Mwenyekiti wa halmashauri ya Arusha, Mhe. Ojung'u Salekwa akiwa watoto waalioletwa Kliniki kwenye zahanati ya Imbibya kata ya Mwandet, kuonyesha hali ya upatikanaji huduma za afya kwenye maeneo ya vijijini.
Na Rose Jackson,Arusha
Jamii imetakiwa kuwahudumia kina mama wajawazito na watoto kwa kuhakikisha wanahudhuria kliniki kipindi chote cha ujauzito, sambamba na kuwapatia lishe bora, huku wakisisitizwa wajawazito kujifungulia kwenye vituo vya kutolea huduma za afya na sio nyumbani.
Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti halmashauri ya Arusha, na Diwani wa Kata ya Laroi, Mhe. Ojung'u Salekwa, alipotembelea zahanati ya Imbibya kata ya Mwandeti, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo na hali ya upatikanaji wa huduma za afya katika vituo vya afya vya halmashauri hiyo.
Mwenyekiti Ojung'u licha ya kuridhishwa na upatikanaji wa huduma za afya katika vituo vya afya vya serikali katika halmasahuri hiyo, lakini pia amebaini changamoto za baadhi ya akina mama wajawazito kutokuhudhuri kliniki, wengine kujifungulia nyumbani, kutokuzingatia lishe bora kwa siku 1000 za ujauzito huku baadhi ya kinamama kuacha kuwapekeka kliniki watoto wa kabla ya kutimiza umri wa miaka mitano.
"Tunapaswa kutambua kuwa, suala la ujauzito ni la familia na jamii nzima, hivyo ni vema wote kuzingatia kumlea mjazito kwa kuhakikisha anahudhuria Kliniki mara anapohisi ana ujauzito, kumpa lishe bora kwa siku 1000 za ujauzito pamoja na kujifungulia kwenye vituo vya kutolea huduma za afya na si nyumbani, na baadaye kiwapeleka watoto kliniki mpaka watakapofikisha umri wa miaka mitano" ,amesisitiza Ojong'u.
Aidha Ojung'u amesisitiza kuwa serikali inaendelea kutekeleza mkakati wa kufikisha huduma za afya karibu na wananchi na zaidi imewekeza nguvu nyingi katika kuboresha miundombinu ya afya na kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba umeimarika, hivyo amewasisitiza wananchi kutumia huduma hizo kwa kuwa zinapatikana katika maeneo yao sasa.
Naye mama Yohana, aliyemleta mtoto wake kliniki, zahanati ya Imbibya, amesema kiwa kwa sasa jamii yao ya kimaasai imepata uelewa mkubwa wa kuhudhuria kliniki na kujifungulia hospitali jambo ambalo hapo awali halikiwepo kabisa.
"Kwa sasa akina mama wengi tunajifungulia hospitali, zahanati yetu ya Imbibya inatoa huduma zote za afya ya uzazi, tunapewa ushauri wa masuala ya lishe, kujikinga na magonjwa, niwashauri kina mama wajawazito wote wa Mwandeti, kuhudhuria kliniki, kujifungulia hospitali pamoja na kuwapeleka watoto klini mpaka watakapofikia miaka mitano, jambo ambalo linahakikishia afya ya mama na mtoto", amesisitiza mama Yohana.
Hata hivyo Mratibu wa Afya ya Uzazi, Muuguzi Bujiku Butolwa amewasisitiza wajawazito kuhudhuria klini na wenza wao, ili wote kwa pamoja wafahamu maendeleo ya afya ya mama na mtoto aliyeko tumboni, pamoja na kupata elimu na ushauri wa utunzaji na ukuaji wa mimba.
Pia mtatibu huyo, amefafanua umuhimu wa mama mjamzito kuhudhuria kliniki kwa wakati ni pamoja na kupata dawa muhimu za kuongeza damu, kuzuia minyoo na malaria, kupima vipimo muhimu, kama uuna tatizo litatuliwe mapema, vipimo hivyo Ni wingi na group la damu, kupata elimu ya Lishe wakati wote wa ujauzito.
"Ni jukumu la familia kumuwezesha mama mjamzito kuhudhuria kliniki kipindi chote cha ujauzito, kumuwahisha kituo cha afya pindi anapohisi uchungu wa kujifungua, ni hatari mjazito kujifungulia nyumbani anaweza kupoteza maisha yake na mtoto, ni vema familia nzima kumtunza na kumsaidia mama mjamzito kujifungulia hosoitali" ,amesisitiza Mratibu huyo wa Afya ya Uzazi.
Halmashauri ya Arusha ina jumla ya hospitali 2, vituo 7 vya afya na zahanati 49, huku kukiwa na huduma za mkoba 'mobile clinic', vituo hivyo vyote vinatoa huduma zote za afya na uzazi, kwa kina mama wajawazito na watoto.
Social Plugin