Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SHIRIKA LA HUMULIZA LAPELEKA WASICHANA 1,269 VYUO VYA UFUNDI


Meneja Mipango wa Shirika la Humuliza lililopo Wilayani Muleba Mkoani Kagera Bi. Lightness Mpunga akitoa takwimu ya wasichana waliopelekwa vyuo vya Ufundi kwa mwaka 2020-2021
Mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Humuliza lililopo Wilayani Muleba Mkoani Kagera,Bw. Victor Nestory

Na Mbuke Shilagi Kagera.

Takribani Wasichana 1,269 wamepelekwa Vyuo vya ufundi kwa mwaka 2020-2021 na shirika la Humuliza wilayani Muleba Mkoani Kagera, kwa lengo la kupata ujuzi ambao utawawezesha kupata kipato kwa ajili ya kuendeshea maisha yao ya kila siku.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Humuliza Bw. Victor Nestory lililopo katika kijiji cha Bunyagongo kata ya Nshamba wilayani humo, wakati akizungumza na Malunde 1 Blog.

Amesema kuwa wasichana hao ni wale waliomaliza elimu ya msingi au sekondari na kushindwa kuendelea na masomo.

Bw. Nestory amesema kuwa wasichana walionufaika na mpango huo ni wale wanaoishi katika mazingira magumu, ambao hawawezi kuendelezwa kielimu na familia zao.


Mkurugenzi huyo ametaja mafunzo waliyopatiwa kuwa ni ya Ushonaji, Mapambo, Mapishi na Ufundi Seremala.


Ameongeza kuwa wasichana hao wamepelekwa katika vyuo tofauti tofauti kulingana na kozi wanazochukua ikiwemo Chuo cha Ufundi Stadi - VETA Kagera, VTC Karagwe, VTC Kagondo, Nyakato mkoani Mwanza na Sengerema.


Amesema baada ya kupata fani hizo Shirika la Humuliza linatoa vitendea kazi kwao, ili kuwawezesha kuendeleza kwa vitendo fani walizopata, na kutaja baadhi ya vitendea kazi hivyo kuwa ni vyerehani, vyombo vya mapishi, vifaa vya mapambo pamoja na vifaa vya uselemala.


Aidha Bw. Nestory ameongeza kuwa Shirika la Humuliza limekuwa likijihusisha na watoto kuanzia mwaka sifuri mpaka miaka 17 na vijana wanaoanzia miaka 18 mpaka 25 wasiojiweza, kwa kuwezeshwa kupewa elimu kwa watoto na kutoa mitaji kwa vijana ili kuwawezesha kupata pesa za kujikimu katika mahitaji mbalimbali.

"Tunatoa pia misaada ya kijamii na kisaiklojia kwa watoto wanaoishi katika mazingira duni wanaokuwa wamefiwa au kutelekezwa, na wanaoishi katika familia zenye migogoro, kwa kushirikiana na jamii inayowazunguka, lengo wapate mahitaji yao", amesema.

Amesema kuwa miradi ya Shirika hilo inatekelezwa katika wilaya saba zilizopo ndani ya Mkoa wa Kagera, ambayo imekuwa ikiwasaidia vijana wanaoishi katika Mazingira hatarishi pamoja na wale wanaoishi na maambukizi ya virusi vya Ukimwi, kwa kuwawezesha kupata elimu pamoja na kupatiwa dawa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com