Wanafunzi wa Uandishi wa habari wanaohudhuria mafunzo ya Sheria za vyombo vya habari yanayoendelea katika Chuo cha Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC)
Taasisi ya vyombo vya Habari Kusini mwa
Afrika tawi la Tanzania (MISA TAN) kwa kushirikiana na taasisi ya sheria ya
Marekani (ABA ROLI) inaendesha mafunzo ya sheria za vyombo vya habari nchini
kwa wanachuo wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC)
ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Mafunzo haya ya siku mbili yanayofanyika
chuoni hapo kwa kuwahusisha wanachuo wa shahada ya kwanza katika fani za
Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa ABA ROLI wa Kuhimiza Uhuru wa Kutoa
Maoni nchini Tanzania na Uganda.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo Afisa Habari na Utafiti wa MISA TAN, Bi. Neema Kasabuliro alieleza kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa Taasisi hiyo wa kukiaandaa vyema kizazi kijacho cha Wanahabari ili kuzielewa, kuzitafsiri na kuzitumia ipasavyo sheria mbalimbali zinazoongoza tasnia ya uandishi wa habari na mawasiliano hapa nchini Tanzania.
Mafunzo haya ni muendelezo wa utekelezaji wa majukumu makuu ya MISA TAN ya kutetea, kuhimiza na kulinda uhuru wa kujieleza na vyombo vya habari, na haki ya raia kupata taarifa.
“Tokea kuanzishwa kwake
MISA TAN imekuwa ikifanya kazi za uraghibishi na kuendesha kampeni mbalimbali zinazolenga
kuboresha sera na sheria zinazofifisha haki ya kikatiba ya kupata na kutoa taarifa.
Aidha, tunafanya tafiti kuhusu utekelezaji wa sheria hizo, hali ya uhuru wa
vyombo vya habari, pamoja na kufuatilia matukio ya uvunjaji wa haki tajwa
hususan dhidi ya Wanahabari”, alifafanua.
Katika mafunzo haya washiriki wataweza
kuongeza maarifa na uelewa wa sheria hizi na kanuni zake, vikwazo na vitisho dhidi
ya uhuru wa kujieleza, pamoja na kuzitumia katika utekelezaji wa kazi za
uandishi wa habari.
Social Plugin