Wanaume katika Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza wametakiwa kuacha tabia ya kwenda kuweka heshima baa wakitumia vibaya fedha nyingi na badala yake watumie fursa hiyo kujenga makazi bora na kuishi kwa upendo na wake zao.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la kutetea haki za wanawake na watoto KIVULINI, Yassin Ally alitoa rai hiyo Jumapili Aprili 17, 2022 wakati akiwasilisha mada kwenye kongamano la 'malezi bora, tabia njema na misingi ya ndoa' lililofanyika katika Msikiti wa BAKWATA wilayani Kwimba.
"Kuna baadhi ya wanaume msimu wa kilimo wanalima pamoja na wake zao, wakivuna wanapata kuanzia milioni mbili hadi tano kisha wanatokomea na hela kwenda kuweka heshima baa na kuhonga, kuanzia leo heshima ya kwanza iwe kujenga nyumba nzuri",alisema Ally.
"Unakuta mwanaume anatafuta sifa baa, mnadani ama kwenye vijiwe vya mpira wakati nyumbani ni chenga tupu, kaone anapolala utashangaa", alisema Ally akiwasihi baadhi ya wanaume wilayani Kwimba wasiowajibika kwa maendeleo ya familia kubadilika.
Pia aliwasihi wanaume kuishi kwa maelewano na wake zao na kuacha kauli tata zinazochochea migogoro kwenye familia na kusababisha kukosekana kwa malezi bora hususani kwa watoto na matokeo yake linaibuka wimbi la watoto wanaokimbilia mitaani.
Kwa upande wake Sheikh wa BAKWATA Mkoa Mwanza, Sheikh Hassan Kabeke alisema kukosekana kwa mafunzo kwa vijana kabla ya kuoana ni chanzo cha ndoa nyingi kukosa maelewano na kuvunjika na kusisitiza kuwa suala hilo litapewa kipaumbele.
"Hatuwezi kuwa na jamii ambayo haina mafunzo, tuanzishe mafunzo hata ya siku 14 kwa vijana kabla ya kufunga ndoa, lakini pia wanaofungisha ndoa hizo wahakikishe wanazifuatilia na kuzilea", alisisitiza Sheikh Kabeke.
Baadhi ya washiriki wa kongamano hilo akiwemo Amina Mussa na Maneno Hassan walisema walitoa rai kwa wanandoa hususani wanaume kurejea misingi ya dini, kuwa na utamaduni wa kusali ili wawe na hofu ya Mwenyezi Mungu jambo litakalosaidia kuishi kwa maelewano na kulea familia pamoja.
Kongamano hilo ni sehemu ya makongamano ya 'malezi bora, tabia njema na misingi ya ndoa" ambayo yameandaliwa na BAKWATA Mkoa Mwanza kwa kushirikiana na shirika la KIVULINI yakitarajiwa kufanyika katika Wilaya zote mkoani Mwanza kwa lengo la kuimarisha maadili katika jamii ili kuondokana na vitendo vya ukatili wa kijinsia, kulea familia na kuondoa watoto wanaokimbilia mitaani pamoja na kupambana na utoro mashuleni.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Mkurugenzi Mtendaji Shirika la KIVULINI, Yassin Ally akizungumza kwenye kongamano hilo.
Waumini wa dini ya kiislamu wakifuatilia kongamano hilo lililofanyika katika Msikiti wa BAKWATA wilayani Kwimba.
Sheikh wa BAKWATA Mkoa Mwanza, Sheikh Hassan Kabeke akizungumza kwenye kongamano hilo.
Washiriki wakifuatilia kongamano hilo.
BAKWATA kwa kushirikiana na KIVULINI wameandaa makongamano 'malezi bora, tabia njema na misingi ya ndoa' katika Wilaya zote mkoani Mwanza.
Mshiriki wa kongamano hilo, Amina Mussa akichangia hoja kwenye kongamano hilo ambapo aliwasihi wanaume kurejesha upendo kwa wake zao na kulea familia kwani wengi wao upendo umepungua ndiyo maana wanatelekeza familia.
"Tumetelekezewa majukumu ya kulea familia na wanaume" alisema Bi. Fatuma Idrisa wakati akichangia mada kwenye kongamano hilo ambapo aliwasili wanaume kuwa na upendo kwa wake zao ili kulea familia kwa pamoja.
Mshiriki wa kongamano hilo, Maneno Hassan aliwasihi wanawake kuwa na upendo wa dhati kwa waume zao hatua itakayosaidia kuishi kwa amani na furaha akisema "unampa mtaji wa biashara mkeo, siku mtaji wako ukikatika, yeye hawezi kukusaidia, hilo nalo ni tatizo".