Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa Mwanza kwa kushirikiana na shirika la kutetea haki za wanawake na watoto (KIVULINI) limeendesha kongamano la kuhamasisha maadili katika jamii wilayani Misungwi ili kusaidia kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Kongamano hilo limefanyika Jumamosi Aprili 16, 2022 katika Msikiti Mkuu wa Waslamu Misungwi na kuhudhuriwa na waumini mbalimbali wa dini hiyo ambapo lengo ni makongamano ya aina hiyo kufanyika katika Wilaya zote za Mkoa Mwanza.
Sheikh wa BAKWATA Mkoa Mwanza, Sheikh Hassan Kabeke amesema kongamano hilo la Malezi Bora, Tabia Njema na Misingi ya Ndoa linalenga kujadili na kuandaa mapendelezo yatakayoeleza sababu za kuporomoka kwa maadili katika jamii na kuwasilishwa serikalini kwa ajili ya hatua za utekelezaji.
Amesema kuporomoka kwa maadili katika jamii kunasababisha ufa katika ndoa ambapo matokeo yake ni kuibuka kwa wimbi la watoto wanaokimbilia mtaani kwa sababu ya kukosa malezi bora.
Sheikh Kabeke amekemea tabia ya wazazi hususani akina baba kukosa muda wa kulea watoto akisema wako ‘busy’ na kuacha watoto kulelewa na akina mama pekee ambapo matokeo yake ni kuibuka kwa ufa uitwao liwatwi (ulawiti).
“Baada ya maadili kuporomoka, watoto wadogo wa kindagaten, shule za Msingi, Sekondari na vyuo wanaangukia kwenye hatari ya kuingiliana kinyume na maumbile, mbaya zaidi imefika hatua baadhi ya familia wanawaalika hadi mashoga kusherehesha sherehe zao, je ni kweli tumeupokea ushoga? (sauti zinasikika hapa), huo ni ufa kwenye ndoa”, ameonya Sheikh Kabeke.
Sheikh Kabeke ameongeza kuwa kukosekana kwa maadili katika jamii pia kumesababisha unyanyasaji wa kijinsia kwenye ndoa ambapo imekuwa kawaida mme kumnyanyasa mke na mke kumnyanyasa mme.
“Imefika mahali wanaume hawafanyi kazi wanabaki kwenye kahawa, wanawake ndio asubuhi utakutana nao kwenye daladala wanahangaika na mabeseni kwenda kutafuta hela ya kutunza familia, mme akirudi jioni anaanza kuhoji chakula”, Sheikh Kabeke amekemea tabia hiyo akiwataka wanaume kuwajibika katika ndoa zao.
Pia Sheikh Kabeke ametoa rai kwa wanandoa kuwa na muda wa kukaa pamoja na kuzungumza masuala ya kulea familia, akisema “Mwanamke anatumia kanga kufikisha ujumbe kwa mmewe kwa sababu hakuna muda wa kuongea, inabidi avae kanga, utamaliza mabucha yote lakini nyama ni ile ile. Hivi ni sawa tuwasiliane kwa mfumo huo wa kanga? Tena ndoa za kiislamu? Wanandoa wanawekeza muda mwingi kwenye simu kuliko kukaa pamoja na kujadili masuala ya ndoa.
Katika hatua nyingine Sheikh Kabeke amelipongeza shirika la KIVULINI kwa jitihada zake kubwa za kusaidia kurudisha maadili kwenye jamii, kuwasiaidia watu waliodhalilishwa na wenye matatizo mbalimbali yanayohusiana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
“Mungu awape nguvu tuzunguke nao Mkoa mzima wa Mwanza. Tunataka baada ya Ramadhan tutoke na andiko litakalosaidia maadili katika ndoa kwani sisi BAKWATA tunapinga watoto wa mitaani, Kivulini wanapinga na Misungwi naamini mnapinga”, amesema Sheikh Kabeke.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la KIVULINI, Yassin Ally amesema wimbi kubwa la ndoa zinazofungwa mwezi wa Shaban linapaswa kujadiliwa kwani nyingi hazidumu na matokeo yake zinakuwa chanzo cha ongezeko la watoto wa mitaani.
“Unakuta mwanaume anatafuta mwanamke wa kumtumikisha, ampikie futari, akijinasibu kwamba funga yake itapokelewa. Inabidi wafungisha ndoa, masheikh wetu hili nalo tulijadili, huenda kuna mapungufu mengi katika misingi ya kuzilea na kuzifuatilia hizi ndoa ndio maana hazidumu”, amesema Ally.
Yassin pia amewasihi wanandoa kuishi kwa furaha na kutaniana kwani ukali umezidi miongoni mwa wanandoa tofauti na wapokuwa nje na nyumbani.
“Unakuta mwanaume akiwa kwa mama ntilie anamtania, leo umependeza ila akiwa kwa mkewe ni mwendo wa kumuamrisha, wewe njoo hapa, chakula kiko wapi” ,amedokeza Ally.
Lakini pia Ally amesisitiza kuwa jukumu la kulea watoto ni la wazazi hivyo ni vyema wakaishi kwa maelewano na kuwalea watoto katika misingi ya maadili inayozingatia kumcha Mungu, kuwapa haki za msingi ikiwemo kupata elimu kwani Serikali imeboresha mazingira ya kuhakikisha kila mtoto anakwenda Shule.
Kwa upande wake Sheikh wa Wilaya Misungwi, Sheikh Hussein Hussein amesema wanandoa wanapokuwa na uchumi imara, watoto wanaepuka hatari ya kukimbilia mitaani na hivyo kushauri vijana wa kiislamu kutobweteka na kuunda vikundi vya uzalishaji mali.
Baadhi ya washiriki wa kongamano hilo akiwemo mzee Hussein Manyilizu wamesema ndoa nyingi hazidumu kwa sababu vijana hukutana kwenye mitandao ya kijamii na kuoana tofauti na zamani ambapo wazee walikuwa wakifanya utafiti wa familia ya kuoa, akisema “siku hizi wanaangalia utajiri na siyo maadili, matokeo yake ndoa hazidumu”.
Naye Ibrahim Mhebi amewaasa vijana wenzake kufanya kazi badala ya kuamkia kwenye vijiwe vya kahawa na michezo haramu ya kubashiri kwani inadhorotesha uchumi wao na kuzikimbia familia. “Una elfu 50 unaamkia kwenye michezo ya ku-BET unaliwa yote, hapo ndoa Sheikh lazima uikimbie. Mimi naomba BAKWATA ije na mifumo ya kutusaidia vijana kujikwamua kiuchumi hatua itakayotusaidia kutunza familia” ameomba Mhebi.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Sheikh wa BAKWATA Mkoa Mwanza, Sheikh Hassan Kabeke (katikati) akifungua kongamano la Malezi Bora, Tabia Njema na Misingi ya Ndoa lililofanyika wilayani Misungwi. Kulia ni Sheikh wa BAKWATA Wilaya Misungwi, Sheikh Hussein Hussein na kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji shirika la KIVULINI, Yassin Ally.
Sheikh wa BAKWATA Wilaya Misungwi, Sheikh Hussein Hussein (kulia) akizungumza kwenye kongamano hilo. Katikati ni Sheikh wa BAKWATA Mkoa Mwanza, Sheikh Hassan Kabeke na kulia ni Mkurugenzi Mtendaji Shirika la KIVULINI, Yassin Ally.
Washiriki wa kongamano hilo ambao ni waumini wa dini ya kiislamu wakimsikiliza Sheikh wa Wilaya Misungwi, Sheikh Hussein Hussein.
Mkurugenzi Mtendaji Shirika la KIVULINI, Yassin Ally akichangia mada kwenye kongamano hilo lililoandaliwa na BAKWATA Mkoa Mwanza kwa kushirikiana na KIVULINI.
Washiriki wakifuatilia kongamano hilo.
Mmoja wa washiriki wa kongamano hilo, Ibrahim Mhebi akichangia mada kwenye kongamano hilo.
Kongamano hilo, pamoja na mambo mengine linalenga kuhamasisha wanajamii kuzingatia maadili bora, kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia na kusomesha watoto/ kuondoa utoro mashuleni ambapo baada ya kutamatika katika wilaya zote za Mkoa Mwanza, BAKWATA itaandaa mapendekezo yatakayowasilishwa serikalini kwa ajili ya utekelezaji.
Mmoja wa washiriki akichangia mada kwenye kongamano hilo.
Mshiriki akichangia kongamano hilo.
Washiriki wakiwa kwenye kongamano hilo lililofanyika katika Msikiti Mkuu wa BAKWATA wilayani Misungwi.
Jumbe mbalimbali kuhusiana na kongamano hilo.
Social Plugin