Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akiongea na wadau wa Afya ya mama na mtoto leo Dodoma kwenye uzinduzi wa Mfumo wa kielektroniki wa Kitaifa wa usafirishaji wa dharura kwa wajawazito na Watoto wachanga unaitwa M_mama unaolenga kupunguza vifo vitokanavyo na ujauzito.
****
Na Dotto Kwilasa,Malunde 1 Blog-DODOMA
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amezindua Mfumo wa kielektroniki wa Kitaifa wa usafirishaji wa dharura kwa wajawazito na watoto wachanga huku akiitaka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kukamilisha haraka iwezekanavyo mpango wa sheria za kulinda taarifa binafsi mtandaoni.
Rais Samia, amebainisha hayo leo jijini Dodoma kwenye uzinduzi wa kitaifa wa mfumo wa usafirishaji wa dharura kwa wajawazito na watoto wachanaga wa M-Mama)wenye lengo la kuboresha huduma za mama na mtoto nchini.
Amesema,kwa vile mfumo huo utahusisha ukusanyaji wa taarifa za watu binafsi unapaswa kuwa na usiri wa kipekee Ili kulinda faragha na kwamba sio taarifa zinakusnywa na kukutwa kwenye mitandao ya kijamii zinasambaa.
Pamoja kuanzishwa kwa mfumo huo wa M-mama RAIS Samia amesema serikali itaendelea kuhakikisha maeneo yote yanakuwa na magari ya kubeba wagonjwa angalau kila kata gari moja.
“Tumeagiza ‘ambulance’ 233 za kawaida ambazo zitamwangwa Tanzania nzima lakini pia tumeagiza ‘ambulance’ 25 ambazo ni ‘advance’ hizi ni kama ngazi ya rufani kama zile zinakuwa hazitoshi au hazina vifaa basi hizi 25 zitatumika lakini pia tumeagiza magari 242 ya uratibu ,
Ni matumaini yangu kwamba magari na ambulance hizi zitakwenda kuongeza nguvu kwenye huu mpango wa m-mama ili kuwawahisha watoto na kina mama mahospitalini”,amesema
Rais Samia pia ameiagiza Wizara ya Afya kufanya haraka kuiangalia mifumo inayotumiwa na Bohari ya Dawa nchini (MSD) hasa katika mfumo wa ufuatiliaji dawa tangu inapotoka hadi pale inapomfika kwenye vituo.
“Naomba niwaahidi watanzania kutoa au kujenga kasi ya mfumo wa huduma bora za afya,tumeanza kulifanyia kazi hilo kutoa huduma bora za afya kama alivyosema waziri wa afya, tumeanza na ujenzi wa miundombinu ambapo vituo kadhaa ngazi ya vijiji,kata,wilaya na ngazi za mikoa na kazi ya kununua na kusambaza vifaa tiba inaendelea.
Upatikanaji wa dawa tumetoa mabilioni kwa ajili ya ununuzi wa dawa lakini kuna mapungufu na juzi nilipotoa agizo kwa wizara ya afya kuangalia masuala ya mifumo nilitoa pia agizo la kuangalia MSD, kwa haraka sana najua sehemu moja ni yangu na nakuahidi kwamba nitaifanya kwa haraka.
Lakini kwenye mifumo ya kutoa huduma ni sehemu yako naomba mkaifanyie kazi haraka sana na zaidi ule mtandao wa kufuatilia dawa mpaka pale inapofika ukiharakishwa itakuwa vizuri zaidi”,amesisitiza Rais Samia
Aidha amesema serikali imejitahidi kuajili watumishi katika sekta ya afya ambapo kwa mwaka jana jumla ya watumishi 3,600 waliajiriwa.
“Na kwa mwaka huu uchumi wetu umeturuhusu kuajiri watumishi 32,000 ndani ya taifa letu ambao kati hizo nyingi zitakwenda katika sekta ya afya na elimu bila shaka”amesema
Rais, Samia aliipongeza kampuni ya simu za mkoani ya Vodacom kwa kuwezesha mfumo huo wa m-mama ambao utasaidia kuratibu usafiri kwa ajili ya wajawazito na watoto wachanga kupitia magari ya kubeba wagonjwa yalisajiliwa na magari binafsi.
Kwa upande wake Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amempongeza Rais Samia kwa jitihada ambazo amekuwa akizifanya katika kuboresha sekta ya afya kwa kutoa kiasi kikubwa cha fedha na kueleza kuwa hivi sasa wanapanga kufanya mazungumzo na kampuni ya Vodacom ili kutengeneza mfumo utakao saidia kufuatilia usambazaji wa dawa kutoka MSD hadi katika vituo vya afya.
“Naomba niweke wazi,Serikali imetoa kiasi kikubwa sana cha fedha hadi sasa umetupatia takribani bilioni 200 za dawa lakini changamoto kubwa ni dawa zinaonekana kwenye makaratasi lakini katika vituo bado watu wanalalamikia kukosa dawa hivyo sasa tunakwenda kutengeneza mfumo amabo utafuatilia dawa ambao utakuwa unaonyesha zilipotoka hadi ile hatua ya mwisho”,alisema.
Naye Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema uamuzi wa Rais Samia wa kuunda Wizara inayojitegemea yenye msisitizo wa Tehama ndio iliyotengeneza msingi wa haya yanayoonekana leo na kwamba lengo la serikali ni kutekeleza mpango wa m-mama nchi nzima ili kukomesha vifo vya wajawazito na watoto wachanga,"amesema.
Sehemu ya wadau wa Afya ya mama na mtoto wakifuatilia hotuba ya Rais Samia kuhusu mpango wa M_mama unaotekekezwa na Serikalà kupitia Kampuni ya simu za mkononi Vodacom unaolenga kuongeza nguvu ya kurahisisha huduma ya mama na mtoto
Social Plugin