Kutokana na uhodari huo, Nabii Dkt. Joshua amewatoa shaka waliodhania Mheshimiwa Rais asingeweza kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi ambapo amesisitiza Watanzania wote waendelee kumuunga mkono na kumpa ushirikiano wa dhati.
Sambamba na kumuombea ili azidi kulitumikia taifa kwa ufanisi mkubwa, kwani nafasi hiyo ya Urais anayohudumu amepewa na Mungu na kwamba Mungu ameiangazia njia yake ya uongozi mwanga mzuri wa kuliletea mafanikio makubwa taifa na wananchi kwa ujumla.
Nabii Dkt. Joshua ambaye pia ni Kiongozi Mkuu wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania yenye makao yake makuu mjini Morogoro ameyasema hayo leo Aprili 19,2022 wakati akizungumza na waandishi wa habari kueleza mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia na mikakati waliyonayo kama mitume na manabii katika kufanikisha juhudi mbalimbali za kuliletea Taifa maendeleo.
Pamoja na mambo mengine, Nabii Dkt.Joshua amebainisha kuwa, Umoja wa Mitume na Nabii nchini utaendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali katika kutoa mchango wa maendeleo ya nchi ikiwemo kusaidia ujenzi wa huduma za kijamii kama vituo vya afya na elimu kama ambavyo baadhi ya taasisi za dini zilizotangulia likiwemo Kanisa Katholiki ambalo limefanikiwa kufanya hivyo kwa ufanisi.
Amesema,umoja huo umedhamiria kuchagiza maendeleo ya nchi kupitia ujenzi wa viwanda ambavyo vitasaidia kutoa ajira kwa vijana na kuhamasisha Watanzania wazidi kujituma kufanya kazi mbalimbali halali za maendeleo katika kuunga mkono jitihada za maendeleo zinazofanywa na Serikali inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.
Nabii Dkt. Joshua pia amesema miongoni mwa majukumu aliyonayo baada ya kuchaguliwa kuwa Rais wa Umoja wa Mitume na Manabii nchini, ni kuhakikisha anawaunganisha Mitume na Manabii kusudi wawe pamoja na kwamba umoja wao uwe na tija kwa nchi ikiwemo kuhamasisha maadili mema, kuendelea kuliombea Taifa, kufundisha mafundisho ya kiroho kwa kuzingatia kikamilifu misingi ya Neno la Mungu.
Pia, Nabii huyo amewataka Mitume na Manabii nchini, kujiepusha na tabia mbaya ikiwemo kutumia vipawa walivyopewa bure na Mungu kuvitumia kama kitega uchumi na kwamba wazingatie misingi ya Neno la Mungu, kwani vipawa hivyo wamepewa bure, hivyo wavitumie bure.
Huku akiwaonya Mitume na Manabii wenye nia ovu na wanaochafua imani kuacha kufanya hivyo badala yake wasimamie kweli ya Neno la Mungu.
"Msingi wa Biblia tumepewa bure vipawa, vipawa vimetolewa na Mungu tuvitumie bure havina chuo tuvitumie bure. Ni kosa kubwa Mtumishi wa Mungu kuuza kipawa, msingi wa wokovu wetu ni upendo ni vizuri watumishi wa Mungu turithi tabia ya mwanzilishi wa imani yetu Yesu Kristo. Sisi Mitume na Manabii tunajipambanua kwa watu kwa kutoa faraja la suluhisho la matatizo yao na siyo kuleta hofu." amesema Nabii Dkt.Joshua.
Ameongeza kuwa, chombo hicho kitasaidia kutoa ushirikiano kwa Serikali katika kudumisha amani kwa njia mbalimbali ikiwemo kuelimisha jamii kujiepusha na matendo yote maovu,kabla sheria za nchi hazijafuata mkondo wake.
Social Plugin