Kulia ni mwakilishi wa Mbunge ambaye pia ni Diwani viti maalumu Bi. Ziyuni Hussein Kajaja akikabidhi futari kwa Sheikh wa Wilaya ya Biharamulo Hamza Khatib Hamza aliye vaa kanzu nyeupe
Sehemu ya futari aliyotoa Mbunge wa Jimbo la Biharamulo Magharibi Mh. Ezra John Chiwelesa
Mbunge wa Jimbo la Biharamulo Magharibi Mh. Ezra John Chiwelesa
**
Na Mbuke Shilagi Kagera.
Zikiwa zimesalia siku chache kutamatika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ambapo Waislamu wote Duniani wakiwa wanaendelea na Ibada hiyo, Mbunge wa Jimbo la Biharamulo Magharibi Mhe Eng. Ezra John Chiwelesa atoa futari kwa wanajibo lake.
Ukiwa ni utaratibu wake wa kila Mwaka tangu awe Mbunge wa Jimbo hilo, Mbunge huyo amekuwa akiungana na Waislamu katika mfungo huu kwa kuwafuturisha kwa kadiri ya anachowezeshwa na Mwenyezi Mungu.
April 26, mwaka huu amekabidhi futari ambayo imesheheni tende box 25, mafuta ya kupikia Lita 10 ndoo 25, mchele kilo 25 Mifuko 25, unga sembe kilo 25 Mifuko 25, Ngano kilo 25 Mifuko 25 pamoja na Maharage kilo 10 Mifuko 25.
Akiongea mara baada ya kukabidhi swadaka hiyo, mwakilishi wa Mbunge na diwani wa viti maalumu Mh. Ziyuni Hussein amesema kuwa futari hiyo imetolewa na Mbunge kwa lengo la kuwafuturisha Waislamu wote wa Wilaya ya Biharamulo ambao uongozi wa dini hiyo utaona wanastahili kupata.
Ziyuni ameongeza kuwa Mbunge anaungana na waumini katika mfungo huu licha ya kuwa yupo Bungeni akiendelea na majukumu ya kuwawakilisha wananchi.
Kwa upande wake Sheikh wa Wilaya ya Biharamulo Hamza Khatib Hamza amemshukuru Mbunge huyo kwa utaratibu aliojiwekea wa kuwafuturisha Waislamu wa Jimbo lake.
Sheikh Hamza amesema kuwa futari ya Mwaka huu imekuwa kubwa kulinganisha na Mwaka Jana ambapo amesema kuwa na wao wataigawa kwa wahitaji kwa uadilifu mkubwa.
Ameongeza kuwa jambo linalofanywa na Mbunge Eng. Ezra ni jambo la kuigwa na Watu wengine huku akitoa wito kwa watu wengine taasisi na wale wenye uwezo kurudisha kile wanachopata kwa wale wenye mahitaji.