Mfano wa jiko la mkaa
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Kagera, Maketi Msangi.
Wanandoa wawili wakazi wa mtaa wa Bunkango, Nshambya manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, maarufu kama mama Osward na baba Osward wamekutwa wakiwa wamefariki dunia ndani ya nyumba walimokuwa wakiishi usiku wa kuamkia jana, chanzo cha vifo hivyo kinatajwa kuwa ni jiko la mkaa.
Mwenyekiti wa mtaa wa Bunkango, Anath Abas amesema kuwa alipata taarifa kuwa mtoto wa wanandoa hao ameshindwa kwenda shule baada ya kugonga mlango wa chumba walimokuwa wamelala wazazi wake kwa muda mrefu bila mafanikio, na kuamua kutoa taarifa kwa jirani.
"Nilifika eneo la tukio nikagonga mlango haufunguliwi, nikaita hawaitiki, nikainama chini nikachungulia, nikamuona mama Osward amelala chini na mume wake amelala kitandani" amesema mwenyekiti huyo.
Amesema baada ya kuona pako kimya aliwaita viongozi wenzake pamoja na baadhi ya wananchi wakasukuma mlango kwa nguvu na kukuta tayari wanandoa hao wamepoteza maisha.
Diwani wa kata Nshambya na Meya wa Manispaa ya Bukoba Godson Gibson amesema kuwa baada ya kupata taarifa hizo kutoka kwa mtendaji wa kata yake, alitoa taarifa polisi kwa hatua zaidi, huku akiwaasa wananchi wake kuacha tabia ya kupikia ndani.
"Tumeambiwa mwanamke alirejea nyumbani usiku, akawasha jiko la mkaa na kumenya ndizi, na kisha kuingiza jiko hilo kwenye chumba kisha wakafunga mlango na madirisha na kupumzika" amesema Godson Gibson.
Akizungumza kwa njia ya simu Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Kagera, Maketi Msangi amekiri kuwepo kwa tukio hilo, na kwamba uchunguzi wa awali umeonesha kuwa vifo vya wanandoa hao vimetokana na jiko la mkaa.
"Uchunguzi wa awali umeonyesha vifo vyao vimetokana na kuvuta hewa yenye sumu inayotokana na mkaa, lakini tunasubiri uchunguzi wa kitabibu ili kujiridhisha kama kweli hicho ndo chanzo cha vifo hivyo na baada ya hapo miili ya marehemu itakabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya mazishi" - Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Kagera, Maketi Msangi.