Kaimu Mkurungenzi wa Idara ya habari-Maelezo Rodney Mbuya akiongea na Waandishi wa habari kuhusu maashimisho ya siku ya uhuru wa habari na kueleza kuwa siku hiyo ni muhimu kwa kuwa ina enzi tasnia ya habari
Na Dotto Kwilasa,Malunde 1 Blog-DODOMA
IDARA ya Habari-Maelezo imemtaja Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuwa mgeni rasmi kilele cha maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari ambayo kitaifa yatafanyika Mei 3,2022 Jijini Arusha.
Kaimu Mkurungenzi Idara ya habari-Maelezo Rodney Mbuya amesema hayo leo Jijini Dodoma wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu tuzo za siku ya uhuru wa wa vyombo vya habari na kueleza kuwa uwepo wa tuzo hiyo ni utambuzi wa umuhimu wa vyombo vya habari.
Amesema,tuzo hizo ni maalumu kwa ajili ya waandishi wa habari na wataalamu wa mawasiliano,vyombo vya habari,wamiliki wa vyombo vya habari,ujumbe wa kidemokrasia na mashirika ya maendeleo ambayo yamekuwa na mchango mkubwa katika kuchagiza maendeleo kupitia majukwaa mbalimbali.
Ameyataja makundi ya tuzo hizo kuwa ni tuzo za kijamii,Sayansi na Teknolojia,utalii na uwekezaji,wamiliki bora wa vyombo vya habari,michezo na burudani,mwandishi ajaye,mwanahabari mwanamke mwenye mafanikio katika tasnia ya habari,vyombo vya habari vya kidigitali,ushirikiano,malengo ya maendeleo endelevu na mtangazaji bora wa Serikali na Umma.
Akifafanua kuhusu tuzo za Sayansi na Teknolojia amesema ni maalum kwa ajili ya kampeni za uandishi wa habari na vyombo vya habari ambazo zimesawiri kwa ufanisi maendeleo ya bidhaa za kiteknolojia, maendeleo ya teknolojia mpya, miundombinu muhimu na teknolojia zinazochochea mabadiliko ya digitali.
"Mshindi wa kategoria hii ni mwandishi wa habari au vyumba vya habari,tuzo hizo zitaonyesha mchango na thamani ya vyombo vya habari duniani na utaenziwa,pia katika tuzo ya utalii mshindi ataonyesha uwezo wa kuandika stori na fursa ya kuwasilisha mvuto wa kipekee wa mahali alipotembelea au uzoefu wa safari,"amefafanua
Kaimu Mkurugenzi huyo pia amefafanua katika kipengele cha wamiliki wa vyombo vya habari kuwa kitawatambua wamiliki waliotoa mchango mkubwa kwenye tasnia ya habari kupitia mipango bora ya maudhui ya vyombo vya habari,kampeni maalum,hafla au matangazo mengine yanayotokana na ushirikiano yaliyoibua fikra mpya na ubunifu katika nyanja ya habari.
Baadhi ya waandishi wa habari wakisikiliza kwa makini Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa habari-Maelezo (hayupo pichani)leo Jijini Dodoma wakati akieleza kuhusu tuzo za uandishi wa habari na kutaja makundi ya tuzo hizo ikiwemo Sayansi na Teknolojia na utaalii.
Social Plugin