udhaifu huu umesababishwa na kukosekana kwa udhibiti katika mfumo wa madai iliyosababisha hasara ya Sh. Milioni 14.41 kwa mfuko.


“Ninapendekeza kwamba Mfuko wa Bima ya Afya(a) Kurejesha kiasi kilichopotea kutoka kwa watoa huduma za afya husika, na (b) Kuboresha mfumo wa madai wa CMIS ili kuhakikisha kuwa unasaidia maafisa wanaohusika kuangalia uhalali wa madai yaliyowasilishwa,”amesema


Katika Hatua nyingine amesema wamegundua kuwepo Kwa mashirika 14 ya kibiashara yanajiendesha kwa hasara likiwemo   Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) na  Shirika la Posta Tanzania (TPC).


Alieleza kuwa hali hiyo ilisababishwa na hasara kwenye uwekezaji uliofanywa,ufanisi duni wa mashirika husika na udhibiti hafifu wa mapato na matumizi.


Amesema kampuni ya ATCL kwa mwaka 2020-2021 imepata hasara ya sh. Milioni 36,499.20 na mwaka 2019-2020 ilipata hasara y ash.milioni 60.


C.A.G amesema Kampuni ya Biotech Production kwa mwaka 2020-2021 imepata hasara ya sh. Milioni 14,779.56 na mwaka 2019-2020 ilipata hasara ya sh.milioni 15,073.79.


Ameyataja Makampuni mengine yaliyojiendesha kwa hasara ni Kampuni ya Mkulazi,Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL),Kiwanda cha Kimataifa cha bidhaa za ngozi Kilimanjaro,(KILC),Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC),Shirika la uuzaji bidhaa Tanzania (EPZA).


Pia,Kampuni ya Kuzalisha nguo za umeme za zege Tanzania (TCPM),Shirika la Posta Tanzania (TPC),Kampuni ya Nyumba za watumishi (Watumishi Housing),Kampuni ya T-PESA kampuni tanzu ya TTCL,Kampuni ya uwekezaji ya PPF,DCC,Kampuni ya uchapishaji ya Chuo Kikuu Dar es salaam (DUP) na Kampuni ya Umeme ya Kikuletwa.


C.A.G amesema hati za ukaguzi zinaonesha katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kati ya hati 185 zinazoridhisha ni  178 zenye shaka sita,hati mbaya ni moja.


Amesema Mashirika ya umma 195 yenye hati zinazoridhisha ni 185 zenye shaka nane hati mbaya hakuna na kushindwa kutoa maoni mawili.


Kwenye Serikali Kuu amesema hati kati ya hati 308 hati zinazoridhisha ni 305 zenye shaka mbili,hati mbaya moja na hakuna ambayo imeshindwa kutoa maoni.


Amesema Halmashauri zilizopata hati zenye mashaka ni ya Wilaya ya Kisarawe,Longido,Mlele,Musoma,Halmashauri ya Sengerema na Bunda.


Kwa upande wa Mashirika ya Umma ameyataja yenye hati zenye mashaka ni pamoja na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Geita,Taasisi ya Mifupa Muhimbili,Mamlaka ya Bandari Tanzania,Kampuni ya Magazeti ya Tanzania,Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL).


Amesema kwa upande wa Serikali kuu,Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT) imepata hati yenye mashaka pamoja na Hesabu Jumuifu za Taifa huku Baraza la Madaktari Tanganyika (MCT) likipata hati mbaya.


Aidha,C.I.G amesema wakusanya mapato katika Mamlaka za Serikali za Mitaa 147 hawakuwasilisha benki makusanyo yanayofikia jumla ya shilingi bilioni 17.


Pia,Mawakala wa kukusanya mapato katika Mamkala za Serikali za Mitaa 12 hawakupeleka benki makusanyo ya shilingi bilioni 3.31 kinyume na mikataba yao.


“Ninapendekeza kwamba Tamisemi iongeze usimamizi wa mapato na kuhakikisha makusanyo yanapelekwa benki bila kuchelewa,”amesema.


Vilevile,amesema Mamlaka ya Serikali za Mitaa 24 zilitumia sh.milioni 664 katika matumizi yasiyo na manufaa kama vile malipo kwa riba na adhabu za kuchelewesha malipo na posho kwa watumishi wasiostahili.


Aidha,Mamkala za Serikali za Mitaa 61 ziliagiza na kulipa sh bilioni 8.44 kwa ajili ya bidhaa ambazo hazikuwasilishwa  na wazabuni kwa muda wa hadi kufikia miezi 24.


UPUNGUFU WA WALIMU KATIKA SHULE ZA MSINGI


Mkaguzi huyo alisema katika ukaguzi wake, Tathmini ya uwiano wa walimu na wanafunzi katika mamlaka 48 za serikali za mitaa na ilibainisha kuwa kati ya walimu 40,458 wanaohitajika kwa shule za msingi walikuwepo walimu 23,881 tu ikimaanisha upungufu wa walimu 16,571 sawa na asilimia 41.


“Hali hii inadidimiza juhudi za Serikali katika kuboresha elimu ya msingi na sekondari,”amesema Kichere.


UBADHIRIFU WA MAPATO YA SH. BILIONI 19.72 YA HALMASHAURI YALIYOKUSANYWA NA MAWAKALA NA WATUMISHI


Kichere amesema alifanya kaguzi maalumu 37 katika Halmashauri 36 na kubaini jumla ya Sh. bilioni 19.72 zilikusanywa kutoka vyanzo mbalimbali lakini hazikupelekwa benki; kati ya hizo, kiasi cha Sh. bilioni 10.13 (asilimia 51) zinahusiana na iliyokuwa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala.


Amefafanua kuwa kati ya Sh. bilioni 10.13, Sh. bilioni 4.64 hazikupelekwa benki na mawakala 20 wakati kiasi cha Sh. bilioni 5.49 hakikupelekwa benki na watumishi 19 waliokuwa wakikusanya mapato.


“Ninapendekeza Serikali ichukue hatua stahiki kwa watumishi na mawakala waliosababisha hasara hiyo na kuhakikisha kiasi hicho kinarejeshwa,”amesema.


USIMAMIZI WA RASILIMALI WATU NA MISHAHARA


Amesema Mamlaka za serikali za mitaa 25 zililipa Sh. milioni 556.84 kwa watumishi waliostaafu, waliofariki, waliotoroka, walioachishwa kazi na watumishi waliokuwa likizo bila malipo.


Kichere amebainisha kuwa Mamlaka za Serikali za Mitaa tano zilitozwa Sh. bilioni 180.70 kama adhabu kwa kushindwa kuwasilisha makato ya watumishi kama michango kwenye Mfuko wa Hifadhi ya Jamii ya Watumishi wa Umma, Mfuko wa fidia kwa Wafanyakazi, Kodi ya mapato na Bima ya Afya.


Mkaguzi huyo amefafanua kuwa ulipaji wa mishahara kwa watumishi wasiostahili husababisha upotevu wa fedha za Umma.


Pia, amesema kutopeleka makato ya kisheria ya watumishi kwa wakati huvutia tozo ambayo ni malipo yasiyo na manufaa.


“Ninapendekeza OR-TAMISEMI izisimamie mamlaka za serikali za mitaa kuepuka kulipa malipo ya mishahara yasiyokuwa na manufaa pia iwasiliane na hazina ili kupeleka michango ya kisheria kwa wakati kwenye Mifuko ya Pensheni na kuepusha tozo zisizo za lazima na kuhakikisha malipo ya mishahara ya wafanyakazi kwa watumishi wanaostahili,”amesema Kichere.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com