Mkurugenzi wa Petroli nchini Gerald Maganga akiongea na Waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu bei Kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli.
Na Dotto Kwilasa-Malunde 1 blog-DODOMA
MAMLAKA ya udhibiti wa huduma za nishati na maji (EWURA)imetangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli nchini kuwa zitaanza kutumika kuanzia kesho ,Jumatano,tarehe 6 Aprili 2022.
Mkurugenzi wa petroli nchini Gerald Maganga ameeleza hayo leo Jijini Dodoma wakati akiongea na Waandishi wa habari na kueleza kuwa Bei za rejareja na jumla za mafuta ya petroli ,dizeli na mafuta ya taa yaliyopokelewa Kupitia bandari ya Dar es Salaam zimeongezeka ikilinganishwa na toleo lililopita la 2 Machi ,2022.
Akiongea Kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa EWURA Mhandisi Geoffrey Chibulunje, Mkurugenzi huyo wa petroli nchini amefafanua kuwa kwa Aprili ,2022 bei za rejareja za petroli, dizeli na mafuta ya taa zimeongezeka kwa shilingi 321/Lita sawa na asilimia 21.45 mtawalia.
"Vilevile katika toleo lililopita bei za jumla za petroli, dizeli na mafuta ya taa zimeongezeka kwa shilingi 320.33/Lita sawa na asilimia 13.29, Shilingi 288.50/Lita sawa na asilimia 12.69 na shilingi 472.41/Lita sawa na asilimia 22.72 mtawalia,"amefafanua.
Akizungumzia mwezi Aprili,2022 Maganga amesema bei za jumla na rejareja kwa mafuta ya petroli na dizeli kwa mikoa ya Kaskazini ikihusisha Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara zimeongezeka ikilinganishwa na bei zilizotolewa 2 Machi,2022.
"Kwa mwezi Machi mwaka huu,bandari ya Mtwara imepokea mafuta ya dizeli tu hivyo kwa Aprili 2022 bei za rejareja na jumla za mafuta ya petroli kwa mikoa ya Kusini yaani Lindi na Ruvuma zitakuwa sawa na zile zilizotangazwa tarehe 2 Machi,2022,
Kwa upande wa dizeli kwa mwezi Aprili 2022,Bei za rejareja na jumla za dizeli zimeongezeka ikilinganishwa na toleo lililopita la mwezi uliopita ,bei ya rejareja ya dizeli imeongeza kwa shilingi 281/Lita sawa na asilimia 11.12 na bei ya jumla ya dizeli ikiwa imeongeza kwa shilingi 279.99/lita sawa na asilimia 11.67,"amefafanua.
Ameeleza kuwa kwa kuwa hakuna matanki ya kuhifadhia mafuta ya taa katika bandari ya Mtwara, waendeshaji wa vituo vya mafuta kwenye mikoa ya Kusini wanashauriwa kuchukua mafuta ya taa kutoka bandari ya Dar es Salaam na kwamba bei za rejareja za mafuta hayo katika mikoa hiyo itakuwa kulingana na gharama za kupokelea mafuta ya taa Kupitia bandari ya Dar es Salaam na gharama za usafirishaji mpaka mikoa husika.
"Mabadiliko haya ya rejareja yanachangiwa na kubadilika kwa bei za mafuta katika Soko la dunia, gharama za usafirishaji na thamani ya shilingi ukilinganisha na dola za Marekani,hivyo EWURA inaukumbusha Umma kwamba bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli kwa eneo husika zinapatikana pia Kupitia simu za mkononi Kwa kupiga namba *152*00#,"amefafanua
Social Plugin